Epuka Adui Huyu Mkubwa Wa Mafanikio Yako Anayekurudisha Nyuma.

Nina imani umewahi kuona watu ambao wameanzia chini kabisa, wakakazana sana kuweka juhudi na hatimaye kufikia mafanikio. Lakini baada ya mafanikio haya wakashindwa vibaya na kurudi tena chini. Inawezekana umeshaona mtu ambaye alikuwa anatafuta nafasi ya kazi au biashara kwa shauku kubwa na kuahidi kwamba akiipata ataweka juhudi kubwa ili kuitumia vizuri. Lakini anapoipata muda mfupi baadaye anaanza kuichukulia ya kawaida na haweki zile juhudi alizoahidi.
 
Kuna mifano mingi ya jinsi watu wamekazana kuanza lakini mwisho wao unakuwa mbaya. Wapo ambao wameyaonja mafanikio kidogo, wengine wameonja makubwa ila mwisho wa siku wote wanarudi chini bila ya kujali mafanikio gani wameweza kufikia.

 
Leo katika makala hii tutaangalia adui mmoja mkubwa sana wa mafanikio yako unayotakiwa kumwepuka kama unataka kuwa na mafanikio ya kudumu. Mafanikio ya kweli ni yale yanayodumu na siyo yale ya kufikia juu kisha kurudi chini na kubaki na hadithi kwamba enzi zangu nilikuwa vizuri. Watu wanataka kuona una nini au unafanya nini kwa sasa na siyo enzi zako zilikuwaje.
 
Adui mkubwa wa mafanikio yako.
Kama umechagua safari hii ya mafanikio kuna adui mmoja mkubwa unatakiwa kumjua ili asirudishe mafanikio yako nyuma. Adui huyu ni kuyazoea mafanikio na kuona ni kitu cha kawaida kwako. Binadamu tuna tabia ya kuzoea vitu, kitu kinapotokea kwetu kwa zaidi ya mara moja tunaona ni kitu cha kawaida, ila shauku na hamasa tuliyokuwa nayo awali inakuwa haipo tena. Kwa mfano kama una hamu sana ya kunywa soda, soda ya kwanza utakayokunywa utaona ni nzuri sana na utaifurahia. Ukiongeza soda nyingine unaona ni kawaida tu. Ukiongeza soda ya tatu unaanza kuona ni mzigo kwako.
Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio. Watu wengi wanapoyapata mafanikio kwa mara ya kwanza, pale wanapoweza kufikia kitu ambacho walikuwa wanakitaka, wanafurahi sana na kuona ni nafasi nzuri sana kwao. Lakini wanapoendelea kupata wanaanza kuona ni kitu cha kawaida kwao. Ile shauku inakosekana na hivyo kuanza kuchukulia kawaida, hapa ndipo changamoto nyingi zinapoanzia.
Mtu anaanza biashara kwa kuwahudumia vizuri wateja wake na kuhakikisha wanapata kile wanachotaka, wateja wanafurahi na kuendelea kuja kwake, yeye anaanza kuona ni kitu cha kawaida kwake, anaanza kutoa huduma za kawaida kwa wateja ambazo zinakuwa ni mbovu na wateja wanaanza kukimbia. Au mtu anaanza kazi kwa kujitoa kuweka juhudi kubwa, anatoa matokeo bora na wengi wanayafurahia, anayazoea na kuanza kufanya kwa kawaida na kujikuta anashusha thamani yake.
Hili ni tatizo kubwa sana ambalo limewafanya watu kupoteza nafasi nzuri ambazo walikuwa wameshajijengea mbele ya wengine na kurudi nyuma. Ndiyo maana ni muhimu sana kwako wewe kama mwana mafanikio kujua hili na jinsi ya kuliepuka. Ukilijua vizuri na jinsi ya kuepuka utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwa na mafanikio yatakayodumu kwa muda mrefu.

Jinsi ya kuepukana na adui huyu wa mafanikio yako.
Kwa kuwa umeshamjua adui huyu wa mafanikio ambaye anamnyemelea kila mmoja wetu, ni vyema ukajua njia za kuepukana na adui huyu ili uweze kumwepuka. Hapa nimekushirikisha zile njia bora kabisa za kuepukana na adui huyu. Karibu tujifunze kwa pamoja.

