Rafiki yangu mpendwa,
Ni kitu gani unachokitaka sana kwenye maisha yako lakini umekuwa hukipati?
Umepambana nacho sana lakini kila anayekuzunguka anakuambia huwezi kukipata!
Vipi leo nikikuambia unaweza kabisa kupata hicho unachokitaka sana?
Unaweza usimamini siyo? Endelea kusoma na ujionee mwenyewe jinsi hilo linawezekana.

Jim Kwik alikuwa mtoto wa kawaida kama walivyokuwa watoto wengine. Alisoma na kuelewa vizuri shuleni.
Lakini kwa bahati mbaya, siku moja alianguka na kuumia kichwa, kitu kilichopelekea apoteze fahamu kabisa.
Alipokuja kuzindika, maisha yake yakawa yamebadika kabisa.

Hakuweza kuwa tena na utulivu wa kujifuza kama watoto wengine.
Hakuweza kupata usingizi vizuri usiku.
Kwa kipibndi chote cha maisha yake ya shule, alikuwa anapambana tu asishindwe kabisa darasa.
Walimu wake walimbatiza kabisa jina la mtoto mjinga.

Jim alienda akiamini hivyo kwa kipindi kirefu cha maisha yake, mpaka alipokutana na mtu aliyemzindua na akaona hapaswi kuendelea alivyokuwa.
Baada ya Jim kuzinduliwa, na yeye akachukua jukumu la kuwazindua wengine ambao nao wamenasa kwenye imani kwamba hawawezi kupata wanachotaka.

Kupitia kitabu chake kinachoitwa LIMITLESS; Upgrade Your Brain, Learn Anything Faster And Unlock Your Exceptional Life, Jim Kwik anatupa maarifa na misingi ya kuweza kupata chochote tunachotaka kwenye maisha yetu.
Hapa tunakwenda kujifunza jinsi ya kuweza kupata chochote tunachotaka kutoka kwenye msingi ambao Jim aliugundua na kuweza kuutumia yeye na hata wengine pia.

Kinachokuzuia kupata unachotaka.

Kama hujapata kile unachotaka kwenye maisha yako, ni kwa sababu kuna ukomo ambao umejiwekea wewe mwenyewe.
Ukomo huo unaweza kuwa ulianzia kwa wengine ambao walikuwa wanakuambia huwezi au haiwezekani, na baadaye ukaja kuamini na sasa umekuwa sehemu ya maisha yako.

Maeneo matatu ya kuondoa ukomo.

Kama kuna chochote unachotaka kwenye maisha yako ila hujakipata, kuna maeneo matatu ambayo utakuwa umejiwekea ukomo.

Eneo la kwanza ni mtazamo ulionao, kwa wengi huwa wana mitazamo hasi na ya kushindwa, kitu kinachokuwa kikwazo kwao kuona uwezekano mkubwa na kuufanyia kazi.

Eneo la pili ni motisha, kama huna motisha sahihi, hutapata msukumo wa kuchukua hatua ili kupata kile unachotaka. Safari ya kupata unachotaka siyo rahisi, unahitaji motisha ili kuendelea na mapambano.

Eneo la tatu ni mchakato, namna unavyofanya mambo yako inaweza kuwa kikwazo kwako kupata unachotaka. Lazima uwe na mchakato sahihi utakaokuwezesha kupata kile unachotaka.

Ili kufanya na kufikia makubwa, lazima uondoe ukomo kwenye maeneo hayo matatu na hilo ndiyo tunakwenda kujifunza kwenye kitabu hiki.
Unaweza kufanya makubwa kuliko unavyodhani sasa, karibu ujifunze na uchukue hatua sahihi.

Soma; jinsi ya kujua kusudi la maisha yako.

Jinsi ya kuondoa ukomo na kupata unachotaka.

Uko hapo ulipo sasa kwa sababu ya ukomo ulioukubali kwenye maisha yako.
Jamii ilikuaminisha huwezi vitu fulani na ukakubaliana nayo na kile unachoamini ndiyo kinatengeneza aina ya maisha uliyonayo sasa.
Unaweza kupata matokeo ya tofauti na unavyopata sasa kama utaondoa kila aina ya ukomo ambao umejiwekea.

Kama tulivyojifunza hapo juu, ukomo uko wa aina tatu;
Mtazamo ambapo unakuwa hujiamini, hujui uwezo wako mkubwa na huoni kama makubwa yanawezekana.
Motisha ambapo unakosa kusudi, msukumo na nguvu za kuchukua hatua ili kupata makubwa.
Mchakato ambapo unashindwa kuchukua hatua sahihi ili kupata matokeo makubwa.

