Ni watu dhaifu ambao wana roho mbaya na wanaofanya ukatili, roho nzuri na upole vinatoka kwa watu ambao ni imara. Watu dhaifu wanaona njia pekee ya kujiweka salama ni kuwafanyia vibaya wengine. Watu imara wanajua ukatili na roho mbaya havina malipo yoyote chanya kwao.
Ni watu dhaifu ambao hawawezi kusamehe na kukaa na kinyongo kwa muda mrefu. Kusamehe na kuachilia kunahitaji uwe imara. Watu dhaifu wanaona kusamehe wengine kunawashusha wao. Watu imara wanajua kusamehe ni kujiondolea mzigo mzito wao wenyewe.
Ni watu dhaifu ambao wanapanga kulipa visasi, kusamehe na kusahau inahitaji uimara. Watu dhaifu huona kulipa kisasi ndiyo njia ya kuwakomesha wengine. Watu imara wanajua kulipa kisasi hakuna msaada wowote kwao, chochote kilichotokea kimeshatokea.
Ni watu dhaifu ambao wanataka kupata zaidi ya wengine kwa njia ambazo siyo halali, hivyo huchukua hatua ya kuiba au kudhulumu ili kupata zaidi. Watu imara wanajua njia pekee ya kupata zaidi ni kuweka juhudi zaidi, na wanafanya hivyo.
Je wewe upo kwenye kundi lipi? La watu dhaifu au watu imara? Kama upo kwenye kundi la watu dhaifu amua kuondoka huko, kwa sababu utayakosa mengi mazuri kwa kuwa dhaifu. Na unaweza kuondoka, maamuzi ni yako wewe mwenyewe.
SOMA; Tabia Tatu Za Viongozi Dhaifu, Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba roho mbaya, ukatili, kutosamehe, kulipa visasi na kudhulumu wengine ni tabia za watu ambao ni dhaifu. Hawa ni watu ambao hawajiamini na hivyo kutumia njia ambazo siyo sahihi kuficha kutokujiamini kwao. Mimi ni mtu imara na sitajihusisha na tabia hizo za watu dhaifu.
NENO LA LEO.
Roho mbaya, ukatili, kutosamehe, kulipa visasi na kudhulumu wengine ni tabia za watu ambao ni dhaifu. Hawa ni watu ambao hawajiamini wao wenyewe na hivyo wanatumia njia ambazo siyo sahihi kuficha kutokujiamini kwao.
Inahitaji mtu imara kuwa na roho nzuri, kuwa mwema, kusamehe, kutolipa visasi na kuepuka kudhulumu wengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.