Maua yatakayochanua kesho, ni yale ambayo yamepandwa leo. Na hivyo kama jana hakuna maua uliyopanda, usitegemee maua yachanue leo. Muhimu zaidi ni kwamba kulalamika na kujuta kwamba kwa nini hukupanda maua jana, hakutasaidia maua yachanue kesho. Njia pekee ya kuhakikisha hilo ni kupanda maua leo.

Huu ni ujumbe maalumu kwa wale wote ambao wanaona kama wameshachelewa, wale wanaosema kwamba ningejua siku zote hizo, au wanaojutia muda waliopoteza. Yote hayo hayasaidii wewe kuwa na maisha unayoyataka kwa siku zijazo. Kinachosaidia ni wewe kuchukua hatua leo, yaani leo hii hii na kutengeneza mazingira mazuri ya kesho.

Huwa nakutana na watu wengi wanaosema kama ningepata nafasi ya kujifunza haya miaka mitano iliyopita basi leo ningekuwa mbali sana. Na mimi nawajibu umeshajifunza leo, fanyia kazi ili miaka mitano ijayo uwe mbali.

Kuchukua hatua ndiyo njia pekee itakayokufikisha kwenye mafanikio, siyo njia nyingine yoyote. Kuwa mtu wa kuchukua hatua, na kila siku utaziona fursa nzuri za kuboresha maisha yako.

SOMA; SIRI YA 37 YA MAFANIKIO; Imani Nakupa Nguvu Ya Kuchukua Hatua

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kujutia au kulalamika nafasi nilizopoteza huko nyuma hakuniwezeshi kupata nafasi hizo kwa siku zijazo. Bali njia pekee inayoniwezesha kupata nafasi hizo nzuri ni kuchukua hatua sasa. Nitakuwa mtu wa kuchukua hatua kila mara ili niweze kufikia kile ninachokitaka.

NENO LA LEO.

Kujuta na kulalamika hatua ambazo ulishindwa kuchukua siku za nyuma hakutakusaidia chochote kwenye siku zijazo. Njia pekee itakayokusaidia ni kuchukua hatua sasa ili siku zijazo uwe kwenye nafasi nzuri.

Kama kuna kitu unataka, utakipata kwa kuchukua hatua, hakuna kuchelewa wala kuwahi, unachohitaji ni kujua ni nini hasa unachotaka na kukifanyia kazi. Kuchukua hatua ndiyo hitaji kuu la mafanikio.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.