Neno bure ni njia rahisi ya kuwapata watu kulipa gharama kubwa. Ni neno ambalo linaweza kuwashawishi watu kuchukua hatua ambazo siyo bora kwao. Kwa sababu watu wengi wanapenda njia rahisi.

Kitu chochote unachoambiwa unapewa bure, chunguza kwa makini, kuna gharama kubwa utakazoingia kwa kukubaliana na kitu hiko. Huenda ikawa ubora unaopata ni hafifu sana na hivyo baadaye kuingia gharama kubwa. Au huenda bure ni hatua ya kwanza na ili kuendelea hatua nyingine unahitaji kuingia gharama. Pia inawezekana utapoteza muda mwingi kwenye bure hiyo ambao ungeweza kuutumia kufanya mambo mengine muhimu kwako.

Jua kwenye kila bure kuna gharama ambazo zimejificha ndani yake, na angalia kama upo tayari kulipa gharama hizo kabla hujaingia kwenye bure hiyo. Kama kitu ni muhimu kwako, kinaongeza thamani kwenye maisha yako, basi kina gharama zake. Kuwa tayari kulipa gharama hizi ili kupata kile unachotaka. Usikimbilie vinavyosemwa ni bure, utaumia zaidi kwa kupoteza fedha, muda na hata utu wako.

Hakuna kitu cha bure kwenye dunia hii ambacho kina thamani kwako. Jiandae kulipa gharama na lipa mwanzoni kabisa ili uweze kuwa na uhuru wa kufika kule unakotaka kufika.

SOMA; UKURASA WA 43; Ushauri Wa Bure Una Gharama Kubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba bure ni neno linalotumika kuwalaghai watu ili watoe gharama kubwa zaidi. Kuanzia sasa nitakuwa makini na kitu chochote kinachosemwa ni bure, nijue ni gharama gani hasa ninayoingia katika bure hiyo. Kitu chochote muhimu kwangu kina gharama zake, na mimi nimechagua kulipa gharama hizi.

NENO LA LEO.

Neno bure ni njia rahisi ya kuwafanya watu waingie kwenye gharama kubwa bila ya wao wenyewe kujua. Hakuna kitu cha bure ambacho ni cha thamani, kuna jinsi unavyolipa zaidi iwe ni kwa fedha, muda au hata utu wako.

Usikimbilie vinavyosemwa ni bure, chunguza kwa makini na utaona kuna gharama kubwa unayolipa kwenye kila kinachosemwa ni bure. Jiandae kulipa gharama ili kufikia mafanikio, na epuka vitu vinavyoitwa ni vya bure.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.