USHAURI; Hatua Tatu Za Kufikia Utajiri Kwa Kuanza Na Kipato Kidogo Kabisa.

Moja ya vitu vikubwa ambavyo nimejifunza kwenye maisha yangu na ambacho kimenishangaza sana ni kwamba mafanikio ya mtu hayatokani na kipato ambacho anakipata. Ndiyo na hata mafanikio ya kifedha, yaani utajiri, hautokani na kipato mtu anachotengeneza, bali unatokana na nidhamu. Yaani kama hutakuwa na muda au uvumilivu wa kutosha kuendelea kusoma maneno zaidi ya elfu moja yaliyopo hapo chini, basi ondoka na hili, utajiri hautokani na kipato, bali utajiri unatokana na nidhamu. Basi.

 

Nina ushahidi mwingi mno wa kudhibitisha hili, na wala haupo mbali ushahidi huo, bali unaanzia hapo hapo ulipo. Jaribu kuwaangalia watu wanaokuzunguka, angalia watu unaowajua, labda unafanya nao biashara au unafanya nao kazi. Hebu waangalie wale ambao wamefika juu kwenye mafanikio ya kifedha, waangalie walianzia wapi. Wengi sana unakuta walianzia chini kabisa, walianza na kipato kidogo mno, wengine hata hawakuwa na kipato.

Lakini kwa nidhamu ya hali ya juu, wameweza kutoka chini mpaka juu na kutengeneza utajiri ambao wengine wengi wanautamani. Katika mazingira hayo hayo wapo watu ambao wanapata nafasi na fursa kubwa za kipato, lakini unashangaa wapo pale pale siku zote.

Linapokuja swala la fedha na utajiri, kuna nidhamu tatu ambazo kila mtu anapaswa kuwa nazo.
Ya kwanza ni nidhamu ya kudhibiti matumizi yako yasizidi kipato chako. Hapa ndipo wengi wanaposhindwa na kuzika kabisa ndoto zao za utajiri. Wengi wanaruhusu matumizi kuzidi kipato hivyo kinachotokea ni kuingia kwenye madeni, na ukishakuwa na madeni ambayo hayazalishi faida, umeshaagana na utajiri.

SOMA; Utajiri Wako Uko Sehemu Hii Moja Muhimu, Acha Kupoteza Muda Huko Uliko Sasa.

Nidhamu ya pili ni kuweka akiba, hutakuwa tajiri kwa kipato unachotengeneza kila siku, bali utakuwa tajiri kwa uwekezaji unaofanya. Kabla hujawekeza unahitaji kuweka akiba, halafu akiba hii ndipo unaiwekeza sehemu ambapo inakuzalishia faida. Kama huwekezi huwezi kuwa tajiri, hata kama kipato chako ni kikubwa kiasi gani. Uwekezaji ni njia ya kuifanya fedha yako ikufanyie wewe kazi, fedha inakuwa mtumwa wako.

Nidhamu ya tatu ni kuongeza kipato chako. Kadiri siku zinavyokwenda matumizi yako yanaongezeka, huwezi tu kuendelea kujibana. Pia utahitaji kuongeza uwekezaji wako kila siku, hivyo unahitaji kuongeza kipato chako. Unahitaji kutumia kila fursa inayokuzunguka kuweza kuongeza kipato chako ili uweze kufikia utajiri.

Sasa rafiki yangu, kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO, tunakwenda kumshauri mwenzetu juu ya nidhamu hizi tatu ili aweze kutoka kwenye changamoto za kifedha na kuwa maisha ya mafanikio na hatimaye utajiri.

SOMA; Njia Nne Za Uhakika Za Kufikia Utajiri, Angalizo; Ajira Sio Mojawapo.

Kabla hatujampa mwenzetu ushauri, kwanza tupate maoni yake aliyotuandikia akiomba kushauriwa;

Samahani mimi kipato changu ni 350,000 natamani kupata maendeleo lakini nikijaribu kubajeti ile pesa inaishia kwenye matumizi. Je kwa hicho kipato changu nilicho nacho natakiwa nihifadhi ngapi ili malengo yangu tafadhali naomba ushauri, natamani nione mabadiliko. L. J. Baraka

Kama ambavyo tumeona kwenye utangulizi hapo juu, kwa kipato ambacho mwenzetu anacho, anaweza kukitumia kwa nidhamu ya hali ya juu na kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yake. 

Anachohitaji ni nidhamu, kisha juhudi na awe tayari kwa muda utakaohitajika ili kufika pale anapotaka yeye.

Yafuatayo ni mambo muhimu sana ambayo msomaji mwenzetu anapaswa kuyazingatia ili kutoka hapo alipo na kufikia mafanikio makubwa.
Kwanza; jilipe wewe mwenyewe kwanza.

