Ukweli ni kwamba tunaishi kwenye zama ambazo kuna usumbufu wa hali ya juu sana. Sasa hivi mtu yeyote anaweza kukusumbua muda wowote anaoamua wewe. Ukuaji wa teknolijia na mtandao na ujio wa mitandao ya kijamii pamoja na simu janja (smartphone) umefanya iwe rahisi sana kusumbuliwa.
Tunasumbuliwa kwa simu zisizokuwa muhimu, kujibu jumbe ambazo hazina mchango mkubwa kwetu, na kubwa zaidi ni mitandao ya kijamii kama facebook na instagram. Na mbaya kuliko wote ni wasap ambapo unaweza kusumbuliwa siyo tu na wale unaowafahamu, bali hata usiowafahamu kupitia makundi mbalimbali ambayo hayana faida kwako.
Kwa usumbufu huu ni vigumu sana kuweza kufanya kazi yenye maana hasa kwa wale ambao wanafanya kazi zinazohusisha zaidi akili na kufikiri. Watu wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye kazi lakini uzalishaji na ufanisi wao ni mdogo sana. Hapa ndipo mwandishi Cal Newport alipofanya utafiti na kuja na mbinu bora za kuweza kufanya kazi yenye maana (DEEP WORK) katika zama hizi.
Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi huu wa kitabu hiki. Kuna mengi sana ya kujifunza, twende pamoja.
- Kazi yenye maana (DEEP WORK) ni ile kazi ambayo mtu anaifanya kwa kufikiri kwa kina. Ni ile kazi ambayo ni ya kibunifu na inaongeza thamani kwenye maisha ya watu wengine. Ni kazi ambayo inahitaji utulivu mkubwa kwenye kuifanya na matunda yake huwa mazuri sana pale inapokamilika. Kazi hii huhitaji akili yako yote kuwa sehemu moja. Ni wachache sana wanaoweza kufanya kazi kwa mtindo huu na hivyo hii ni fursa kubwa kwa anayeweza. Thamani yake itakuwa juu sana iwe ni kwenye kazi au biashara.
- Kazi isiyo ya maana au kazi ya juu juu (SHALLOW WORK) ni kazi ambayo inafanyika kwa mazoea, mtu hahitaji kutuliza akili yake ili kuifanya. Anaweza kufanya kazi hiyo huku akiendelea na mambo mengine kama kuperuzi mitandao. Ni kazi ambayo haina utofauti mkubwa na hivyo thamani yake ni ndogo. Na ni kazi ambayo kila mtu anaweza kuifanya, hivyo haina uhitaji mkubwa. Hii ndiyo aina ya kazi ambayo watu wengi wanapenda kufanya na ndiyo inapelekea kuwa na maisha magumu kwa kuwa na kipato kidogo.
- Sababu namba moja ya watu kushindwa kufanya kazi zenye maana ni kuongezeka kwa mitandao ya burudani na mitandao ya kijamii. Sasa hivi kuna mitandao mingi ambayo inawavutia watu kutembelea na hata unapoitembelea unajijenga utegemezi kwenye mitandao hii. Mtu anaweza kuingia facebook na kuperuzi kwa muda, akatoka lakini baada ya dakika chache anataka kuingia tena kwa sababu kuna kitu anaona anakosa. Mitandao hii imekuja kuwa changamoto kubwa sana kwenye kazi zetu.
- Tunaishi kwenye ulimwengu wa uchumi mpya, (NEW ECONOMY) huu ni ulimwengu ambao mashine zinazidi kuwa bora kila siku. Na waajiri wanapendelea zaidi mashine kuliko watu, kwa sababu mashine zina ufanisi mkubwa na uzalishaji mkubwa sana. Kadiri teknolojia inavyokwenda, watu ndivyo wanavyozidi kurudi nyuma na hii kuhatarisha ustawi wa watu. Hali hii inafanya kazi yenye maana kuwa na thamani kubwa sana. Waajiri wataajiri wale ambao wanaweza kufanya kwa ubora sana kuliko mashine, au kuziendesha mashine kwa ubora.
- Katika ulimwengu huu wa uchumi mpya, kuna makundi matatu ya watu ambao wataweza kuhimili na kufikia mafanikio makubwa sana.
Kundi la kwanza ni wale ambao wanaweza kujifunza mambo magumu na kuyafanyia kazi. Hawa ndiyo wale ambao wanaweza kutumia mashine na teknolojia mpya kurahisisha kazi wanazofanya.
Kundi la pili ni watu ambao wana vipaji na wanavifanyia kazi na kuwa bora sana (super stars) kwenye kile wanachofanya. Hii inaongeza thamani yao na hivyo kupata kipato kikubwa.
Kundi la tatu ni wale wenye mitaji mikubwa na kuweza kuwekeza kwenye mawazo bora ya biashara zinazoendeshwa na wengine.
Je wewe unaingia kwenye kundi lipi kati ya hayo matatu? Kundi la tatu linaweza kukushinda, lakini la kwanza na la pili, ushindwe mwenyewe tu.
