Habari rafiki?
Kwa wale ambao ni waajiriwa mnajua ni kwa jinsi gani ajira za sasa zimekuwa na changamoto nyingi. Kwa sasa nafasi za ajira zimekuwa chache na wanaozihitaji ni wengi. Hali hii inawapa waajiri nguvu kubwa ya kuweza kuchagua ni aina gani ya watu watawaajiri na kwenda nao.
Hali hii pia imeshusha thamani ya kazi za watu wengi. Kwa kuwa wapo wengi wanaoweza kuzifanya, na ambao wapo tayari kuzifanya kwa malipo kidogo kuliko yale ambayo mtu analipwa kwa sasa, imekuwa vigumu kwa wengi kuomba kuongezewa kipato. Kwa kuwa wengi waliopo kwenye ajira wameshatengeneza utegemezi kwenye ajira hizo, hali kama hii inafanya maisha yao kuzidi kuwa magumu.

BONYEZA HAPA KUPATA KITABU HIKI

 
Leo kupitia makala hii tunakwenda kujifunza njia moja ya uhakika ya kuongeza thamani ya kazi yako na kuongeza kipato chako pia. Na hii ni kwa watu wote iwe umeajiriwa au umejiajiri mwenyewe. Kwa sababu hata kwenye kujiajiri na biashara kuna wengi wanaofanya kile unachofanya, hivyo thamani inakuwa ndogo na kipato kidogo pia.
 
Njia ya uhakika ya kuongeza thamani ya kazi yako.
Njia ya uhakika ya kuongeza thamani ya kazi yako ni kutengeneza hali ya kutegemewa kupitia kile ambacho unakifanya. Hapa unatafuta jinsi ambavyo unaweza kuwafanya wengine wakutegemee sana wewe ili mambo yao yaweze kwenda vizuri. Kama ni kwenye ajira mwajiri wako na wafanyakazi wenzako wakutegemee sana wewe ili kazi zao ziweze kwenda vizuri. Kama ni kwenye biashara mteja wako akutegemee sana wewe ili mambo yake yaweze kwenda vizuri.
Hii ni njia nzuri na ya uhakika ya kuongeza thamani ya kazi yako na uzuri ni kwamba inaanza na wewe mwenyewe. Haihitaji nguvu kubwa kutoka nje, bali inaanzia ndani yako.
Hali hii ya kutegemewa ni nzuri kwako wewe kwa sababu unakuwa na kitu unachotoa ambacho wengine hawawezi kukitoa. Inaweza kuwa jinsi unavyofanya kazi yako, inaweza kuwa jinsi unavyoshirikiana na wengine, inaweza kuwa jinsi unavyosaidia wengine na kadhalika.

SOMA; Njia 4 Zinazoweza Kuboresha Utendaji Wako Unapokuwa Kazini

Unawezaje kutengeneza hali hii ya kutegemewa?
Ni rahisi kutengeneza hali hii ya kutegemewa kwenye kazi unayoifanya. Na hizi hapa ni hatua ambazo unaweza kuzipitia kutengeneza hali hiyo.
Kwanza angalia ni eneo lipi la kazi yako unapenda kulifanya kwa utofauti na kwa kwenda hatua ya ziada. Wewe unaijua kazi yako au biashara yako, na unayajua majukumu yako vizuri. Angalia ni majukumu yapi unapenda kuyakamilisha kwa ubora na kwa kwenda hatua ya ziada. Majukumu haya ndiyo unayoweza kutengeneza utegemezi wa wengine.
Pili angalia uhitaji wa wengine kwa majukumu yale. Kwa yale majukumu ambayo unapenda kuyafanya, angalia ni kwa jinsi gani wengine wanayahitaji. Kadiri ambavyo watu wanayahitaji na kuyategemea ndivyo thamani ya majukumu hayo inavyozidi kuwa kubwa. Angalia ni jinsi gani watu wanaweza kuathirika kwa kukosa kitu fulani ambacho unakifanya wewe. Chagua moja au machache ambayo unaweza kuyafanyia kazi na kutengeneza utegemezi.
Tatu kuwa bora sana kwenye jukumu au majukumu hayo uliyochagua kwenye hatua ya pili. Kwa kuwa umeshajua ni majukumu yapi ambayo wengine wanayategemea, sasa unahitaji kuwa vizuri sana kwenye majukumu hayo. Unahitaji kuwa bora sana na uweze kutoa matokeo mazuri kwa kila unachokifanya. Kwa njia hii utawapatia wengine kile ambacho wanakitaka na hakuna sehemu nyingine au mtu mwingine anayeweza kuwapatia kwa njia hii. Hapa unakuwa mbunifu na kuangalia ni wapi ambapo watu hawaridhishwi na unaongeza juhudi kwenye eneo hilo. Kadiri wengi wanavyokutegemea moja kwa moja, na kadiri kile unachofanya kinavyokuwa na thamani kubwa ndivyo unavyoongeza thamani ya kazi yako na kuweza kuongeza kipato chako pia.

SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.

Utajuaje kama kwenye kazi yako watu wanakutegemea?
Ni vizuri kujua kama kwenye kazi unayoifanya kuna watu wameshatengeneza utegemezi kwako. Hii pia itakuwezesha kujua ni maeneo gani unaweza kutengeneza utegemezi zaidi. Kujua hili angalia ni kitu gani ambacho watu wakishindwa ni lazima waje kwako. Kwa kazi unayofanya au biashara yako, kuna vitu ambavyo watu wakishindwa lazima waje kwako. Watahangaika kwa wengine wote ila watakuwa na uhakika kwamba wakifika kwako watapata suluhisho. Jiulize ni mambo gani ambayo umeshaweza kufikia hatua hii kwenye kile unachofanya. Jua ni maeneo gani ambayo watu watakutafuta kwa njia yoyote. Na kama ukifikiria huoni maeneo hayo ambayo watu wanakuja kwako kupata suluhisho, basi jua hakuna kikubwa unachofanya, upo upo tu.
Njia nyingine ya kujua kama unategemewa au la ni kuangalia wakati unapokuwa umekosekana. Kama imetokea hupo kazini au kwenye biashara yako, ni kitu gani ambacho watu wanakikosa. Je watu wanakutafuta au kukusubiri mpaka urudi ndiyo wakamilishe mahitaji yao? Kwa njia hii utaona ni kwa jinsi gani watu wameshatengeneza uhitaji mkubwa kwako na wapo tayari kukusubiri wewe ili wapate kile wanachotaka. Kwa sababu wanajua ni kupitia wewe pekee ndiyo wanaweza kupata wanachotaka.
Kadiri unavyoweza kuwafanya wengine wakutegemee kwa kile unachofanya, ndivyo unavyoongeza thamani ya kazi au biashara yako. Hiki ni kitu ambacho unaweza kuanza kukifanya sasa na kujitengenezea fursa kubwa kwa mbeleni. Ila unahitaji kuwa makini usijione ya kwamba umeshinda pale ambapo watu wameshaanza kukutegemea. Kwa sababu unapoona ya kwamba umefika, utaacha kuboresha zaidi na watakuja wengine wanaofanya kwa ubora na wale wanaokutegemea watapata mtu mwingine wa kumtegemea.

SOMA; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Usikubali kuwepo tu kusukuma siku, bali kazana uwe na mchango wa kipekee kupitia kile ambacho unakifanya, ambao wengine watauona na kuuthamini. Hii ndiyo inaleta ubora wa kazi na maisha pia na itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kutengeneza utegemezi wa wengine kwenye kile unachokifanya.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz