Jambo moja la kushangaza kuhusu maisha ni kwamba ili uweze kupata kile unachotaka, ni lazima ufanye kile usichotaka kufanya. Huu ndiyo ukweli wa maisha na hakuna namna unaweza kuukwepa.
Kama unataka kuwa na afya bora ni lazima ule vyakula ambavyo hupendi kula, mara zote vile vyakula unavyopendelea kula huwa siyo vinavyoleta afya bora. Utahitaji kula vyakula ambavyo kwa hali ya kawaida na maendeleo tuliyonayo, utaona siyo vizuri kama unavyopendelea wewe.
Kama unataka kupata mafanikio ni lazima uweke juhudi kubwa sana kwenye kile unachofanya. Ni lazima uwe tayari kuweka muda wa ziada kuliko wengine wanavyoweka. Ni lazima ujinyime muda wa kustarehe na badala yake ufanye kazi. Mwili wako utataka kustarehe lakini wewe utahitaji uulazimishe kufanya kazi.
Chochote kikubwa unachotaka kwenye maisha yako, hutaweza kukipata kama utaendelea kufanya kile ambacho unachotaka kufanya, au kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Kwa sehemu kubwa utahitaji kufanya vitu ambavyo haupo tayari kufanya, kutokana na ugumu wake au kwa kutokuwa vinavutia kufanya. Na hiki ndiyo kinachotofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wanaofanikiwa wanafanya vitu ambavyo wanaoshindwa hawafanyi. Na ukweli ni kwamba siyo kwamba wanaofanikiwa wanakuwa wanataka kufanya vitu hivyo, ila wanajua hawana namna bali kufanya. Anza na wewe kufanya vile usivyotaka kufanya, na utapata kile unachotaka kupata.
SOMA; Hivi Ndivyo Waajiriwa Wanavyopoteza Uhuru Wao Wenyewe, Na Jinsi Ya Kuudai Tena.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba ili nipate kile ninachotaka, ni lazima nifanye kile ambacho sitaki kufanya. Vile ambavyo sitaki kuvifanya ndivyo vyenye thamani kubwa kwangu kuweza kufikia mafanikio. Nitafanya kila ambacho ni muhimu kufanyika ili kufikia mafanikio, bila ya kujali napenda kukifanya au la.
NENO LA LEO.
Ili upate kile ambacho unataka kupata, ni lazima ufanye kile ambacho hutaki kufanya.
Kama unataka kuwa na afya bora unahitaji kula vyakula ambavyo hupendi kula.
Ili ufanikiwe ni lazima uweke juhudi kubwa kwenye kazi yako kuliko ulivyo tayari kuweka.
Hakuna kilicho bora kinakuja kirahisi, unahitaji kujitoa ili kupata kilicho bora.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.