- Kuna mahitaji mawili muhimu unatakiwa kufikia ili kuweza kufanikiwa kwenye ulimwengu huu wa uchumi mpya;
Hitaji la kwanza ni kuweza kufanya vitu vigumu. Vile vitu ambavyo wengine hawapo tayari kufanya ndivyo vyenye thamani kubwa, ukiweza kuvifanya unajiweka kwenye nafasi nzuri.
Hitaji la pili ni kuweza kuzalisha kwa viwango vya juu sana kwa ubora na kasi nzuri. Kufanya vitu vigumu pekee hakuwezi kukusaidia kama hutatoa matokeo bora na kwa muda ambao yanategemewa. Hili pia lipo ndani ya uwezo wako, fanyia kazi.
- Peleka mawazo yako yote kwenye kile kitu ambacho unakifanya kwa wakati mmoja. Kwa njia hii unaweza kuitumia akili yako vizuri na hivyo kutoa matokeo bora. Lakini kama unafanya kitu huku mawazo yako yapo sehemu nyingine, huwezi kutoa matokeo bora.
- Tenga muda wako kulingana na kazi unayofanya na kisha kaa mbali na usumbufu wowote utakaoondoa akili yako kwenye kazi hiyo. Tafiti zinaonesha kwamba unapofanya kitu halafu ukakatisha na kwenda kufanya kitu kingine, ukirudi kwenye kile ulichokuwa unafanya mwanzo itakuchukua muda mrefu mpaka kufikia ile hatua ambayo ulikuwa mwanzoni. Ili uweze kuzalisha kazi yenye maana, unahitaji kuwa na muda ambao hauingiliwi na vitu vingine, kama mawasiliano au mahitaji ya wengine.
- Binadamu tuna tabia ya kufanya kile ambacho ni rahisi kufanya hasa inapokuja kwenye kazi. Kufuata njia rahisi ni kinyume kabisa na kuzalisha kazi ya maana na ambayo ni bora. Na kadiri unavyofanya kazi kwenye mazingira yenye usumbufu ndivyo inavyokuwa rahisi kwako kutafuta njia rahisi.
- Unaweza kufanya kazi unayofanya sasa kwa muda mfupi kuliko unaotumia kufanya sasa kama ukiamua kuachana na mambo yanayokupotezea muda wako wa kazi. Mara nyingi kazi hujaza muda unaopatikana na kama muda ni mwingi kuliko kazi basi mtu anakuwa na mambo mengi ya kupoteza muda katikati ya kazi zake.
- Kuna watu wanafikiri kwamba kitu chochote ambacho kipo kwenye mtandao basi ni sahihi na muhimu. Kwa fikra hizi wengi wamekuwa wakiruhusu mtandao kuwa usumbufu mkubwa kwao, kufungua kila wanachokiona na kujikuta wanapoteza muda wa kufanya kazi zao.
- watu wengi huwa wanafikiri kwamba kazi ni mzigo kwao na hivyo kutafuta vitu rahisi vya kufanya kama kuperuzi mitandao na usumbufu mwingine. Lakini tafiti zinaonesha kwamba watu wanakuwa na furaha pale ambapo wanafanya kitu kigumu na kuweza kukikamilisha. Pale watu wanapopata changamoto na kuifanyia kazi ndipo wanapoona maana ya maisha yao. Ndiyo maana ni muhimu sana ufanye kazi yenye maana.
- Ili uweze kufanya kazi yenye maana, unahitaji kujiwekea utaratibu wa maisha yako (routine). Kwa sababu utashi wetu unapungua na hivyo kadiri tunavyofanya maamuzi mengi ndivyo utashi wetu unavyokosa nguvu. Na hii inasababisha wengi kuahirisha mambo. Kama ukijiwekea utaratibu, kwamba baada ya kitu fulani basi unafanya kitu fulani, inakuwa rahisi kwako kuchukua hatua. Kwa mfano unaweza kujiwekea utaratibu ukiamka tu, unajisomea, au ukifika kazini tu cha kwanza ni kazi na siyo kuingia kwenye mtandao.
- Kuna njia tatu unazoweza kutumia kwenye kufanya kazi yenye maana kwa kuepuka usumbufu wa mitandao na wengine.
Njia ya kwanza ni kuondoka kabisa kwenye usumbufu (disconect) hapa unapotea kabisa na kujifungia ambapo hakuna usumbufu wa hali yoyote na hapo kuweza kufanya kazi zako kwa kina. Kwa njia hii watu hawakuoni kabisa.
Njia ya pili ni kugawa siku yako, muda fulani huonekani na unafanya kazi yako kwa kina na muda mwingine unaonekana kwenye kazi ambazo siyo za kina.
Njia ya tatu ni kutenge muda fulani kwenye siku yako ambapo unafanya kazi yako bila ya usumbufu. Kwa mfano kutenga asubuhi kuwa muda wako wa kazi na hivyo kutoruhusu usumbufu kwenye muda huo.
- Chagua mambo machache ambayo utayafanya kwa kina na kupata matokeo bora kuliko kung’ang’ania kufanya mambo mengi na kupata matokeo ya hovyo. Ukweli ni kwamba kadiri unavyokazana kufanya mambo mengi ndivyo unavyoshindwa kupata matokeo bora. Angalia majukumu yako kwa kina na chagua yapi ni muhimu kwako kufanya na yapi siyo muhimu na uyaache.
- Jiwekee ukomo kwenye muda wako wa kazi. Hivi vifaa vya kisasa kama kompyuta na simu, vimefuta kabisa mstari kati ya kazi na maisha ya kawaida. Kwa sasa mtu anaweza kufanya kazi za ofisini hata akiwa nyumbani. Kwa njia hii mtu anashindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi na kupoteza muda wake wa kuishi. Ili kuondokana na hili jiwekee ukomo kwenye muda wako wa kufanya kazi na usikubali kuiba muda mwingine. Jiambie muda wako wa kazi unaisha labda saa kumi na moja jioni, baada ya hapo fanya mambo mengine na usifanye jambo linalohusiana na kazi. Kwa kujijengea nidhamu hii utaongeza umakini kwenye muda wako wa kazi.
- Watu wengi wanapokuwa hawana kitu cha kufanya (iddleness) hutafuta usumbufu wa kujaza muda huo. Na hili limefanya wengi kuwa wategemezi wa usumbufu, kama kuangalia mitandao ya kijamii. Ni nadra sana kwa sasa kukuta mtu amesimama kwenye mstari anasubiri kitu akiwa hajashika simu yake, na ukiangalia simu hiyo yupo wasap, facebook au instagram. Jipe ruhusa ya kuwa na upweke na tumia muda huu kutafakari yale unayofanya kwenye maisha yako. Jizuie pale hamu ya kutafuta usumbufu inapokujia na kwa njia hii utajijengea nidhamu nzuri.
- Acha kutumia mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii ndiyo usumbufu namba moja ambao unawazuia wengi kufanya kazi zenye maana. Na mitandao hii imetengenezwa kwa mbinu za kisaikolojia ambazo zinamfanya mtu aone kama anapitwa asipoingia kwenye mitandao hii. Ukweli ni kwamba kama hutumii mitandao ya kijamii kukuingizia fedha, basi wewe ni mteja wa watu wengine, na kwa kifupi ni kwamba unapoteza muda. Na siyo kweli kwamba ukiacha kutumia kuna kikubwa unakosa.
Na njia nzuri ya kuacha kutumia mitandao hii ni kujipa siku 30 za kutoingia kabisa kwenye mitandao ya kijamii, hili unafanya kama jaribio. Baadaye angalia maisha yako yamebadilikaje kwa siku hizi 30, kwa asilimia kubwa yatakuwa bora zaidi. Na fanya hili kimya kimya, wala usimwambie yeyote na wala wengi hawatajua kama haupo maana kuna mengi yanawasumbua kuliko uwepo au kutokuwepo kwako kwenye mitandao hii.
- Linda sana muda wako, kuwa mchoyo sana na muda wako, maana hiki ndiyo kitu pekee ambacho kinakuwezesha kufanya kazi yenye maana kwako. Usiseme neno NDIYO kirahisi, ndiyo itakuzuia wewe kufanya yale ambayo ni muhimu kwako. Usiwe rahisi kufikiwa na kupokea majukumu ya wengine ambayo hata siyo muhimu kwako au kwa wengine. Mfano mtu anaweza kuwa amechoka na hivyo kutafuta mtu wa kumpumzikia, anakutumia wewe ujumbe ukiwa kwenye kazi yako, unaacha kazi na kuanza kumjibu, unapoteza muda wako na yeye haimsaidii chochote. Kuwa makini sana na muda wako.
- Jipe muda wa kupumzika na heshimu sana muda huu. Kupumzika ina maana unapumzisha akili yako kwa kuwa mbali na kazi na pia kutokuwa karibu na usumbufu. Kuangalia tv siyo kupumzika, kuperuzi mitandao ya kijamii siyo kupumzika. Pumzisha mwili na akili yako kwa njia bora kama kusinzia au kutembea sehemu tulivu na wakati mwingine utakapoanza kazi utakuwa na nguvu za kutosha.
Hizi ndizo mbinu unazoweza kutumia kuepuka usumbufu wa ulimwengu huu tunaoishi sasa na kuweza kufanya kazi yenye maana. Kumbuka ni kazi yenye maana itakayokutambulisha wewe na kukuletea sifa na sio kelele utakazopiga kwenye usumbufu kama mitandao ya kijamii. Weka kipaumbele kwenye kile unachozalisha na siyo unachotumia. Kufanya kazi yenye maana ni kuwa ACTIVE, kuperuzi mitandao ya kijamii, kuangalia tv na kufuatilia habari ni PASSIVE, sasa chagua unataka maisha gani, ACTIVE au PASSIVE.
Nakutakia kila la kheri katika kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha maisha yako, kwa kufanya kazi yenye maana.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,