Kipimo halisi cha kujifunza ni kubadili tabia.

Haijalishi unajua kiasi gani, kama tabia yako haiendani na kile unachojua, basi unachojua hakina msaada wowote kwako.

Na hiki ndiyo kipimo cha hekima, hekima haitokani na kujua bali kufanyia kazi kile ambacho unakijua.

Kwa mfano mtu ambaye ni daktari wa binadamu, anajua kabisa ya kwamba kuvuta sigara kuna hatari nyingi mno za kiafya. Lakini unamkuta mtu huyu anavuta sigara. Hapo anachokosa ni hekima, maarifa anayo, bila ya shaka lakini hajaweza kuyatumia.

Usiwe mtu wa kukusanya maarifa na kuendelea kuishi kwa mazoea, badala yake kuwa mtu wa hekima kwa kutumia kila maarifa kuboresha maisha yako zaidi.

Kwenye kila kitu ambacho unajifunza, jiulize unawezaje kukitumia kwenye maisha yako ili yawe bora zaidi? Hata kama ni kitu kidogo sana ukiweza kukitumia maisha yako hayawezi kubaki kama yalivyo.

Kujifunza pekee haitoshi, tumia ulichojifunza kubadili tabia zako na uwe bora zaidi.

SOMA; Ndio, hakuna jipya, lakini bado unahitaji kujifunza “KILA SIKU”.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba sijajifunza kitu mpaka pale ambapo naweza kutumia kile ambacho nimejifunza kubadili tabia zangu. Nitatumia kila ninachojifunza kuhakikisha kuboresha maisha yangu zaidi ili niweze kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio.

NENO LA LEO.

Hujajifunza kitu kama hujabadili tabia yako.

Maarifa yoyote unayopata yanahitaji kupelekea wewe ubadili tabia zako ili uwe bora zaidi.

Tumia kila unachojifunza kubadili tabia zako na siyo kwa ajili ya kujua pekee.

Hakuna maana ya kujua vitu kama huwezi kuvitumia kubadili tabia zako na kuwa na maisha bora zaidi.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.