Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, inakuwa rahisi kwetu kufanya jambo kama kila mtu anakubaliana na sisi na yupo tayari kutusaidia. Ni salama zaidi kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, au wanakushauri kufanya. Kwa sababu kama utashindwa basi watakusaidia.

Lakini hivi unavyolazimika kufanya siyo vile ambavyo ni bora kwako, na siyo vitakavyokufikisha kwenye mafanikio unayotarajia. Utaishia kufanya vile ambavyo ni vya kawaida na hivyo kupata majibu ambayo ni ya kawaida.

Ili uweze kufikia malengo yako na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, ni lazima ufanye vitu tofauti na wengine wanavyofanya. Na hapa unajiweka kwenye hatari kubwa, kwa sababu wanaokuzunguka watakupinga, wataona unakosea na unajiweka kwenye hatari. Kikubwa zaidi hawatakusaidia pale utakaposhindwa, kwa sababu watakuambia walikuonya lakini hukusikia.

Hali hii imekuwa inawafanya wengi kuua ndoto zao. Kuacha malengo yao na kufanya kile ambacho kitawafurahisha wengine, kwa sababu ni salama kuwa kwenye kundi la wengi.

Wewe usikubali kuingia kwenye mtego huu, ni lazima uweze kusimama wewe mwenyewe, ni lazima uchague kufanya kile ambacho unajua ni muhimu kwako na hata kama utashindwa ukubali matokeo na kuanza tena, wewe mwenyewe. Hivi ndivyo wote walioshinda walivyopita, haikuwa rahisi lakini walipofanikiwa, kila mtu alikuwa pale kushangilia. Unapowategemea wengine kwa kila kitu unakuwa umewapa ruhusa ya kufanya maamuzi yote ya maisha yako.

Siyo safari rahisi ndiyo maana ni wachache sana wanaoweza kuifuata. Kuwa mmoja wa hao wanaoifuata njia hii na weza kusimama mwenyewe. Na utakapochagua kusimama mwenyewe haitakuchukua muda mrefu kabla hujapata watakaokuwa tayari kusimama na wewe. Thubutu kusimama mwenyewe, ndiyo njia ya uhakika ya kufika pale unapotaka kufika.

SOMA; Njia 30 Za Kufikia Mafanikio Makubwa Sana(World Class)

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kikwazo kikubwa kwangu kuishi maisha ambayo ni bora kwangu ni watu wanaonizunguka, hasa wale ambao ni wa karibu kwangu. Na ili niweze kuondokana na kikwazo hiki nahitaji kuweza kusimama mwenyewe. Ninapowategemea wengine moja kwa moja ninawapa nguvu ya kunifanyia maamuzi, lakini ninapoweza kusimama mwenyewe nawavutia wale wanaoweza kwenda na mimi na hivyo kufika ninapotaka.

NENO LA LEO.

Ili uweze kupata kile hasa unachotaka kwenye maisha yako, unahitaji kuweza kusimama mwenyewe. Unapowategemea wengine kwa kila kitu, unawapa ruhusa ya kufanya maamuzi yote ya maisha yako. na ubaya ni kwamba maamuzi watakayoyafanya siyo bora kwako.

Amua kusimama mwenyewe na usiogope pale wengine wanapokuwa tofauti na wewe. Kwa kusimama mwenyewe utawavutia wale wenye mtazamo kama wako na mtaweza kufanya makubwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.