Habari za leo rafiki?
Ni imani yangu kwamba uko vizuri na unaendelea kuweka juhudi ili kuboresha maisha yako zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Kitu kimoja ambacho nakukumbusha tena ni kwamba katika maisha kama huendi mbele basi unarudi nyuma. Hakuna kusimama, kwa sababu pale unapofikiri unasimama, dunia inakuacha, maana dunia inakwenda kwa kasi sana.
Hii ina maana kwamba unahitaji kwenda kasi, unahitaji kufanya mambo makubwa, ambayo hujawahi kufanya hapo awali, kama kweli unataka kufanikiwa. Lakini hapa linakuja tatizo, kwa sili binadamu hatupendi kujitesa, hatupendi kufanya vitu ambavyo hatuna uhakika navyo, na hivyo kushindwa kuchukua hatua. Na hapa ndipo tunapohitaji kitu kimoja muhimu sana ili tuweze kupiga hatua, na kitu hiki ni HAMASA.

Hamasa ina msaada sana kwenye kutusukuma sisi kuchukua hatua na kuweza kufanya mambo makubwa, yanayotufikisha kwenye mafanikio. Pamoja na umuhimu huu tunakutana na changamoto kubwa ya hamasa, huwa haikai kwa muda mrefu. Watu wengi huwa wanahamasika sana pale wanapoona watu wanafanya makubwa, na wao wanahamasika, ila unapofika wakati wa utekelezaji hamasa ile inakuwa haipo tena.

Nafikiri wewe utakuwa shahidi, huenda umewahi kusoma makala na ukahamasika sana, na ukasema unakwenda kuchukua hatua, ila inapofikia kuchukua hatua hamasa ile inakuwa imeshapita. Au umehudhuria semina na waongeaji wakakupa hamasa kubwa sana, ukaona kama unaweza kila kitu, na kutoka na nia kwamba unakwenda kufanya makubwa. Lakini inapofikia wakati wa kufanya hamasa haipo tena, na wakati mwingine unajishangaa uliwezaje kufikiria kama ungeweza kuchukua hatua kwenye kile ulichopanga.
Hili ni tatizo la wengi, na leo tutaangalia hatua za kuchukua ili uweze kuondokana na hali hii. Kabla hatujaangalia hatua hizi tusome maoni ya msomaji mwenzetu, ambaye amekutana na hali kama hii;
Changamoto kubwa kwangu inayonizuia kufikia mafanikio niyatakayo ni kutokutimiza, yaani ninaweza kuwa na hamu au shauku kubwa ya kufanya jambo au mambo fulani, moyoni huwa nawaza kwamba nitakuwa na furaha na amani sana nikifanya au kutimiza jambo fulani, huwa najipa siku kwamba siku fulani au saa fulani nitaanza rasmi kutekeleza jambo fulani, lakini cha ajabu siku au saa hiyo ikifika hamu na shauku ya kufanya lile jambo inatoweka. Natanguliza shukrani.
J. Shimoka.
Kama ambavyo tumesoma maoni ya msomaji mwenzetu, na ambavyo wengi tumekuwa tunapitia hili, hamasa imekuwa tatizo kwetu kuchukua hatua. Tunakuwa na hamasa kubwa ila haidumu, pale tunapofikia kuchukua hatua, hamasa inakuwa haipo tena. Je tunaweza kuchukua hatua gani ili kuepuka hili? Karibu tujifunze kwa pamoja;

1. Jua aina za hamasa, na ipi bora kwako.
Ni rahisi sana kuhamasika, lakini kuifanya hamasa idumu ndiyo changamoto kubwa. Kabla hatujaangalia kwa undani jinsi ya kudumu na hamasa kwa muda mrefu, ni vyema tukazijua aina za hamasa na ipi ni bora kwako.

Kuna aina mbili za hamasa;
Aina ya kwanza ni hamasa kutoka ndani, hii ni ile hamasa ambayo inatoka ndani yako mwenyewe. Na hii huwa inatokana na malengo fulani au kitu fulani ambacho una shauku ya kukifikia au kukipata.
Aina ya pili ni hamasa kutoka nje, hii ni ile unayoipata kutoka kwa wengine, kwa unavyowaona au kusikia mambo makubwa waliyofanya.
Katika hamasa hizi mbili, hamasa kutoka nje huwa haina nguvu kubwa na inaisha haraka. Lakini hamasa kutoka ndani yako inaweza kwenda kwa muda mrefu, kama utakuwa umeiweka vizuri na kuifanyia kazi.
SOMA; Sababu 7 Zinazokufanya Upoteze Hamasa Kwa Kile Unachokifanya.

