Habari mpendwa rafiki na msomaji wa Amka Mtanzania? Karibu katika makala yetu ya leo ambapo tutajifunza mambo muhimu ya kuzingatia pale unapotaka kufunga ndoa na utajiri.
Mafanikio ni safari. Hivyo kabla hujaanza safari ya kufunga ndoa na utajiri au mafanikio kuna mambo muhimu unapaswa kuyajua ili ukianza safari yako wewe ni kusonga mbele kwani ukijua kweli itakuweka huru. Tunahitaji kila mtu afanikiwe katika maisha yake kiroho, kimwili na kiakili. Haitoshi kufanikiwa kifedha tu bali fanikiwa katika nyanja zote. Mafanikio ni zaidi ya fedha kwa hiyo ni vema kuimarisha na kuboresha kila idara katika ya maisha yako kuwa bora.

Yafuatayo ni Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Kabla Hujaanza Safari Ya Kufunga Ndoa Na Utajiri;
 
1. Badili Mtazamo Wako;
Ili uweze kufanikiwa kitu cha kwanza unatakiwa kubadili mtazamo ulikua nao juu ya mafanikio. Kama ulikuwa ni mtu wa mtazamo hasi ambaye huamini katika uwezekano (pessimism) unatakiwa ubadili mtazamo wako na kutoka huko shimoni na kuingia katika mtazamo chanya kwa watu wanaoamini katika uwezekano wa mambo kutokea (optimism). Ukiwa katika mtazamo hasi ni ngumu kufanikiwa kwani utakuwa unawaza tu katika kushindwa kila jambo unalofanya unaamini haliwezekani kutokea. Unakuwa kama vile una ukungu mbele yako ambapo ukungu huo unakufanya usione vema mbele. Hivyo kama kweli umejitoa katika safari ya kufunga ndoa na utajiri ingia katika kundi la watu chanya ili uweze kuleta mapinduzi katika maisha yako.
 
2. Usisubiri Upewe Ruhusa;
Maisha ni mafupi sana hapa duniani ukisema usubiri kupewa ruhusa ndio uanze kuthubutu jambo fulani katika maisha yako unakuwa bado hujapata uhuru. Kuna msemo mmoja wa kiutafutaji uliosemwa na James Baldwin unasema hivi ‘’uhuru siyo kitu ambacho kila mtu anaweza kupewa. Uhuru ni kitu ambacho watu wanaamua kuchukua. Na watu wako huru kama wanavyotaka kuwa.’’ Hivyo basi ,ukisema unasubiri ruhusa maana huna uhuru na maisha yako na uhuru ni kitu ambacho watu wanaamua kuchukua sasa hauoni kama ukiendelea kusubiri kupewa ruhusa ni kupoteza muda? Mwanafalsafa Seneca aliwahi kusema hivi ‘’ Maisha ni muda. Na maisha ni marefu kama ukiutumia muda wako vizuri hapa duniani.’’ Hivyo basi kazi ni kwako kuchukua hatua juu ya maisha yako.
SOMA; Hizi Ndizo Faida Za Kufunga Ndoa Na Utajiri Na Kuupa Umasikini Talaka.
 
3. Kubali Changamoto Na Uzikabili;
Kwanza kabisa hakuna maisha bila changamoto. Changamoto ndio maisha, hivi kila kitu kingekuwa ni rahisi maisha yangekuwaje? Katika safari ya mafanikio changamoto haziepukiki na dawa nzuri ya changamoto yoyote katika maisha yako ni kuikabili na kuipatia ufumbuzi na siyo kuikimbia. Kukimbia tatizo ni kuongeza tatizo lingine tena. Kaa ukijua kwamba hakuna kitu kirahisi na siyo kwamba ukifunga ndoa na utajiri ndio uweke mikono mifukoni lahasha unatakiwa utoe mikono mifukoni uendelee kupanda ngazi mpaka unafika kileleni. Changamoto zipo na zitaendelea kuwepo ukisema unaogopa changamoto huwezi kufanya jambo lolote. Tafiti zinaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotekea na kusababisha vifo vingi ni ajali za barabarani ukilinganisha na ajali za usafiri wa anga. Sasa hata kama magari ni changamoto barabarani ndio utaacha kupanda gari? Lazima utapanda gari kwa namna yoyote ile. Kwa hiyo changamoto ni sehemu ya maisha yetu na wakati mwingine huweza kuwa fursa.
 
4. Hakuna Mafanikio Ya Haraka;
Ndio hakuna mafanikio ya haraka, huwezi kupanda leo na kuvuna kesho. Hapa lazima upande ngazi na hakuna lifti. Mafanikio hayatokei kama ajali au radi bali ni hatua na katika kila hatua kuna hatua ndani yake. Mwingine anafanya kitu kwa mkumbo akisikia kitu Fulani kinalipa naye huyo anakurupuka anafanya bila kuwa na maarifa ya kutosha ,anashindwa na hatimaye kukata tamaa na kwenda kutangaza kwa wengine mtazamo hasi juu ya mafanikio kwa kuwa yeye alishindwa na aliingia kichwa kichwa.
Unatakiwa uwe mtu wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa waingereza wanasema work hard but smart. Unapoingia katika safari hii lazima utambue hilo kama ulizoea kufanya mambo kwa kujisikia na kuahirisha hapa sema hapana kabisa tena unatakiwa kufanya kazi zaidi ya masaa ukilinganisha na wengine. Hivyo hakuna mafanikio ya haraka.
 
5. Uwe Mtu Anayependa Kujifunza;
Maarifa ndio kila kitu katika safari ya mafanikio ya kufunga ndoa na utajiri. Kama unafanya kazi kwa juhudi tu bila kutumia maarifa basi ujue unakosea na badilika. Uwekezaji siku hizi unahitaji taarifa mbalimbali ili uweze kufanya kazi zako kwa ufanisi wa hali wa juu na kuleta matokeo bora. Unatakiwa kujifunza kwa kusoma vitabu, semina na kujifunza kwa watu waliofanikiwa. Hapa unaweza kumtafuta hata mtu wa mfano kwako anayekuongoza katika kile unachofanya.
 
6. Kukubali Kulipa Gharama.
Pia unatakiwa kuwa mtu wa kupenda kujifunza kila siku na uwe tayari na kukubali kulipa gharama. Mafanikio ni gharama na kila kitu kina bei yake lazima ulipie ili upate huduma. Kama ukiwa mtu wa kujifunza lazima ukubali kulipa bei ya gharama kwani kila kitu kina gharama yake lazima ulipie bei ili upate huduma. Ukubali kulipia bei katika kujifunza kwani utahitaji kununua vitabu, utahitaji semina mbalimbali nk. Kama utakuwa umejiandaa kulipia bei ya gharama basi utayaona mafanikio. Unakuwa mbahili wa kulipia gharama na kufanya kazi kimazoea na kujifariji unajua kila kitu matokeo yake unakuwa uko sehemu hiyohiyo kila siku bila kupiga hatua. Usidharau kabisa kitu kinachoitwa maarifa. 
 
7. Acha Ushabiki Wa Vitu Visivyokuwa Na Ulazima au Msingi;
Kama umejitoa katika safari ya kufunga ndoa na utajiri unabidi uachane na ushabiki wa kijinga ambao haukuingizii kitu chochote. Kama ulikuwa ni mtu wa kulalamika bila kuchukua hatua acha, kubishana na kukaa vijiweni sema hapana kubwa leo. Vitu vya ushabiki vitakupotezea muda wako kabisa unashibikia vitu utafikiri una hisa zako juu ya hicho kitu unachobishania. Kama umeingia katika safari hii tafadhali achana na ushabiki na vitu ambavyo havina ulazima kwako.
 
8. Uwe na Nidhamu;
Nidhamu ni daraja la mafanikio. Hata kama ukiwa na vyote lakini ukikosa nidhamu binafsi ni tatizo. Unatakiwa kuwa na nidhamu ya muda, nidhamu ya fedha na nidhamu ya kila kitu katika maisha yako. Kama umekosa nidhamu ni ngumu kufika katika kilele cha mafanikio. Hata ukiwa mtafutaji mzuri lakini huna nidhamu ya fedha unakuwa bado umefunga ndoa na umasikini. Nidhamu itafanya mambo yako kwenda katika mstari ulionyooka kukujengea heshima kubwa.
 
9. Uishi Katika Falsafa Ya Kutokuwa Na Hofu.
Hofu ni adui katika safari ya mafanikio. Ukishampa nafasi bwana hofu basi umehatarisha maisha yako. Ukiwa na hofu utaogopa kukosea, utaogopa kujaribu na kuthubutu. Katika safari ya mafanikio usiogope kufeli kwani kufeli ni kujifunza. Kama umeanguka jifunze kupitia anguko lako. Ambaye hajawahi kuanguka kamwe hajawahi kupanda waingereza wanasema he who never fell never climbed.
Hivyo usikate tamaa, kukabali kukosea, usiishi na falsafa ya hofu kwani ni utumwa na itakuharibia mambo yako mengi ni bora kuipa hofu talaka na ufunge ndoa na kujiamini ili ufanye mambo yako kwa uhuru zaidi. Dunia leo ingekuwaje kama kila mtu angekuwa na hofu ya kutimiza ndoto yake? Hata wewe una kitu kizuri ambacho ni zawadi kwako na kwa dunia.
 
10. Uwe Mtu Wa Kujali Afya;
Usipokuwa mwangalifu wa afya basi yote unayoyafanya katika safari yako ya mafanikio ni sawa na hakuna. Katika safari ya mafanikio kitu cha kwanza ni afya na huwezi kutimiza wala kufika katika malengo yako yote uliojiwekea. Unatakiwa kujali afya kwani afya ndio utajiri namba moja duniani. Hata gari lako liwe na mafuta lakini kama halina oil basi ujue utaua injini ya gari lako na hatimaye litakufa. Tunza afya yako kwa gharama yoyote ile. Usipotunza afya yako leo utakuja kulipia gharama tena kwa riba kubwa. Usidharau afya kabisa. Ukiwa mgonjwa mambo yako yote yana simama na hata uzalishaji unapungua kwako na familia yako na watu wenye mahusiano mazuri nawe. 
 
Mwisho, uwe na shauku na hamasa ya kutaka kuwa na mafanikio, badilisha marafiki ambao hawaendani na falsafa ya maisha yako, kuwa mtu sahihi utawapata watu sahihi, uwe mtu mwenye uwezo wa kuona fursa, ujenge uhusiano mzuri na watu. Kuwa na kauli mbiu yako moja itakayosimamia yote haya na kukupa hamasa kubwa. Yaani ukiona tu falsafa yako na kuikumbuka hata kama ulikuwa na uvivu wa kufanya jambo Fulani unaisha na unanyanyuka na kwenda kutimiza wajibu wako. Usisahau kuwa na malengo na mipango katika safari yako ya kufunga ndoa na utajiri.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com