Habari rafiki?
Ni imani yangu kwamba uko vyema na unaendelea kuweka juhudi kwenye kufanyia kazi malengo na mipango yako ya kuwa na maisha bora na ya mafanikio. Najua unajua ya kwamba hakuna mtu mwingine wa kukuletea wewe maisha bora wala mafanikio, hili ni jukumu lako mwenyewe na unahitaji kuweka juhudi kubwa ili kuweza kufikia maisha hayo. Hongera sana kwa kujua hilo na kulifanyia kazi.

Aliyekuwa mwandishi na mchekeshaji kutoka nchini Marekani Mark Twain aliwahi kunukuliwa akisema kuna siku mbili muhimu sana kwenye maisha ya kila mwanadamu. Siku ya kwanza ni ile siku anayozaliwa, na siku ya pili ni ile siku ambayo anajua kwa nini amezaliwa. (“The two most important days in your life are the day you are born and the day you find out why.” ― Mark Twain)
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA


Kila mtu anaijua siku yake ya kuzaliwa, yaani kila mtu anajua ya kwamba alizaliwa na wengi wanazijua kabisa tarehe za siku walizozaliwa. Lakini ni wachache sana wanaopata bahati ya kujua kwa nini walizaliwa. Nasema ni bahati kwa sababu hakuna mtu yeyote anayeweza kumwambia mtu kwa nini alizaliwa, yaani alizaliwa ili kuja kufanya nini. Wazazi watajaribu kubashiri lakini hawawezi kupatia, walimu watajaribu kukutengenezea njia wanayoona ni sahihi lakini hawawezi kujua ukweli wako. Na hata jamii itakazana kukulazimisha ni kipi ufanye, lakini itakuwa inakosea.
Hili ni zoezi ambalo mtu analifanya mwenyewe na siyo wengi wanaoweza kupata nafasi ya kufanya zoezi hili. Kwanza tuzungumzie siku ya kwanza na wakati mwingine tutajadili siku hiyo ya pili muhimu.
Siku unapofika hapa duniani ni siku muhimu sana kwa kila mwanadamu. Ni siku ambayo unaipata fursa ya kuweza kuonja maisha haya ya dunia kwa kipindi kifupi sana. Ambacho kama utakitumia vizuri utaweza kufurahia na kutoa mchango wako kwa wengine.
Siku yangu ya kwanza ilikuwa tarehe 28 mwezi wa tano, ambapo juzi jumamosi ilikuwa siku ya kuadhimisha siku yangu ya kuzaliwa.

Lengo la kuandika makala hii ya leo ni kutoa shukrani kwa marafiki zangu wote kwa jinsi ambavyo mmenitumia salamu za siku yangu ya kuzaliwa. Mmeniandikia jumbe nzuri sana ambazo zimenihamasisha zaidi na kunifanya nione nina deni kubwa la kuendelea kufanya hiki ninachofanya, tena kwa ubora wa hali ya juu.
Nimepokea salamu kutoka kwa marafiki zangu wengi ambao ni wasomaji wangu na hata marafiki wa kwenye mitandao ya kijamii. Pia nimepokea zawadi kutoka kwa marafiki ambao tupo pamoja kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA. Tarehe 28 mwezi huu wa tano imekuwa siku ya hamasa kubwa kwangu kwa jinsi ambavyo ninyi marafiki zangu mmenijali.
Maneno ya shukrani naona kama hayatoshi, nazidi kusema asante.

Ahadi yangu kwenu marafiki.
Nawaahidi ya kwamba tutaendelea kuwa pamoja, tukishirikishana maarifa bora ili kila mmoja wetu aweze kuishi maisha ya ndoto yake, maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa.
Nawaahidi kwamba tunakwenda kujenga mafanikio yaliyokamilika kwenye maisha yetu, kwa kuangalia maeneo matano muhimu ya maisha yetu ambayo ni maisha binafsi, kazi au biashara, fedha, mahusiano na imani, na afya. Haya ni maeneo ambayo yanategemeana sana ili kuweza kuwa na maisha bora, na hatutaacha hata moja nyuma.
Nawaahidi ya kwamba tutaendelea kusaidiana ili kila mmoja wetu aweze kujua dhumuni la yeye kuwepo hapa duniani, kwa sababu kuna wengi ambao mmejikuta tu hapa duniani, ambapo tayari mmeshadanganywa na kila mtu lakini bado mnaona kuna kitu kinakosekana kwenye maisha yenu.
Na mwisho kabisa nawaahidi ya kwamba ndoto zangu ambazo nimekuwa nawashirikisha mara kwa mara bado zipo pale pale na nina uhakika mkubwa wa kuzifikia. Na ndoto kubwa kabisa ni kuwa raisi wa nchi yetu Tanzania mwaka 2040.
SOMA; Tumia Siri Hii Moja Kupata Chochote Unachotaka Kwenye Maisha Yako.

Ombi langu kwenu marafiki.
Kama umekuwa rafiki yangu na msomaji wa kazi zangu, nina maombi muhimu sana kwako.
Endelea kuwashirikisha watu wengi zaidi makala unazosoma kwenye AMKA MTANZANIA na waalike nao wajifunze kupitia makala hizi.
Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo tutakuwa karibu zaidi kupitia kundi la wasap, tutajifunza mengi na kupeana hamasa ya kuweka juhudi zaidi ili kufikia maisha ya ndoto zetu. Kama ungependa kujiunga nitumie ujumbe kwa wasap kwenye namba 0717396253.
Endelea kujifunza kila siku, kwa kila nafasi unayopata jifunze, na fanyia kazi yale ambayo unajifunza. Haijalishi unajua vitu bora na vingi kiasi gani, kama huwezi kuvitumia kuboresha maisha yako havina maana kwako.
Asante sana rafiki yangu kwa kuendelea kuwa pamoja na mimi kwenye safari hii. Nakusihi tuendelee kuwa pamoja zaidi, hiki ni kitu nilichochagua kufanya kwa maisha yangu yote hapa duniani, kuna mengi ya kujifunza na kuboresha kwenye maisha yetu.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako.
Makirita Amani.
makirita@kisimachamaarifa.co.tz