Jambo moja ambalo unaweza usifurahi sana kulisikia ni kwamba kila mtu anataka wewe ushindwe. Ndiyo kila mtu, hasa wale wa karibu zaidi kwako, ndiyo wanataka ushindwe zaidi. Pale unapochagua kufanya mambo makubwa, ambayo wengine hawayafanyi, kila mtu atataka wewe ushindwe.
Hii ni kwa sababu kama ukiweza kufanikiwa kufanya, wao watajisikia vibaya kwamba kwa nini nao hawawezi kufanya. Kufanikiwa kwako kwenye hayo makubwa unayofanya kutawafanya wao waonekane ni wazembe na hawajui wanachofanya kwenye maisha yao.
Hivyo watazuia wewe usiweze kufanya hayo makubwa, na watakuambia unachotaka hakiwezekani, unapoteza muda wako. Wakati mwingine wanaweza wasikuambie moja kwa moja, usoni watakuambia unaweza, wewe fanya tu, lakini moyoni wanajua hutaweza na wanataka sana ushindwe ili ujue ya kwamba siyo rahisi ndiyo maana wao hawajaweza.
Kwa mfano ukiwaambia watu sasa hivi kwamba unataka kuandika kitabu, hata kama watakuambia andika moyoni watakuwa wanajisemea hawezi kuandika kitabu cha maana. Ukikazana na kumaliza kukiandika watasema hatapata mtu wa kukubali kukichapisha. Kama kitachapishwa watasema hakitanunuliwa na wengi. Na kama kikinunuliwa watasema ni bahati tu.
Inawaumiza watu sana pale ambapo wewe unaweza kufanya vitu ambavyo wao hawajaweza kufanya. Na iko hivi kwa asili yetu binadamu, hata kamani ndugu wa karibu au hata wazazi. Kuna hisia fulani za kutaka mtu ashindwe ili aelewe kwamba mambo siyo rahisi.
Nakuambia haya siyo kwa ajili ya kugombana na watu wako wa karibu au kuwakimbia, bali kuwaelewa na kujua ya kwamba safari ya mafanikio siyo safari rahisi. Imewashinda wengi hivyo unahitaji kuwa na kitu cha ziada kuweza kushinda. Na unahitaji kuanza kuvuka vizuizi hivi vya watu wanaokuzunguka.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kila mtu anataka mimi nishindwe. Pale ninapochagua kufanya mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanywa na wengine, wanataka nishindwe ili wao wasijisikie vibaya kwa nini hawakuweza kufanya muda wote. Ninawaelewa watu hawa lakini sitakubali wanirudishe nyuma, mimi nimeshaamua kufanikiwa, hakuna cha kunizuia.
NENO LA LEO.
Kila mtu anataka wewe ushindwe, hata wale wa karibu yako kama ndugu na marafiki.
Unapochagua kufanya mambo makubwa, ambayo wengine hawajaweza kufanya, inawaumiza kama utafanikiwa kwa sababu itawafanya wao kuonekana ni wazembe.
Wanataka ushindwe ili ujue ni vigumu ndiyo maana wao hawakuweza kufanya. Waelewe na achana nao, wewe weka juhudi na utafanikiwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.