Ni jambo lililo wazi ya kwamba kwa sasa kusoma siyo uhakika wa kupata ajira kama ilivyokuwa zamani. Zamani ilikuwa uhakika kwamba ukimaliza masomo unapata ajira, ila kwa sasa nafasi za ajira ni chache ukilinganisha na idadi ya wahitimu wa elimu za kitaalamu. Hivyo mwanafunzi wa chuo kufikiria ajira pekee ni kujiweka kwenye wakati mgumu.
Huu ni wakati wa kuanza kuangalia mambo mengine ambayo mtu anaweza kufanya tofauti na ajira. Ili pale inapotokea amekosa ajira baada ya kuhitimu masomo, aweze kuwa na kitu cha kumwezesha kusimama na kuendesha maisha yake. Ha hapa ndipo unapokuja umuhimu wa kufanya biashara.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.

 
Lakini pia biashara siyo kitu rahisi kuingia kama mtu anavyoweza kusema au kufikiri. Kuna changamoto nyingi kwenye kuingia na kufanya biashara kama mtu hujajiandaa vizuri utashindwa kuhimili kwenye biashara. Leo kwenye kipengele chetu cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufikia mafanikio tutaangalia jinsi ya kuingia kwenye biashara baada ya kuhitimu masomo. Kuna wahitimu wengi na wengine wanaelekea kuhitimu ila bado hawajajua mbinu bora za kuingia kwenye biashara. Leo tutajifunza mambo yote muhimu hapa.

Kabla hatujaingia ndani na kuona ni jinsi gani mtu anaweza kuingia kwenye biashara baada ya kuhitimu elimu yake, tuangalie kwanza maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kuhusu changamoto hii;
Niko Mtwara mjini ni mwanafunzi wa chuo mwaka wa mwisho. Nina malengo ya kufanya biashara ila sina mtu yoyote ninae mfahamu kwa msaada wa kupata eneo, usimamizi kama partner nina idea nyingi tu. Na kikubwa nahitaji anza maisha ya ku fight mkoani hapa, hapa kuna fursa nyingi ila ushirikiano, ndio hakuna baina ya wenyeji na wageni, hivyo kama yupo ambaye anapatikana Mtwara Lets do business. Z. Kundael.

Ndugu Kundael, hongera sana kwa kuwa na mpango wa kuingia kwenye biashara baada ya kuhitimu masomo yako ya chuo. Ni njia bora uliyoichagua mapema, kwa sababu wakati wenzako wakiendelea kuzungusha bahasha bila ya majibu ya uhakika, wewe utakuwa unaweka juhudi kwenye biashara yako. kama hutakata tamaa utaweza kukuza biashara yako na hatimaye kuweza kuajiri watu wengine. Hapa nataka nikushauri mambo matatu muhimu kulingana na ulivyoomba ushauri hapo juu. Karibu uyapitie na ufanye maamuzi ni hatua ipi utakayochukua kwenye maisha yako.

Jambo la kwanza; mawazo mengi ya biashara.
Kama ulivyosema kwenye maelezo yako hapo juu ni kwamba una mawazo mengi ya kibiashara. Hongera sana kwa mawazo hayo mengi uliyonayo, nina uhakika yote yanakuhamasisha na yanaonekana kuwa mawazo bora. Lakini hapa kuna changamoto moja, huwezi kutekeleza mawazo yote kwa wakati mmoja. Na kingine ambacho unaweza usikifurahie ni kwamba mawazo uliyonayo ya biashara yanaweza yasiwe bora kama unavyofikiri. Huenda hamasa uliyonayo ndiyo inakufanya uone mawazo uliyonayo ni ya kipekee sana. Lakini ukweli ni kwamba kila wazo lina changamoto zake, na itakuchukua muda mpaka biashara iweze kusimama kweli.

Hapa unahitaji kuchagua wazo moja ambalo utaanza kulitekeleza. Wazo hili litokane na vitu ambavyo tayari unavipenda na kuwepo na watu wenye matatizo au changamoto ambazo unaweza kuzitatua kupitia wazo lako hilo. Pia wazo hilo uweze kuanza kidogo na kulikuza kadiri siku zinavyokwenda. Pia jua utakutana na changamoto, hivyo chagua wazo ambalo upo tayari kuteseka nalo. Mambo siyo mteremko kama unavyofikiri kwa sasa, ukiingia kwenye biashara utakutana na mengi ambayo hukuyafikiria wakati unapanga mawazo yako ya kibiashara.

SOMA; USHAURI; Biashara Nzuri, Inayolipa Na Unayoweza Kuifanya.

