Kile unachokitaka hasa, ndiyo unachokwenda kukipata, ndivyo maisha yalivyo. Hupati tofauti na unachotaka.
Na hivyo kile unachotaka ndicho kinastahili muda wako na mawazo yako. yafanye mawazo yako kutawaliwa na kile ambacho unakitaka, na tumia muda wako kufanya kitu hiko.
Tunaishi kwenye dunia yenye kelele na mengi yanayotaka akili zetu na muda wetu. Lakini siyo muhimu sana kwetu. Ni lazima tuweze kuyavuka haya kama kweli tunataka kufikia kile ambacho tunakitaka hasa.
Vitu viwili muhimu unavyohitaji ili kupata kile unachotaka vinapatikana kwa uhaba sana. Na hivyo ni lazima uwe na ubahili na vitu hivi. Vitu hivyo ni muda, ambao ni masa 24 tu kwa siku, huwezi kuongeza. Na kitu cha pili ni nguvu zako, ambapo unaianza siku ukiwa na nguvu na kadiri inavyokwenda unapoteza nguvu zako.
Tumia vizuri muda wako na nguvu zako kwa yale mambo ambayo ni ya muhimu zaidi kwako, mengine usiruhusu kabisa yaibe nguvu na muda wako. Yaache kama yalivyo na wewe weka juhudi kwenye kile unachotaka. Hakuna juhudi zitakazopotea, kila unachoweka ndicho unakuja kupata.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Ya Uhakika Ya Kuwafanya Watu Wakupe Kile Unachotaka.
TAMKO LANGU;
Nimejikumbusha ya kwamba ninapata kile ambacho ninakitaka hasa. Na pia nimejua ya kwamba rasilimali mbili muhimu ninazohitaji ili kupata ninachotaka zipo kwa uhaba. Rasilimali hizi ni muda na nguvu, nitakuwa mchoyo wa rasilimali hizi ili niweze kufika kule ninakotaka kufika.
NENO LA LEO.
Kile unachokitaka hasa, ndicho unachokipata kwenye maisha yako. na ili uwe na uhakika wa kupata chochote unachotaka, unahitaji kuwa makini na rasilimali mbili muhimu sana ulizonao; muda na nguvu.
Kuna vitu vingi vinanyemelea rasilimali hizi lazini siyo muhimu kwako. Kuwa mchoyo wa rasilimali hizi na zipeleke kwenye yale ambayo ni muhimu kwako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.