Rafiki yangu mpendwa,

Leo tarehe 28/05/2021 ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwangu, siku niliyokuja hapa duniani miaka 33 iliyopita.

Katika kipindi hiki kifupi ambacho nimekuwa hapa duniani, nimepata fursa ya kujifunza mengi kuhusu maisha, watu na mafanikio kwa ujumla kupitia vitabu zaidi ya elfu moja nilivyosoma na kusikiliza na kufanya kazi na watu mbalimbali.

Tarehe 25/12/1999 Majengo Kwa Mtei Moshi nikiwa na dada zangu.

Kwa miaka sita iliyopita, tangu 2015 nimekuwa naandika makala maalumu ya siku ya kuzaliwa kwangu, nikishirikisha yale niliyojifunza kwenye maisha na kutoa mwelekeo wa jinsi huduma mbalimbali ninazotoa zitakwenda kwa mwaka unaofuata.

Mwaka 2015 nilishirikisha kitu cha kufanya ili kuboresha maisha yako.

Mwaka 2016 nikashirikisha siku mbili muhimu kwenye maisha yako.

Mwaka 2017 nilishirikisha mambo 29 niliyojifunza kwenye miaka 29 ya maisha yangu.

Mwaka 2018 nikajiwasha moto na kuweka azimio la muongo wa maisha yangu.

Mwaka 2019 nikajipa jukumu kuu kwamba kazi yangu ni wewe.

Mwaka 2020 nikajiwekea lengo la kuandika vitabu 100 ndani ya miaka 10.

Mwaka huu 2021 nina ujumbe muhimu sana kwako, ujumbe utakaokuwezesha kuyabadili maisha yako na kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Kabla ya kukupa ujumbe niliokuandalia leo nichukue nafasi hii kukushukuru sana wee rafiki yangu kwa namna ambavyo tumekuwa pamoja tangu nimeanza kutoa huduma hii rasmi mwaka 2013.

Kila nikikumbuka tulipoanzia na jinsi mambo yalikuwa magumu, najua bila ya uwepo wako nisingeweza kupiga hatua na kufika hapa nilipo sasa. Ukuaji wa huduma ninayotoa umekuwa unatokana na ninyi marafiki zangu, pale mnapotaka zaidi kutoka kwangu ndipo nachukua hatua na huduma inakua.

Mfano tulianza na AMKA MTANZANIA ambapo makala zilikuwa bure kabisa kusoma. Wapo waliosoma na kufanyia kazi, wakaona matokeo mazuri na kunitafuta wakitaka mafunzo na ushauri zaidi, na hapo ndipo nikaanzisha KISIMA CHA MAARIFA.

Hivyo kutoka ndani ya nafsi yangu kabisa namshukuru kila ambaye amewahi kusoma makala na vitabu nilivyoandika, kwa sababu amechangia sana kukua kwa huduma hii.

Siyo kazi rahisi kutoa maarifa chanya kwenye jamii yetu ya Kitanzania, jamii iliyojaa watu waliokata tamaa na ambao wanafurahia kuwakatisha wengine tamaa. Lakini uwepo wa wachache ambao wanaelewa maarifa haya na kuyafanyia kazi kisha kufanikiwa inanipa moyo kuendelea na huduma hii.

Kama ambavyo nimewahi kuahidi huko nyuma, uandishi na utabibu ni vitu ambavyo nitavifanya kila siku ya maisha yangu mpaka siku naondoka hapa duniani, hivyo uwepo wako unanisaidia kukamilisha azimio hilo. TIMU.SOMA.ANDIKA ni maneno matatu ninayoyafanyia kazi kila siku.

Malengo yangu makubwa mawili bado yako pale pale na sijawahi kuyumba kuhusu kuyafikia. Najua wapo ambao walinijua baada ya kuyatangaza malengo hayo makubwa wazi kwa kila mtu, wengi wakiniambia hayawezekani na ushauri mwingine wa aina hiyo. Lakini sijawahi kuyumba kwenye malengo hayo mawili ambayo ni KUWA BILIONEA mwaka 2030 na kuwa RAISI WA TANZANIA mwaka 2040. Huhitaji kubishana na mimi kama yanawezekana au la, wewe niangalie katika hicho kipindi.

SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2017

Baada ya utangulizi huo muhimu, sasa nikushirikishe ujumbe muhimu wa siku hii ya kuzaliwa kwangu.

VITU VIWILI VYA KUFANYIA KAZI KWENYE MAISHA YAKO.

Ili uweze kufikia mafanikio makubwa na kuacha alama hapa duniani, kuna vitu viwili vikubwa unavyopaswa kuvifanyia kazi. Nimeweza kuja na vitu hivi viwili baada ya kujifunza na kutafakari kwa kina na kuona jinsi watu wanahangaika na mambo mengi lakini hawapati matokeo yoyote makubwa.

Ukiamua kuachana na mengine yote unayohangaika nayo na kufanyia kazi haya mawili tu, utaacha alama kubwa hapa duniani.

Mambo hayo mawili ni KUJUA NA KUISHI KUSUDI LAKO na KUWA NA NDOTO KUBWA unazofanyia kazi kwenye maisha yako. Haya mawili tu ndiyo yanahitaji muda, umakini na nguvu zako zote ili uweze kufanya makubwa.

KUSUDI LA MAISHA YAKO.

Mark Twain amewahi kusema kuna siku mbili muhimu kwenye maisha ya mwanadamu, siku ya kuzaliwa kwake na siku anayojua kwa nini amezaliwa.

Kila mtu huwa anazaliwa, ndiyo njia pekee ya kuja hapa duniani. Lakini ni wachache sana wanaojua kwa nini walizaliwa na hao ndiyo wanaoleta matokeo makubwa na kuacha alama hapa duniani.

Ubaya ni kwamba kujua kwa nini umezaliwa ni wajibu wako mwenyewe, hakuna anayeweza kukufundisha wala kukuambia. Hata wazazi waliokuzaa hawajui kwa nini ulizaliwa. Walimu wanaokufundisha ndiyo kabisa wanaharibu, maana wanakulazimisha uwe kitu kingine na siyo wewe.

Unahitaji mabadiliko makubwa kwenye maisha yako ili uweze kujua kwa nini ulizaliwa, unahitaji kuvunja mazoea mengi uliyojenga kwenye maisha yako ili uweze kuisikiliza sauti ya ndani yako na kujua kwa nini uko hapa duniani.

Wengi hawajui kusudi la maisha yao kwa sababu wameamini kile ambacho jamii na mfumo wa elimu umewalisha kwa miaka mingi. Kama shule ilikuambia umefeli kwa sababu huna akili, unaamini hivyo kwamba huna akili. Wakati shule haiwezi kupima uwezo mkubwa ulio ndani yako, kitu ambacho shule inapima ni kukariri.

SEMINA YA UZINDUZI WA VITABU 2019

KUJUA KUSUDI, SEMA NDIYO KWA KILA KITU.

Ili uweze kujua kusudi la maisha yako unahitaji kurudi kwenye maisha ya utoto wako, na kusema ndiyo kwa kila kinachokuja mbele yako. Jaribu mambo mengi uwezavyo, fanya kila kinachokuvutia kufanya na kadiri unavyofanya hivyo utaona kuna vitu unapenda kuvifanya vizuri zaidi na watu wanavifurahia unapovifanya. Hapo ndipo utajua kusudi lako lilipo na kuweza kulifanyia kazi.

Nilijua kusudi la maisha yangu baada ya njia iliyokuwa imenyooka kuzimika ghafla. Nilikuwa muumini mzuri wa falsafa ya nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri.

Nikasoma kwa bidii sana, nikapata ufaulu wa juu sana na kuchaguliwa kusoma udaktari. Nikiwa mwaka wa tatu, tarehe 15/10/2011 nilisimamishwa masomo ya chuo kikuu kwa muda usiojulikana kwa kushiriki kwenye maandamano.

SIKU YA MGOMO ULIOPELEKEA NIFUKUZWE CHUO (kwenye picha nimevaa miwano na suruali ya kaki)

Kwa miaka mitatu nilikaa mtaani na hapo ndipo niliishi falsafa hii ya kusema ndiyo kwa kila kitu. Katika miaka hiyo mitatu nilifanya kila kilichopita mbele yangu. Nilifundisha shule na vyuo, nilijifunza kutengeneza website na blogu, nilijifunza kutengeneza programu za komyuta, nilifanya biashara za mtandao, nilifanya kilimo, nilifanya biashara za fedha na nyingine nyingi.

Katika kipindi hicho sikusema hapana kwenye chochote kilichokuja mbele yangu, nilisafiri maeneo mbalimbali kila niliposikia kuna fursa fulani huko. Nakumbuka katika hicho kipindi tuliwahi kusafiri na rafiki yangu kwenda Mlimba kwa treni kwenda kuangalia fursa za kilimo cha mpunga na kununua mchele. Ni moja ya safari ambazo mpaka sasa naikumbuka kwa sababu ilikuwa na misukosuko mbalimbali.

Ni katika kipindi hicho pia ndiyo nilianzisha blogu ya AMKA MTANZANIA hatimaye KISIMA CHA MAARIFA na uandishi wa vitabu pia. Katika kipindi hicho pia nilisoma sana vitabu vya maendeleo binafsi.

Nakumbuka Januari mwaka 2012 baada ya kuona hakuna mwelekeo wowote wa kurudi chuoni kwa siku za karibuni, nilijiambia sasa napaswa kushika hatamu ya maisha yangu. Na hapo nilianza kwa kusoma kitabu cha RICH DAD, POOR DAD, kitabu hicho ni kama kiliifungua dunia kwangu. Baadaye nikasoma kitabu cha THINK AND GROW RICH, kisha THE RICHEST MAN IN BABYLON.

Nimekuwa nasema vitabu hivyo vitatu ndiyo msingi wa maisha yangu, ndiyo viliniwezesha kuiona dunia kwa mtazamo wa tofauti na hatimaye kunijenga nilivyo leo. Mpaka sasa nimesoma na kusikiliza vitabu zaidi ya elfu moja, lakini hivyo vitatu nimekuwa navirudia mara kwa mara na nimekuwa nashauri yeyote anayetaka kushika hatamu ya maisha yake basi aanze kwa kusoma vitabu hivyo.

Katika mengi niliyofanya katika hicho kipindi, kusoma, kuandika na kufundisha ni vitu vitatu ambavyo nimekuwa napenda sana kuvifanya na sichoki hata kidogo kuvifanya. Naweza kutumia mpaka masaa 10 kwa siku nikisoma au kuandika. Naweza kusoma kitabu na kumaliza ndani ya siku moja. Na pia naweza kuandika mpaka maneno elfu 10 kwa siku moja, kuandika maneno elfu 5 kwa siku ni kitu cha kawaida kwangu na wala sioni ni kazi nzito.

Hivyo fanya zoezi hili rafiki yangu, kama bado hujajua kusudi la maisha yako, chagua kipindi utakachorudi kwenye utoto wako na sema ndiyo kwa kila kitu. Kila kinachokuvutia kufanya, kifanye. Tenga muda ambao utafanya majaribio mbalimbali kwenye maisha yako na kujifunza kwenye kila unachofanya.

SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2020

KUISHI KUSUDI, SEMA HAPANA.

Baada ya kujua kusudi la maisha yako, sasa unahitaji kuweka umakini wako wote kwenye kuishi hilo. Hupaswi tena kuhangaika na mambo mengine nje ya kusudi hilo.

Muda na nguvu zako vina ukomo, usipoteze kuhangaika na mambo mengine. Kuna mazuri yatakayokuja kwako na yenye fursa ya kunufaika zaidi, lazima uweze kusema hapana kwa hayo mazuri ili uweze kupata yaliyo bora kupitia kuishi kusudi lako.

Ili kuishi kusudi lako, SEMA HAPANA kwa mambo mengine yote na baki kwenye kuishi kusudi lako tu.