Jambo la pili; kupata mshirika bora wa kibiashara.
Kama ulivyoeleza hapo juu, unahitaji mtu wa kushirikiana naye kwenye biashara. Lakini jambo hili umelipa uzito mdogo sana kama vile ni jambo dogo. Kuchagua mshirika wa kibiashara siyo jambo dogo kama ulivyoonesha kwenye maelezo yako, kwamba kama kuna mtu yeyote yupo tayari basi aje mfanye biashara. Huchagui tu mtu yeyote na kuanza kufanya naye biashara, hata kama atakupa maneno mazuri kiasi gani.

Kama nilivyoeleza hapo juu, biashara zina changamoto, hivyo unahitaji kupata mtu ambaye mnaweza kwenda naye vizuri katika nyakati zote za biashara. Unahitaji mtu ambaye ana mtizamo chanya, anajituma, ni mwaminifu na mwadilifu. Unahitaji mtu ambaye ni mtendaji hasa na mwenye ndoto kubwa za kufanikiwa kupitia biashara kama wewe. Awe na malengo ya muda mrefu na siyo kukimbilia biashara kwa kufikiri ndiyo njia ya haraka ya kufanikiwa.

Mara zote huwa ninasema unapochagua mtu wa kushirikiana naye kwenye biashara unahitaji kuwa makini kuliko unapochagua mke au mume. Mke au mume unachagua kwa hisia za mapenzi, lakini biashara hazihitaji hisia, unahitaji mtu mwenye sifa ambazo zitaiwezesha biashara kukua. Ukiweka hisia tu unakwenda kuharibu kabisa, na utapata mtu ambaye atakuwa mzigo kwako. Fanya uchunguzi wa kina na mjue mtu vizuri kabla hujakubali kufanya naye biashara. Tabia za mtu zinaathiri biashara moja kwa moja, hakikisha unachagua mtu mwenye tabia bora.

SOMA; Huyu Ni Kijana Wa Kitanzania Aliyeanza Biashara Kwa Mtaji wa Milioni Nne na Baada Ya Miaka Mitatu Ana Zaidi Ya Milioni Mia Moja.

Jambo la tatu; acha kulalamika.
Katika maelezo yako, unaonekana kulalamika kwamba kwa eneo ulilopo watu hawatoi ushirikiano mzuri, hasa kwa wageni. Hizi ni dalili za kulalamika, kitu ambacho ni sumu kubwa kwenye mafanikio ya biashara. Biashara hazihitaji mtu wa kulalamika na kulaumu wengine, bali zinahitaji mtu anayeona nafasi na kuitumia, anayejituma na kupambana na vikwazo vyote vinavyomzuia kufanikiwa kupitia biashara yake.

Inawezekana unachosema ni sahihi, lakini sina hakika kama umeshajaribu kuchukua hatua zozote za kulivuka hilo. Huenda ni maneno yanayosemwa na wengi, na wewe ukaamua kuyachukua. Nina uhakika kama ukiachana na maneno hayo na kuanza kujenga mahusiano mazuri na wenyeji mtaweza kufanya biashara vizuri. Kikubwa ni uache kuhukumu kwamba watu hawaoneshi ushirikiano na anza wewe kuonesha ushirikiano, chagua watu ambao unaona mnaweza kwenda pamoja, na anza kujenga nao mahusiano mazuri. Kadiri siku zinavyokwenda mtajenga kuaminiana na mnaweza kufanya biashara vizuri, iwe ni kwa kuwa washirika kwenye biashara au kuwa wateja wa biashara yako.
Unapoingia kwenye biashara, kama kuna kitu hukitaki au hukipendi kibadilishe, na kama huwezi kukibadilisha basi achana nacho. Kulalamika au kulaumu ni kupoteza muda wako ambao ungeweza kuutumia kukuza biashara yako.

SOMA; Biashara Ndani Ya Ajira; Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.

Nihitimishe kwa kusema kwamba kama malengo yako ni kuingia kwenye biashara baada ya kuhitimu masomo, chagua ni biashara ipi unakwenda kuanza nayo. Chagua ni watu gani unaoweza kushirikiana nao na jiandae kukutana na changamoto na hata kushindwa. Sikuambii hivi ili ukate tamaa, bali nataka uwe na picha halisi ya kibiashara ili usije ukakata tamaa pale utakapoanza na kukutana na vitu hivyo. Kuwa mtu wa kuchukua hatua, utaweza kuikuza biashara yako bila yakujali ni changamoto zipi unazipitia.
Nakutakia kila la kheri katika biashara unayokwenda kufanya, iwe na mafanikio makubwa kulingana na juhudi unazochagua kuweka.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
 
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.