Moja ya changamoto ambazo wengi tunazipata katika safari hii ya mafanikio ni kukosa watu wa zuri wa kuwa mfano kwetu, kwa Kiingereza wanaitwa role models. Kimsingi unahitaji kuwa na mtu wa karibu ambaye ameshafanikiwa na anakupa hamasa na unaweza kuona kwa macho yako ni jinsi gani anafanya mpaka anafanikiwa.
Lakini jamii zetu zina watu wachache sana ambao wamefanikiwa na ambao wapo tayari kuwaonesha wengine jinsi wanavyofanya mpaka wakafanikiwa. Wengi wa wanaokuzunguka ni watu ambao wameshindwa na wameshakata tamaa. Hawapigani tena kufikia mafanikio na hivyo hawakupi hamasa wala huwezi kujifunza moja kwa moja kutoka kwao.
Lakini kuna njia nyingine ya kujifunza kuhusu mafanikio kutoka kwa watu hawa. Kwa njia hii utajua ni vitu gani ufanye au uepuke kufanya ili uweze kufikia mafanikio kwenye maisha yako. njia hii ni kwenda kinyume na wale ambao wameshindwa. Kwa kuwa wamekuzunguka na unawaona ni nini wanafanya na nini hawafanyi, basi wewe amua kwenda kinyume nao. Kwa njia hii utaepuka kupata yale matokeo ambayo wamepata wao.
Mambo ya kwenda kinyume ni mengi, hapa nakushirikisha machache;
- Wengi hawapendi kujifunza kwa kujisomea, basi wewe fanya kujifunza na kujisomea ni msingi wako.
- Wengi wanapenda kushabikia mambo bila ya kufikiri, kataa kushabikia jambo lolote ambalo huoni msingi wake au manufaa yake kwako.
- Wengi wanapenda kulalamika na kulaumu, kataa kata kata kulalamika au kulaumu, acha mara moja.
- Wengi wanapenda kuangalia tv na kusikiliza redio muda mwingi. Wewe acha kabisa kuangalia tv, au chagua vipindi vyako vichache, usizidishe nusu saa au saa moja kwa siku.
- Wengi wanapenda kushinda kwenye mitandao ya kijamii na kufuatilia maisha ya wengine, ambao nao wanaigiza. Acha kabisa kupoteza muda wako kwenye mitandao hii, tenga muda mfupi wa kupitia yale muhimu.
- Wengi wanategemea misaada, usitegemee kabisa msaada, pambana.
- Wengi hawapo tayari kujitoa na kufanya kazi kwa bidii, jitoe sana na weka juhudi kubwa kwenye kazi.
- Wengi siyo waaminifu, kuwa mwaminifu sana na mwadilifu pia.
- Wengi hawana nidhamu ya fedha, muda, jijengee nidhamu hizi muhimu.
- Wengi hawajiamini, wewe jiamini.
- Wengi wanapoteza muda wao kujadili watu na matukio, acha kabisa mambo hayo, usipoteze muda wako huko.
- Wengi wanapenda kuahirisha mambo, wewe fanya kila jambo kwa wakati uliopanga kufanya.
Angalia kile ambacho walioshindwa wanapenda kufanya na usikifanye, na kile wasichopenda kufanya, kifanye. Halafu fanya kwa muda mrefu, usikate tamaa wala usiwasikilize watakaokurudisha nyuma.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba nahitaji watu wa kuwaangalia ili niweze kujifunza kwao mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa. Lakini siwapati watu hawa kwenye mazingira niliyopo. Nimechagua kuangalia yale ambao walioshindwa wanafanya au hawafanyi na kwenda kinyume nao.
NENO LA LEO.
Unahitaji watu waliofanikiwa ambao utajifunza kutoka kwao kwa jinsi wanavyofanya mambo yao. Lakini jamii zetu hazina wengi waliofanikiwa na ambao wapo tayari kukufundisha.
Hivyo njia pekee unayoweza kutumia ni kuangalia wale walioshindwa wanapenda kufanya nini na wewe usikifanye, na angalia hawapendi kufanya nini na wewe ndiyo ukifanye.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.