Baada ya mimi kujua kusudi langu lipo kwenye kufundisha wengine kupitia uandishi na ukocha, nimekuwa nasema hapana kwa mengine yote isipokuwa kusudi hili.

Nilikuwa nawatengenezea watu blog na wananilipa vizuri, nilikuwa nawahifadhia (hosting) watu blogu zao mtandaoni na wananilipa, nilikuwa nashauri mtu mmoja na mengine mengi. Lakini yote hayo nimekuwa nayafuta ili nibaki kwenye lengo langu kuu.

Kila siku kuna watu wananitafuta wakitaka niwafanyie baadhi ya vitu nilivyokuwa nafanya awali na wanilipe, lakini kwa sababu sitaki kutoka kwenye kusudi nimekuwa nasema hapana na kuwapeleka kwa wanaoweza kuwasaidia katika maeneo hayo.

Najua kusema hapana kunanigharimu kwa kiasi kikubwa, lakini nikisema ndiyo itanigharimu zaidi baadaye. Juhudi ninazoweka kwenye kusudi langu kwa sasa ninajua zitazalisha matokeo makubwa sana baadaye kuliko nikihangaika na mambo mengine.

Ukishajua kusudi lako, yapangilie maisha yako kwa namna ambayo kuishi kusudi hilo ndiyo kipaumbele kikubwa kwako na sema hapana kwa mengine yote ambayo hayahusiani na kusudi hilo.

Ni kwa njia hiyo ndiyo unaweza kuweka umakini, muda na nguvu za kutosha kwenye kusudi lako na liweze kuleta matunda mazuri kwako.

NDOTO KUBWA YA MAISHA YAKO.

Maisha yasiyokuwa na ndoto ni maisha ambayo hayana msukumo wa kuyaishi.

Kama unataka kuacha alama hapa duniani, lazima uwe na ndoto kubwa, lazima uwe na picha ambayo hakuna anayeiona na hata ukiwaambia wengine hawaamini kama inawezekana.

Ukishakuwa na picha hiyo kubwa, unapaswa kuifanyia kazi kila siku mpaka utakapoifikia. Unapaswa kuwa tayari kutoa kafara ya kila aina kwenye maisha yako ili kufika kwenye ndoto yako kubwa.

Hii sitaielezea sana kwa sababu ni mchakato mkubwa na ndiyo kitu tunachofanyia kazi kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

WANACHAMA WA KISIMA CHA MAARIFA KWENYE SEMINA YA MWAKA 2020

KARIBU KWENYE KISIMA CHA MAARIFA.

Rafiki yangu mpendwa, kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, nichukue nafasi hii kukukaribisha sana kwenye jamii hiyo ya tofauti na ya kipekee.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA tunafanyia kazi mambo haya mawili niliyoshirikisha hapa, KUSUDI na NDOTO.

Kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA tutafanya kazi kwa karibu kabisa na utaweza kulijua KUSUDI LA MAISHA YAKO na kuliishi.

Pia utakuwa na ndoto yako kubwa, unayopambana kila siku ili kuifikia na nitakusimamia kwa karibu ili kufika kwenye ndoto hiyo.

KISIMA CHA MAARIFA ni sehemu pekee ambapo utapata msukumo mkubwa wa kuyabadili maisha yako na kuweza kufika kwenye mafanikio makubwa na kuacha alama hapa duniani.

Jiunge leo kwa kutuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap namba 0717 396253.

Nimalize kwa kukushukuru zaidi wewe rafiki yangu, uwepo wako umekuwa wajibu wa maisha yangu na karibu sana tuendelee kuwa pamoja kwenye safari hii ya mafanikio.

Kuendelea kusoma makala nzuri bure kabisa kila siku fungua; https://amkamtanzania.com

Kupata vitabu nilivyoandika fungua; https://amkamtanzania.com/vitabu/

Kupata chambuzi za vitabu na vitabu vizuri vya kusoma fungua; https://www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki yako anayekupenda sana,

Kocha Dr Makirita Amani.