Kuondoa ukomo kwenye maeneo hayo matatu kutakuwezesha kufanya makubwa mno.
Kwa kuondoa ukomo kwenye mtazamo utajua nini hasa unachotaka, uwezo wa ndani yako wa kukipata na uwezekano wa kitu hicho kupatikana.
Kwa kuondoa ukomo kwenye motisha utajua kwa nini unataka kile unachotaka kwa kuwa na kusudi la maisha, kuwa na msukumo na nguvu ya kulifanyia kazi kusudi hilo.
Kwa kuondoa ukomo kwenye mchakato utazijua hatua sahihi za kuchukua na jinsi ya kuzichukua ili uweze kufanya makubwa.

Soma; jinsi ya kupata hamasa isiyopoa.

Unahitaji kuondoa ukomo kwenye yote matatu.

Ili usiwe na ukomo kabisa kwenye maisha yako, ili uweze kufanya makubwa, lazima uondoe ukomo kwenye maeneo yote matatu.
Ukiondoa ukomo kwenye mtazamo na motisha pekee, utakuwa na hamasa kubwa, ila bila mchakato hutafanya lolote.

Ukiondoa ukomo kwenye motisha na mchakato utakuwa na nguvu ya kutekeleza, ila mtazamo wako utakuzuia kufanya makubwa.

Ukiondoa ukomo kwenye mchakato na mtazamo utakuwa na mawazo mazuri sana, ila ukomo kwenye motisha utakuzuia usichukue hatua.

Kwa kuchanganya yote matatu, yaani mtazamo sahihi, motisha mkubwa na mchakato bora utaondoa kila ukomo kwenye maisha yako na kuweza kufanya makubwa sana.

Maadui Wanne Wanaokuweka Kwenye Ukomo.

Kitendo cha kuondoa ukomo kwenye maisha yako ni kitendo cha kishujaa. Kitendo chochote cha kishujaa huwa hakikosi maadui wanaokipinga na kukizuia.
Kadhalika kwenye kuondoa ukomo, wapo maadui wakubwa wanne wanaowafanya watu kuendelea kubaki kwenye ukomo.
Kwa kuwajua maadui hao wanne na kuweza kuwavuka, utaweza kuondoa ukomo na kuifungua akili yako kwa ajili ya kujifunza na kufanya makubwa.

Maadui hawa wanne wanatokana na teknolojia ambayo inakua kwa kasi na tunaitegemea na kuitumia kila siku ya maisha yetu.
Kwa kuwa ni kitu chenye manufaa pia, siyo rahisi kuwakabili maadui hao wanne.
Hapa tunakwenda kuwajua maadui hao na jinsi ya kuwakabili.

✔Moja; Mafuriko ya kidijitali (digital deluge).
Ukuaji wa teknolojia hasa kwenye upande wa simu janja na mitandao ya kijamii, umetuweka kwenye mafuriko ya taarifa mbalimbali.
Kwa siku moja tunapokea taarifa nyingi mno kuliko alizokuwa anapokea mtu kwa mwaka mzima kwenye karne ya 20.
Wingi wa maarifa na taarifa umekuwa kikwazo kwa wengi kujifunza yale muhimu na yanayoweza kuwa na manufaa kwao.
Taarifa nyingi siyo muhimu na hazina manufaa, ila zinasambazwa kwa kasi kwa sababu zinaibua hisia kwa watu.
Mafuriko hayo ya taarifa yamekuwa hayampi mtu nafasi ya kutafakari na kujifunza kwa kina ili kuelewa na kuchukua hatua sahihi.
Tenga muda ambao utakuwa mbali na vyanzo vya taarifa za kidigitali, pia chagua njia za uhakika utakazokuwa unatumia kujifunza yale muhimu na yenye tija kwako.
Mitandaoni kuna taarifa na maarifa mengi, ila kwa sehemu kubwa sana hayana manufaa yoyote kwako.
Chagua kwa umakini mkubwa na achana na yasiyo na tija.

Soma; Jinsi ya kuepuka utumwa wa kidijitali.

✔Mbili; Usumbufu wa kidijitali (digital distraction).
Kutokana na wingi wa taarifa na maarifa, watu wamekuwa wanayasukuma kwako kwa njia mbalimbali.
Lengo ni kukamata umakini wako ili wao wanufaike.
Hili limezalisha usumbufu mkubwa sana wa kidijitali ambapo inakuwa vigumu mtu kupata utulivu wa kuweka umakini kwenye yale muhimu.
Simu janja tunazotumia zina viashiria mbalimbali vya kutukumbusha kuingia mtandaoni na kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa kuwa akili yako imezungukwa na usumbufu muda wote, ni vigumu kufunguka na kufanya makubwa.
Hivyo unapaswa kuondoa usumbufu huo wa kidijitali, kupitia kutenga muda wa kuwa nje ya mitandao ya kijamii na hata simu yako kwa ujumla.
Pia kwenye simu yako, ondoa viashiria vyote vya usumbufu (notifications) ili uweze kupata utulivu na umakini kwenye yale muhimu unayofanya.

