Tunapoona mafanikio ya wengine, huwa tunaona mafuriko. Tunaona jinsi mambo makubwa yanavyotokea kwao huku wakionekana hawaweki juhudi kubwa sana. Na sisi tunafikiria kwenye mlengo huo huo kwamba kama na sisi tutaweza kutengeneza mafuriko kama ya hao wengine, basi mambo yetu yatakuwa vizuri sana.
Ambacho hatuoni ni kwamba watu hawa hawakuanza na mafuriko, bali walianza na matone madogo madogo na wakaendelea bila ya kukata tamaa mpaka matone haya yalipojikusanya na kuwa mafuriko makubwa unayoona sasa.
Swali ni je inachukua muda na kiasi gani kwa matone kuwa mafuriko? Jibu ni muda mwingi na nguvu kubwa. Hivyo hiki ndiyo unachohitaji ili kufikia mafanikio.
Hivyo badala ya kupoteza muda kuandaa mafuriko, hebu tumia muda huo kutengeneza matone ambayo baadaye yataleta mafuriko. Hii ina maana badala ya kusubiri mpaka upate mtaji mkubwa ndiyo uanze biashara, hebu anza na mtaji mdogo ulionao na ukweke juhudi kwenye kukuza biashara yako. Badala ya kusubiri mpaka kipato chako kiongezeke ndiyo uweke juhudi kwenye kazi, hebu anza kuweka juhudi kidogo kidogo sasa na baada ya muda utakuwa mbali.
Chochote unachoangalia chenye mafanikio na kikakuvutia, jua kuna watu wameweka muda na juhudi mpaka kufikia hapo. Je na wewe upo tayari kuweka muda na juhudi hizo?
SOMA; KITABU; Kurasa Za Maisha Ya Mafanikio, Toleo La Kwanza 2016.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mafanikio hayaji kama mafuriko, bali matone madogo madogo ndiyo yanayotengeneza mafuriko ya mafanikio. Nimejua ninahitaji muda na kuweka juhudi ili niweze kupata mafanikio ninayotaka. Nipo tayari kwa hili na nitalifanyia kazi kila siku.
NENO LA LEO.
Mafanikio hayaji kama mafuriko, bali matone madogo madogo ndiyo yanatengeneza mafuriko ya mafanikio.
Usiache kuchukua hatua kwa sababu una kidogo, anza na kidogo ulichonacho na baadaye kitakuwezesha kufikia makubwa sana.
Jua unatakiwa kuweka muda na juhudi kubwa, hakuna kitu chenye thamani kinachokuja kwa urahisi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.