Kwenye maisha yako kuna watu ambao ukikaa nao unapoteza kabisa hamasa uliyokuwa nayo na hata nguvu ya kuanza.

Labda umepata wazo zuri la kufanyia kazi, na unamwambia mtu ila anaanza kukuonesha kila sababu kwa nini wazo hilo haliwezekani. Atakupa kila mfano wa watu waliojaribu na wakashindwa. Ukitoka hapo huna tena hamasa ya kumwambia mwingine wazo hilo.

Kuna watu ukikaa nao wao ni kulalamika tu jinsi maisha ni magumu na kuanza kusema jinsi ambavyo maisha yatazidi kuwa magumu huko mbeleni. Kwa kukaa na watu hawa hata kama ulikuwa na mipango yako mizuri ya mbeleni unapoteza kabisa nguvu za kuifanyia kazi na kuona kama kila kitu hakiwezekani.

Watu hawa ni wanyonya nguvu na hamasa, ni watu hatari sana kwa sababu wana nguvu kubwa ya kukurudisha nyuma.

Fanya tathmini ni watu gani wanaokuzunguka ambao wana tabia kama hizi na waepuke kwa nguvu zako zote. Kama ni wazo jipya usiwape na unapokuwa nao wakaanza kutoa malalamiko yako ondoka haraka sana.

Unahitaji kuwa na hamasa na nguvu muda wote kwa sababu kuna changamoto nyingi zipo mbele yako. Usikubali wanyonya nguvu wawe sehemu ya changamoto hizo, waepuke haraka sana.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuna watu ambao wamekuwa wananinyonya nguvu zangu na hamasa niliyonayo. Kuanzia sasa nitakuwa makini na watu ninaowashirikisha mipango yangu mikubwa. Pia nitakuwa makini na wale wanaonizunguka, mtu yeyote ambaye muda wote analalamika na kuona mambo yatazidi kuwa magumu sitaruhusu akae karibu na mimi.

NENO LA LEO.

Kuna watu ambao ni wanyonyaji wa nguvu na hamasa. Watu hawa ukikaa nao muda mfupi tu, ukiondoka unajikuta huna tena hamasa wala nguvu ya kufanyia kazi malengo yako.

Watu hawa ni walalamikaji na wakatishaji tamaa, kuwa makini na watu wa aina hii kama unataka kufikia mafanikio makubwa. Weka mawazo yako kwenye kile unachoweza kufanya na siyo ambacho huwezi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.