✔Tatu; Kusahau kidijitali (digital dementia).
Ni lini mara yako ya mwisho kukariri na kukumbuka namna ya simu ya mtu? Unajiambia hilo halina haja, unaweza kutunza namba za simu kwenye simu au mtandaoni kiasi kwamba huwezi kuzipoteza hata iweje.
Tunafurahia teknolojia hizi zinazotupunguzia mzigo wa mambo ya kukumbuka, lakini hili linakuja na madhara yake.
Ubongo wako ni kama misuli ya mwili, ukifanya mazoezi inakuwa imara ila usipofanya inakuwa dhaifu.
Unapoutumia ubongo kukariri na kukumbuka vitu unaufanya uwe imara, lakini usipoutumia unajikuta ukiwa msahaulifu.
Watu wengi kwa sasa ni wasahaulifu kwa sababu hawaupi ubongo wao zoezi la kujenga kumbukumbu.
Wengi huona kujilazimisha kukariri na kukumbuka vitu unavyoweza kutunza mtandaoni ni kujaza akili, lakini ukweli ni kwamba akili huwa haijai, kadiri unavyoitumia ndivyo inazidi kuwa imara.
Acha kutegemea teknolojia kwenye kutunza kumbukumbu zako, chagua baadhi ya vitu muhimu utakavyokariri na kukumbuka kila wakati.
Katika kukariri na kukumbuka unaifanya akili hako kuwa imara na bora zaidi.
Anza kwa kukariri na kukumbuka namba za simu za watu wako wa karibu.

✔Nne; Maamuzi ya kidijitali (digital deduction).
Akili yako inakuwa imara pale unapopata taarifa, unafikiria kwa akili yako na kufanya maamuzi yako mwenyewe.
Lakini hivyo sivyo hali ilivyo sasa, watu hawafanyi tena maamuzi wenyewe,  badala yake wanaingia mitandaoni na kuangalia wengine wana maoni gani kisha kuyachukua hayo kama ndiyo maoni yao.
Kwa sasa watu hawajengi tena maoni yao na kufikia maamuzi yao, badala yake wanachukua maoni ya wengine au kuiga maamuzi ya wengine.
Watu hawawezi tena kufanya maamuzi kabla hawajaingia mtandaoni na kuangalia wengine wanafanyaje.
Hakuna kitu kinaharibu akili za watu kama hili la kubeba maoni na maamuzi ya wengine. Kwani kadiri mtu anavyofanya hivyo kwa muda  mrefu, ndivyo anavyokosa kujiamini na kujikuta anategemea kila kitu kutoka kwa wengine.
Anza kufanya maamuzi yako mwenyewe. Unaweza kukusanya taarifa uwezavyo, unaweza kupitia maoni ya wengine, ila mwisho wa siku, unapaswa kukaa kwenye eneo tulivu na lisilo na usumbufu ili ufanye maamuzi yako mwenyewe.
Anza kufanyia kazi hili mara moja, fikiria na ufanye maamuzi yako mwenyewe, yanayoendana na wewe.

Maadui hawa wanne wana mbinu kubwa za kutuhadaa na kutuweka kwenye ukomo. Lazima na sisi tuwe na uwezo mkubwa wa kuwakabili, kwa sababu hatuwezi kuachana nao moja kwa moja, tunazihitaji teknolojia hizi kwenye maisha yetu ya kila siku.
Muhimu ni sisi tuzitumie teknolojia na siyo teknolojia zitutumie sisi.

Huu ni utangulizi tu wa mengi utakayojifunza kwenye uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha LIMITLESS.
Utajifunza jinsi ya kujenga mtazamo sahihi utakaokuwezesha kuvunja kila aina ya ukomo na kuona uwezekano wa makubwa.
Utajifunza jinsi ya kujenga motisha sahihi utakaokusukuma kuchukua hatua kubwa na kupata unachotaka.
Na pia utajifunza jinsi ya kuwa na mchakato sahihi unaoufuata ili kuzalisha matokeo sahihi kwenye kile unachotaka.

Karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu cha LIMITLESS ambao unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA.
Kujiunga na channel hii, fungua; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza Join Channel.

Usikubali kuendelea kujiwekea ukomo unaokukosesha yale unayotaka kwenye maisha yako.
Soma leo uchambuzi wa kitabu cha LIMITLESS ili uvunje kila aina ya ukomo na uwe huru kupata chochote unachotaka.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.