Kuna majibu ambayo watu wakikupa pale unapowaambia kitu unaona ni jinsi gani ambavyo wanajizuia wao wenyewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Unamwambia mtu aweke juhudi ili kufikia utajiri, anakuambia siyo kila mtu anaweza kuwa tajiri. Ni sawa siyo kila mtu anaweza, lakini kuna ambao wanaweza, sasa kwa nini wewe usiwe mmoja wao?
Unamwambia mtu aanze mipango ya kujiajiri akiwa bado kwenye ajira ili baadaye aweze kuondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri na hata kuajiri wengine. Anakuambia hatuwezi wote tukawa waajiri, nani ataajiriwa. Nakubali kabisa, lakini kama kuna wachache ambao wameweza kuajiri, kwa nini na wewe usiwe mmoja wao?
Tatizo langu ni pale watu wanapochagua kukaa upande wa wengi, na wakati wote tunajua ya kwamba upande wa wengi ni upande ambao ni nadra sana kufikia mafanikio. Kwa nini ujitetee na wengi, kwa nini usiamue na wewe kuwa kwenye lile kundi la wachache?
Na cha kushangaza zaidi ni kwamba japo wengi wanajitetea siyo wote wanaweza kuwa kwenye kundi la wachache, watu hao ndio wanatamani sana kuwa kwenye kundi hilo. Sasa hebu acha kutamani na amua kuchukua hatua. Huku ukiacha kabisa kutumia huo utetezi kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa kwenye kundi la wachache. Huu ni utetezi wa wale ambao walishakata tamaa, kama na wewe ni mmoja wao basi kila la kheri.
SOMA; Unaweza Kupata Chochote Unachotaka Kwa Kufanya Kitu Hiki Kimoja.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba tabia ya kujitetea kwamba siyo wote wanaoweza kuwa kwenye kundi la wachache ni tabia ya walioshindwa na kukata tamaa. Mimi sitakubali kuwa kwenye kundi hili. Nitachagua kile ambacho ninataka na kukifanyia kazi bila ya kujali kila mtu anaweza au la.
NENO LA LEO.
Ni kweli kwamba siyo kila mtu anaweza kuwa tajiri, siyo kila mtu anaweza kuwa mwajiri na siyo kila mtu anaweza kufikia mafanikio makubwa. Lakini kwa nini usiwe wewe?
Acha kujitetea kwa kuwa kwenye kundi la wengi na kuona kundi la wachache halikuhusu. Chagua kile unachotaka na fanyia kazi, bila ya kujali ni wengi au wachache wameweza.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba tabia ya kujitetea kwamba siyo wote wanaoweza kuwa kwenye kundi la wachache ni tabia ya walioshindwa na kukata tamaa. Mimi sitakubali kuwa kwenye kundi hili. Nitachagua kile ambacho ninataka na kukifanyia kazi bila ya kujali kila mtu anaweza au la.
LikeLike
Safi sana.
Naona unafukua ya kale na kujifunza.
Ona jinsi nguvu ya maarifa yasivyooza.
LikeLike