2. Tengeneza hamasa ndani yako.
Hata kama utapata hamasa kutoka nje, kwa watu au kutokana na kitu ulichosoma, jaribu kujenga hamasa ya ndani inayoendana na hamasa hiyo ya nje uliyoipata. Kwa mfano kama umehamasika kuanzisha biashara, baada ya kusoma kitabu au makala ya biashara, kaa chini na utafakari kwa nini unataka kuanzisha biashara. Fikiria kuanzisha biashara kutakuwa na manufaa gani kwako? Na hapa utaona vitu kama kuwa na uhuru wa kifedha, kutawala muda wako, kusaidia wengine na kadhalika. Kwa kutengeneza sababu hizi zinazoendana na wewe utahamasika zaidi na kwa muda mrefu kuliko ungebaki na ile hamasa ya nje pekee.

3. Hamasa siyo kitu cha kudumu.
Changamoto nyingine inayofanya hamasa iwe changamoto kwa wengi, ni pale wanapofikiri hamasa ni kitu cha kudumu, hasa hamasa kutoka nje. Mtu anafikiri akishahudhuria semina moja basi anapata hamasa ya kutosha kufanya mambo makubwa. Au akisoma kitabu kimoja tayari ameshapata hamasa ya kutosha. Ukweli ni kwamba hamasa kutoka nje siyo kitu cha kudumu, bali ni kitu ambacho unahitaji kupata mara kwa mara.
Aliyekuwa mwandishi na mhamasishaji maarufu kutoka marekani Zig Zigler aliwahi kuulizwa ikiwa semina zake za kuhamasisha watu zinawasaidia kwa muda mrefu kiasi gani? Alijibu kwa kusema kuoga ni muhimu, lakini huwezi kuoga mara moja na ikawa imetosha, bali unahitaji kuoga kila siku. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye hamasa, huwezi kupata mara moja, bali unahitaji kupata kila siku.
Hivyo ni muhimu kujitengenezea mazingira ambayo yatakuwezesha wewe kupata hamasa kila siku, na siyo mara moja pekee.

4. Fika hatua ya kutotegemea hamasa moja kwa moja.
Kufanya jambo kutokana na hamasa kubwa uliyoipata kutoka kwa wengine ni sehemu nzuri ya kuanzia. Kama ambavyo mtoto anaanza kutembea kwa kutumia vitu vya kumzuia asianguke. Lakini ili mtoto aweze kukua ni lazima afike wakati aweze kutembea bila ya msaada. Na wewe pia unahitaji kukua katika hili la hamasa, usitegemee kila siku kusubiri hamasa ndiyo uchukue hatua.
Unahitaji kufika mahali na uwe unafanya kitu kwa sababu ndiyo umechagua kufanya, iwe una hamasa au la. Na ukishafikia hapa ndipo unaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako. na kama unahitaji hamasa basi utumie ile hamasa ya ndani. Na hata kama hamasa hii haikupi tena msukumo wa kufanya, endelea kufanya. Ni lazima uweze kuvuka hatua hii kama unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

5. Jipe ushindi mdogo mdogo.
Kitu ambacho kinawafanya wengi kushindwa kuchukua hatua baada ya hamasa, ni pale ambapo hamasa inawasukuma watake kufikia makubwa sana. Lakini ukweli ni kwamba huwezi kufikia makubwa kwa wakati mmoja, ni lazima uanze kidogo kidogo. Unaweza kuhamasika sana kwa habari za mfanyabiashara aliyeanza kuchoma mahindi lakini sasa anamiliki biashara za kimataifa. Na wewe utasahau kuhusu kuchoma mahindi na utaangalia biashara za kimataifa. Huwezi kufika huko bila ya kuanzia chini.
Unapopata hamasa ya kufanya makubwa, sahau hayo makubwa kwanza na angalia ni hatua zipi ndogo ndogo unazohitaji kupitia. Jiwekee malengo madogo madogo kwa kutumia hatua hizo na yafanyie kazi. Kila lengo dogo unalotimiza jipe ushindi. Kwa njia hii utapata hamasa kubwa ya kufanya zaidi na kuweza kufikia mafanikio makubwa.

6. Chukua hatua mara moja.
Watu wengi wanapopata hamasa ya kufanya kitu, huwa wanasema watachukua hatua watakapokuwa tayari. Na inapofika wakati wakaona wako tayari, hamasa ile inakuwa haipo tena. Ili kuondokana na hili, kuwa mtu wa kuchukua hatua mara moja. Kama umehamasika na kitu, anza kuchukua hatua hapo hapo, hata kama ni hatua ndogo sana. Fanya chochote ambacho kitakukumbusha kwamba umeshafanya maamuzi na sasa wewe ni kutekeleza tu.
Usianze kujiambia kwamba haupo tayari na wala usisubiri kuwa tayari, hakuna wakati utakuwa tayari zaidi ya ulivyo sasa. Kuwa mtu wa kuchukua hatua na hutasubiri tena hamasa.

SOMA; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Katika ulimwengu huu ambao kila jambo unalofanya lina changamoto, na licha ya hilo kuna wengi ambao wanakukatisha tamaa, unahitaji hamasa zote mbili. Hamasa kutoka nje na hamasa kutoka ndani yako mwenyewe. Itumie hamasa kuanza na jijengee tabia ya kuchukua hatua mara moja ili usiwe mtu wa kutegemea hamasa pekee.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
 
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.