Rafiki yangu mpendwa,
Vipi kama leo nikikuambia kuna neno moja ambalo ukiweza kulitumia vizuri litakupa muda zaidi, utulivu na mafanikio makubwa?

Na vipi kama nitakuambia neno hilo unaweza kuanza kulitumia hapo ulipo sasa na kuanza kuyaona matunda yake mazuri?

Rafiki, majibu ni ndiyo, hilo neno lipo na leo utakijua na jinsi ya kulitumia ili upate matunda mazuri.

Rasilimali muhimu zina ukomo.

Muda ni rasilimali muhimu sana kwako, lakini una ukomo, una masaa 24 tu kwa siku, huwezi kuongeza haya sekunde moja.
Kutumia muda wako kwenye jambo moja ni kushindwa kuutumia kwenye jambo jingine.

Fedha ni rasilimali muhimu, lakini wakati unaanza safari zinakuwa na ukomo. Kutumia fedha kwenye jambo moja ni kushindwa kuzitumia kwenye jambo jingine.

Nguvu za mwili wakk zina ukomo, unachoka kwa kufanya mambo mbalimbali. Unapofanya jambo moja ukachoka, unashindwa kufanya jingine.

Umakini wako una ukomo, huwezi kufuatilia vitu viwili kwa wakati mmoja kwa umakini mkubwa, lazima uache vingine vyote na kuweka umakini wako wote kwenye kitu kimoja.

Kama tunavyoona hapa, rasilimali hizo muhimu sana zina ukomo.
Swali ni je unawezaje kuzidhibiti na kuzitumia vizuri ili kufanya makubwa kwenye maisha yako?

Hapo ndipo unapokuja umuhimu wa neno tunalokwenda kujifunza hapa. Neno litakalokupa muda zaidi, utulivu mkubwa, umakini na mafanikio makubwa.

Neno hilo ni HAPANA.

Hapana ni neno rahisi lakini lenye miujiza mikubwa kwenye maisha ya kila mtu.

Ukiyachunguza maisha yako, utagundua kila wakati umeingia kwenye matatizo ulishindwa kutumia neno hapana.

Ulikuwa na fedha kidogo lakini ukashindwa kusema hapana, kilichotokea ni kutumia zote na kuingia kwenye madeni.

Unajua una uhaba wa muda lakini haupo tayari kusema hapana kwa mengi yanayokuja kwako, kinachotokea ni kuwa na mengi ya kufanya huku muda hautoshi, unazalisha msongo.

Naweza kusema hakuna tatizo au changamoto umewahi kuingia ambayo isingeweza kuzuilika kwa kutumia neno hapana.

Wakati wa kutumia neno HAPANA.

Unaweza kujua umuhimu wa neno hapana, lakini unajua wakati sahihi wa kulitumia.

Mwandishi Seth Godin amewahi kushirikisha vigezo muhimu vya kutumia kusema hapana.
Na hapa tunakwenda kuvipitia kwa ufupi, ili na wewe utengeneze vya kwako vitakavyokusaidia.

1. Kama huwezi kujivunia kwa kile utakachofanya, usikifanye.

2. Kama huwezi kufanya kazi iliyo bora kabisa usiikubali.

3. Kama itakuwa usumbufu kwako kufanya yale yaliyo muhimu zaidi acha ikupite.

4. Kama hujui kwa nini watu wanataka ufanye wanachokuambia ufanye, uliza.

5. Kama inabidi ufiche mama yako asijue, fikiria mara mbili.

6. Kama kitakunufaisha wewe pekee na kisiwanufaishe wale unaowajali, kataa.

7. Kama unafuata mkumbo, shtuka.

8. Kama itakujengea tabia ambayo itakuja kukugharimu baadaye, usianze.

9. Kama hakikusukumi kwenda mbele zaidi, sita kisha achana nacho.

Unapochagua kusema NDIYO, sema ndiyo ya kweli na fanya kitu bora na chenye manufaa makubwa.

Siyo rahisi kutumia neno HAPANA.

Tumeona jinsi neno HAPANA lilivyo muhimu na lenye manufaa.
Lakini kwa bahati mbaya sana, siyo neno rahisi kutumia.

HAPANA siyo rahisi kusema kwa sababu kubwa mbili.

Moja ni kuona kama mtu unakosa fursa nzuri. Unaona ukisema hapana unapoteza fursa ambayo ingeweza kukunufaisha.
Lakini hupaswi kutegwa na hili, jua kila mahali kuna fursa na chagua mambo unayosema ndiyo na tumia fursa zilizo ndani ya mambo hayo.

Mbili ni kutokutaka kuwaumiza wengine. Kwa kuwajibu watu hapana wanajisikia vibaya na kuona hatujali. Hivyo kukwepa kuwaumiza unawajibu ndiyo, japo ndani yako unajua kabisa hutaki.
Kinachotokea ni unaishia kujiumiza wewe mwenyewe na hata wao pia, maana hufanyi kilicho bora.

Siyo lazima useme hapana kikatili na kuwaumiza wengine.
Waeleze kwa nia njema kabisa hutaweza kufanya wanachotaka na washauri namna bora kwao kupata wanachotaka.

Kuna watakaokuelewa na kuna ambao hawatakuelewa. Muhimu ni wewe umetumia hapana kulinda rasilimali muhimu kwako.

Pia siyo muhimu kutoa sababu ya HAPANA yako, hapana ni neno ambalo ni sentensi iliyokamilika.
Huna haja ya kusema HAPANA kwa sababu …
Wewe sema tu hapana na inatosha kabisa.

Hatua za kuchukua.

Umeona jinsi neno HAPANA lilivyo na nguvu kubwa kwenye mafanikio yako.
Jiwekee sheria zako za wakati gani wa kusema NDIYO na wakati gani wa kusema HAPANA.

Anza na kusudi la maisha yako na ndoto zako kubwa. Hayo ndiyo maeneo mawili makubwa ya kusema NDIYO.
Mengine yote jibu lako linapaswa kuwa HAPANA.

Kila unapokutana na fursa mpya au watu wanapokuja na mapendekezo kwako, jiulize namna gani yanachochea au kuathiri maeneo hayo mawili kwako.
Sema Ndiyo kama yanachochewa na hapana kama tanaathiriwa.

Jifunze kusema hapana yenye tija kwako na kwa wengine pia.
Matakwa yako ya haraka yasiwe kikwazo kwa malengo yako ya muda mrefu.

Sema hapana ili uzitumie vizuri rasilimali zako kwa yale muhimu na yanayokufikisha mbali zaidi.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz

0752 977 170 kupata vitabu.