1. Jua mafanikio ni mchakato na siyo hitimisho.
Watu wengi huwa wanafikiri ya kwamba wakishapata kile walichokuwa wanatafuta basi wamefikia kilele cha mafanikio. Hii ni fikra potofu ambayo inawapoteza wengi. Chochote unachokipata leo, kesho thamani yake inaanza kupungua. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo dunia inavyobadilika na vitu vyote vinabadilika. Kama wewe utabaki na vitu vya nyuma, vitapoteza thamani na hutakuwa tena na mafanikio.
Ni muhimu ujue kuwa mafanikio ni mchakato, ambapo kila siku unafanya jambo ambalo linazidi kukusogeza karibu na kile unachotaka au kuboresha zaidi kile ambacho tayari umeshapata. Kamwe usifike mahali na kujiona ya kwamba umeshamaliza kila kitu, mafanikio ni safari ya maisha yako yote.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.

2. Kila kitu kinaweza kuboreshwa zaidi.
Hakuna kitu chochote ambacho kimeshafikia kilele cha ubora, kila kitu kinaweza kuboreshwa zaidi ya kilivyo sasa. Ukilijua hili hutatengana na mafanikio. Biashara zote mpya zinazoanzishwa na kufanikiwa, huwa zinaanzishwa kwa misingi hii. Unakuta kuna biashara nyingine kama hiyo, lakini kuna maeneo inakuwa na udhaifu, wengine wanaona madhaifu hayo na kuyatumia kuanza biashara.
Jua ya kwamba chochote unachofanya, na kwa ngazi yoyote ambayo umeshafika, unaweza kuboresha zaidi na zaidi. Na hivi ambavyo mambo yanabadilika, hasa kwa teknolojia na mtandao, kuna fursa nyingi za kuboresha kile unachofanya. Zitumie fursa hizi na utabaki kwenye mafanikio maisha yako yote.

3. Usiache kufanya kile kilichokufikisha kwenye mafanikio.
Hapa ndipo matatizo mengi yanapoanzia, unakuta mtu anaanzia chini kwa unyenyekevu sana. Anajituma na kuweka juhudi kubwa, anafanya kazi za ziada ukilinganisha na wengine, anaweka gharama zake za maisha chini, anaepuka starehe. Lakini anapopata mafanikio anaanza kubadilika, anaacha kuweka juhudi kubwa kwenye kile anachofanya, anaanza kuendekeza starehe na hatimaye anashindwa kuendelea kutoa ule ubora aliokuwa anautoa.
Kuna usemi wa kiswahili unasema pata pesa tujue tabia yako, kwamba tabia za wengi kabla hawajafanikiwa siyo tabia zao halisi, wako vile kwa sababu ya shida tu. Wewe usikubali kubadilika na kuacha kufanya kile kilichokufikisha kwenye mafanikio. Kama unabadilika unahitaji kubadilika kwa kuwa bora zaidi, siyo kwa kuacha. Kile ambacho umechagua kufanya, hakikisha unaweza kukifanya kwenye maisha yako yote.

4. Msukumo usiwe fedha pekee.
Pale ambapo msukumo wa kufanya kitu unakuwa fedha, ukishazipata ule msukumo unaisha. Unahitaji kuwa na sababu ya kufanya zaidi ya kupata fedha. Unahitaji kuwa unapenda kile ambacho unakifanya kwa sababu unaona mchango wake kwenye maisha ya wengine. Kwa njia hii utapata hamasa zaidi bila ya kujali umefikia kiwango gani cha mafanikio.
Unapoona ya kwamba kile unachofanya kina maana kwako na kwa wengine na kimefanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi unapata msukumo wa kuendelea kufanya. Hii inaanza pale ambapo unapenda kile unachofanya.

5. Ongeza ubunifu kila siku.
Kila siku mpya inayoanza, jiulize ni kitu gani kipya unachokwenda kufanya kwenye kazi au biashara yako. kuwa mbunifu kwa kuanza na vitu vidogo vidogo, hivi ndiyo vitu ambavyo vitaleta mabadiliko makubwa baadaye. Usifikiri kuna siku utafika na kuona mabadiliko makubwa haya hapa, bali utayatengeneza kwa hatua ndogo ndogo unazochukua. Zichukue hatua hizi vizuri kwa kuwa mbunifu kwenye kila unachofanya.
SOMA; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.
Hakuna adui mkubwa wa mafanikio kama kuyazoea mafanikio, pale unapoona ya kwamba umeshafika ndipo unapokuwa umepotea njia. Pale unapofikiria kwamba umeshapata kila kitu ndipo unakuwa umeanza kupoteza kila kitu. Hakuna hatua ya mwisho ya mafanikio, unahitaji kuweka juhudi kila siku ili kuwa bora zaidi.
Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi njia hizi za kuondokana na adui wa mafanikio yako.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: