Tunaishi kwenye dunia ambayo mtu aliyekufa miaka 100 iliyopita, akifufuka leo ataona kila kitu ni kigeni. Maana miaka 100 iliyopita hakukuwa na kompyuta, simu za mkononi, mtandao wa intaneti, tv, redio na vingine vingi ambavyo kwa sasa tunavichukulia kama vitu vya kawaida. Mtu huyu akifufuka leo atashindwa kabisa kuamini kama hii ni dunia ile ile ambayo aliishi yeye.
Ninachotaka kusema hapa ni kwamba tunaishi kwenye wakati ambao fursa ni nyingi sana. Kila kinachotuzunguka ni fursa nzuri kwetu kukitumia kupata kile ambacho tunakitaka kwenye maisha yetu.
Lakini utawasikia watu wakisema, sijapata fursa nzuri. Tatizo siyo fursa kukosekana, bali tatizo ni unazitumiaje fursa zilizopo kwa sasa. Unatumiaje fursa ambazo zinakuzunguka hapo ulipo ndiyo tatizo.
Badala ya kusema kwamba fursa ni tatizo, hebu anza kuangalia kila kinachokuzunguka. Una kazi hebu anza kuiangalia unawezaje kuongeza thamani. Una biashara hebu angalia ni vitu gani unaweza kuboresha zaidi kwa wateja wako. Unataka kuanza biashara lakini hujui uanze biashara gani, hebu angalia ni kitu gani watu wanateseka kupata, au hawapati kwa ubora wanaostahili.
Fursa zipo kila mahali, ni wewe unazitumiaje fursa hizi katika kufikia malengo yako kwenye maisha.
SOMA; Huoni Fursa Za Mafanikio Kwa Sababu Hii Kubwa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba hakuna uhaba wa fursa, bali kuna uhaba wa kuchukua hatua juu ya fursa zilizopo. Kuna fursa nyingi zinazonizunguka kwenye maisha, lakini mimi sijazichukulia kwa uzito. Sasa naacha kulalamika juu ya uhaba wa fursa na ninachukua hatua kwa ile fursa ninayochagua kuifanyia kazi.
NENO LA LEO.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kuna uhaba wa fursa, hii siyo kweli, fursa zipo nyingi, uhaba upo kwenye utekelezaji.
Kila kinachokuzunguka ni fursa kwako kuweza kufikia maisha ambayo unayataka. Ni wewe uamue kuchukua hatua kwenye fursa hizo ndiyo utaona mabadiliko kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.