Katika jambo lolote ambalo unachagua kufanya, kuna wengine wengi ambao nao pia wanalifanya. Inawezekana umeanza kufanya kwa sababu uliona wengine wanafanya au wengine wamekuona wewe unafanya na wao wakaanza kufanya. Hivyo ushindani ni kitu ambacho huwezi kukikimbia.
Kama unavyojua, kushindana moja kwa moja ni kitu ambacho sikushauri ufanye kwa sababu kutakuumiza sana. Ushindani wa moja kwa moja lazima utakuacha na majeraha. Badala ya kushindana moja kwa moja, unahitaji kuwa mbele ya wengine, yaani kuwaacha nyuma sana.
Unapoweza kuwa mbele ya wengine, unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kufanya makubwa na kufanikiwa zaidi kwenye jambo lolote unalofanya.
Kuna njia mbili unazoweza kutumia ili kuwa mbele ya wengine. Na njia hizo ni kama ifuatavyo.
Njia ya kwanza ni kutumia akili, hapa unahakikisha unawazidi akili na ujanja wale wengine ambao wanafanya kile unachofanya. Kwa njia hii unakuwa mbunifu na kuongeza ubora kwenye kile unachofanya. Unahakikisha unaona mbali zaidi ya wengine na kufanyia kazi yale unayoona.
Njia ya pili ni kutumia juhudi au nguvu, hapa unahakikisha ya kwamba unaweka juhudi kubwa sana kwenye kile unachofanya na hivyo kuzalisha matokeo mengi zaidi. Kwa njia hii unakuwa na uzalishaji mkubwa kuliko washindani wako.
Uzuri ni kwamba kama huwezi kuwazidi wengine akili, basi unaweza kuwazidi jitihada, weka jitihada za kutosha na siku zote utakuwa mbele ya wengine.
SOMA; Nani ni mshindani wako kwenye biashara? Umuhimu wa kujua na jinsi ya kutumia vizuri ushindani.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba naweza kuwa mbele ya wengine kama nitatumia njia hizi mbili, akili na jitihada. Nitahakikisha mara zote natumia akili kwenye mambo ninayofanya na pia nitaweka juhudi kubwa ili niweze kupata matokeo ninayotaka kupata. Hata kama wengine watanizidi akili, sitakubali wanizidi juhudi.
NENO LA LEO.
Kuna njia mbili unazoweza kutumia kuwa mbele ya wengine wanaofanya kile unachofanya. Akili na juhudi.
Tumia akili katika kuboresha unachofanya, kuwa mbunifu na mgunduzi. Pia weka juhudi kubwa na nenda hatua ya ziada kwenye jambo lolote unalofanya.
Na ikiwa wengine watakuzidi akili, basi hakikisha wewe unawazidi juhudi. Hakuna kinachoweza kukuzuia kwenye hilo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.