Siri ya utajiri ni moja, jilipe wewe mwenyewe kwanza. Kwa kiasi chochote cha fedha unachopata, usikimbilie kuwalipa wengine na wewe ukabaki mikono mitupu, au kubaki na madeni. Badala yake anza kujilipa wewe mwenyewe kwanza.

Kiasi unachopaswa kujilipa ni angalau asilimia kumi ya kipato chako. Kwa mwenzetu ambaye kipato chake ni 350,000 basi kila mwezi anapaswa kujilipa 35,000. Na hii anayojilipa siyo kwa ajili ya matumizi, bali ni kwa ajili ya akiba ambayo baadaye ataitumia kwa uwekezaji.

Ni muhimu sana kuhakikisha kila fedha unayoipata, unajilipa wewe mwenyewe kwanza. Hii ni nidhamu muhimu kujijengea, na usiangalie ni kiasi gani umepata, tumia sheria hii kuanza kujenga misingi yako ya utajiri.

Pili; mapato yako yasizidi kiasi kinachobaki baada ya kujilipa wewe mwenyewe.

Umeshajilipa asilimia 10 ya kipato chako, sasa umebaki na asilimia 90. Sasa hakikisha matumizi yako hayazidi sehemu ya kipato chako iliyobaki. Hakikisha matumizi yako yanakuwa chini ya fedha uliyobaki nayo baada ya kutoa makato mengine yote.

Na ninajua hapa ndipo pagumu kuliko sehemu nyingine zote, kwa sababu kwa kipato kidogo, ni jambo ambalo linaonekana haliwezekani. Lakini ugumu huu ndiyo muhimu kwako ili utoke hapo ulipo. Unahitaji kupata hasira ya kukusukuma kuondoka hapo ulipo sasa.

Kuendelea kuishi maisha ambayo ni juu ya uwezo wako, ni kujidanganya kwamba una uwezo na akili yako kutulia. Lakini utakapoanza kuishi maisha halisi ya uwezo wako, akili yako haitaweza kutulia, hivyo utajikuta ukifikiri zaidi na kutumia kila nafasi inayojitokeza mbele yako.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Sumaku Ya Fedha, Njia Kumi (10) Za Kuivuta Fedha Ije Kwako Muda Wote.

Utakapokosa fedha ya kula na ukashinda au kulala njaa, utafikiria kwa kina namna ya kuyapeleka maisha yako.

Hivyo nakushauri sana, hata kama kipato chako ni kidogo kiasi gani, anza kuishi kwenye uhalisia wa kipato chako, ishi kulingana na kipato hicho na jizuie kabisa kwenda zaidi ya kipato ulichonacho. Maisha yatakapokuwa magumu kutokana na kutokutosheleza kwa kipato, utasukumwa kufanya vitu ambavyo awali uliona huwezi kuvifanya.

Tatu; ongeza kipato chako.

Kama ambavyo tumeona hapo juu, utapitia wakati mgumu mno wa maisha yako pale utakapoanza kuishi uhalisia wa maisha yako. Kuna vitu ulikuwa unavipata ila sasa hutavipata tena, kuna starehe ulikuwa unafanya ila sasa hutafanya tena. Na kuna namna ulikuwa unaonekana kwenye jamii yako ila sasa hutaonekana hivyo tena.

Hichi ni kipindi cha mpito tu, hakipaswi kuwa hivyo muda wote, badala yake unahitaji kujipanga kutoka hapo muda siyo mrefu. Na njia pekee ya kutoka hapo ni kuongeza kipato chako. Kama umeishi uhalisia wa kipato chako na maisha yamekuwa magumu, sasa hiyo iwe hasira ya wewe kuongeza kipato.

Kama upo kwenye ajira na kipato ni kidogo fikiria kuanzisha biashara ya pembeni, tafuta kitu chochote na kiuze, anzia chini kabisa, anza hata na kitu kimoja na kiuze, endelea kukua kwa kuanzia hapo.

Kama umejiajiri au upo kwenye biashara yako mwenyewe, ikuze zaidi biashara yako. Toa huduma bora zaidi na wafikie wateja wengi zaidi. Kwa chochote unachofanya, hakikisha unaongeza kipato chako, hata kama ni kwa kiwango kidogo sana.

Kama kuna kitu unakitaka kweli kwenye maisha yako na huwezi kukimudu kwa kipato ulichonacho sasa basi ongeza kwanza kipato ndiyo upate kitu hicho. Kwa kufanya hivi utakuwa na hamasa ya kuongeza kipato, na uzuri ni kwamba ukishapata njia moja ya kuongeza kipato, utaziona nyingi zaidi.

Hayo ndiyo mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kufikia mafanikio kwa kuanza na kipato kidogo. Yafanyie kazi kila siku, na kuwa mvumilivu, utapata matokeo bora kabisa kwenye maisha yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya juma tatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: