Kuweza kufanya na kufanya ni vitu viwili tofauti kabisa. Watu wengi wanasema wanaweza kufanya, lakini cha kushangaza huwaoni wakifanya. Wanasubiri mtu mwingine afanye halafu wao ndiyo waje kukosoa, ya kwamba hata wao wangeweza kufanya vizuri zaidi ya vile ambavyo wengine wanafanya.
Pande mbili za jambo hili.
Upande wa kufanya.
Kama wewe upo upande wa kufanya, yaani umejitahidi kufanya kitu lakini akaja mtu na kuanza kukukosoa ya kwamba yeye angeweza kufanya bora zaidi kuliko ulivyofanya wewe, angalia kwanza kama ameshafanya. Kama ameshafanya jifunze kutoka kwake. Kama hajafanya achana naye mara moja, hawezi kufanya na anaona vibaya mtu mwingine anapojaribu kufanya. Wewe endelea kufanya.
Upende wa kuweza kufanya.
Kama upo upande wa pili, kwamba wewe ndiye unayewaambia wengine ya kwamba ungeweza kufanya vizuri kuliko wao, huna haja ya kupiga kelele, wewe fanya na wataona wao wenyewe. Na kama unaweza kufanya lakini hutaki kufanya, basi kaa kimya kwa sababu hakuna unayemsaidia kwa maneno yako. Watu wanaelewa zaidi vitendo kuliko maneno.
Fanya au kaa kimya, kila mtu anaweza kusema ya kwamba anaweza kufanya, wanaoleta tofauti siku zote ni wale wanaofanya.
SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Ni Unachofanya, Siyo Unachosema.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kufanya na kuweza kufanya ni vitu viwili tofauti. Wengi wamekuwa wakisema wanaweza kufanya ili kujiondoa kwenye maumivu ya kushindwa kufanya. Ila wanaoleta mabadiliko ni wale anaofanya. Mimi nitakuwa mtu wa kufanya, sitapiga kelele kwamba naweza kufanya, badala yake nitafanya na watu watajioneka kwa macho yao.
NENO LA LEO.
Kufanya na kuweza kufanya ni vitu viwili tofauti. Watu wanaosema wanaweza kufanya mara nyingi sio wanaofanya, wale wanaofanya wanachukua hatua bila hata ya kupiga kelele.
Fanya au kaa kimya, kuwaambia watu unaweza kufanya, halafu hufanyi hakuna kikubwa unachosaidia. Pia kuwaambia watu ungeweza kufanya vizuri kuliko wao, kwa nini usifanye? Kusema ni rahisi, kufanya ni changamoto.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.