Pale tunapotaka kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa, tunajua tunahitaji kufanya mambo makubwa ambayo hatujawahi kufanya hapo awali. Na hapa ndipo tunagundua ya kwamba hatuna uwezo huo na hivyo kuhitaji uwezo kutoka nje yetu.

Tulipokuwa watoto tulikuwa tunajipa sababu ya udogo na hivyo kusema tukiwa wakubwa tutafanya kitu fulani. Cha kushangaza tunafikia ukubwa lakini bado hatujapata kile ambacho tunataka kwenye maisha yetu.

Hii imekuwa inasababishwa na tabia ya kusubiri. Ni kama tumekuwa tunamsubiri mtu aje atupe nguvu za kufanya, aje atupe hamasa ya kuweka juhudi ili kupata kile ambacho tunakitaka.

Leo nina habari njema kwako kuhusu mtu huyu ambaye umekuwa unamsubiri siku zote. Habari hizi njema ni kwamba mtu huyu ameshafika, na amefika kimya kimya. Ni wewe mwenyewe unatakiwa kujua uwepo wake na kuweza kuutumia ili kuweza kupata kile ambacho unataka kupata.

Mtu huyo ni wewe mwenyewe kwenye mtazamo chanya wa maisha yako. unahitaji kubadili mtazamo wako wa maisha kama unataka kupata kile unachotaka kwenye maisha. Unahitaji kuondoka kwenye fikra za siwezi na kwenda kwenye fikra za naweza. Unahitaji kuacha kujiambia huwezi na uanze kujiuliza unawezaje?

Hakuna mtu mwingine atakayekuja kukutoa hapo ulipo zaidi yako wewe mwenyewe. Ni uamue sasa kuinuka na kuchukua hatua, au uendelee kusubiri milele. Ila unachotakiwa kukumbuka ni kwamba muda haukusubiri.

Shujaa uliyekuwa unamsubiri tayari ameshafika, tambua uwepo wake kwa kubadili mtazamo wako na upate kile unachotaka.

SOMA; SIRI YA 12 YA MAFANIKO; Shika Hatamu Ya Maisha Yako.

TAMKO LANGU;

Ninajua ya kwamba hakuna mtu mwingine anayeweza kunitoa hapa nilipo na kunifikisha pale ninapotaka kufika ila mimi mwenyewe. Najua ya kwamba mimi ndiyo shujaa mkubwa wa maisha yangu. Nitatengeneza mtazamo bora wa maisha yangu ambao utanipa hamasa ya kuchukua hatua ili niweze kufikia yale maisha ya ndoto zangu.

NENO LA LEO.

Ulipokuwa mtoto ulikuwa unasema nikiwa mkubwa nitafanya hiki na kile, lakini umekuwa mkubwa na bado hufanyi.

Unajua tatizo ni nini? Tatizo ni mtazamo ulionao juu ya maisha yako. unachotakiwa kujua ni kwamba wewe ndiye shujaa wa maisha yako, chochote unachotaka utakipata kama utaweka juhudi. Na hakuna yeyote anayeweza kukutoa hapo ulipo zaidi yako mwenyewe. Chukua hatua.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.