Njia Tatu Za Kuongeza Ufanisi Wako Eneo La Kazi Na Kuepuka Kupoteza Muda Kwa Hadithi Zisizo Na Msaada Kwako.

Habari ndugu msomaji. Ni imani yangu kuwa unaendelea kujifunza na kufanya mabadiliko katika maisha yako ya kila siku kila kunapokucha. Leo ningependa tuangalie maeneo yetu ya kazi au ofisini kwetu. Mara nyingi watu wamekuwa wakishindwa kabisa kufanya kazi wakiwa ofisini kutokana na changamoto ya hadithi nyingi pindi wanapokuwa katika maeneo ya kazi lakini pia hadithi hizi haziishii hapo ofisini tu. Ukifika nyumbani unakuta kuna mwenza, ndugu au marafiki ambao kwa namna moja au nyingine wanakufanya usitimize/ usikamilishe majukumu yako uliyojipangia.

KUNA WAKATI UNAHITAJI KUJICHIMBIA ILI UFANYE KAZI BORA

 
Unaweza ukawa unatamani sana uwabadilishe kwa kuwashawishi wasome baadhi ya makala au vitabu au waangalie video za uhamasishaji ili na wao waone umuhimu wa kuzingatia ratiba zao na muda wao na kwa kufanya hivyo itakupa wewe urahisi wa kufanya shughuli zako, lakini inawezekana kila ukijaribu kufanya hivyo wao hawaungani na wewe. Hivyo bila kupenda na huku ukiwa na maumivu ya kutotimiza mipango yako, siku zinakwenda na hakuna kinachobadilika.
Napenda tuangalie baadhi ya vitu vinavyoweza kukusaidia kubadilisha hali hii katika eneo ulilopo. Lakini kabla hatujaangalia ningependa kukukumbusha kuwa sio rahisi kumbadili mtu mwingine kama yeye hajakusudia kufanya hivyo, lakini unaweza kubadilika wewe mwenyewe bila kujali msukumo wowote uliopo kutoka nje. Kubadilika kwako kunaweza kuwa chachu ya mabadiliko ya watu wanaokuzunguka mara tu baada ya kuona matokeo ya kile unachokizungumzia.
SOMA; Sehemu Kubwa Ya Watanzania Hatufanyi Kazi, Na Hili Ni Tatizo Kubwa Kwa Maendeleo.
Napenda kukutia moyo kama kuna mtu anaona kutimiza majukumu yako ni kama kichekesho kwake, na kuona kuwa “umepania maisha”, usijali wala usikasirike, kama unafahamu kwa nini unafanya kazi kutokana na mipangilio yako na unajua matokeo yake yatakufanya ujisikie vizuri kuliko kuwafurahisha wengine kwa kuungana nao katika ratiba zao ambazo baada ya siku kuisha unajuta kwa kuona umeipoteza siku yako bure na kiukweli utakua umeipoteza siku yako bure ambayo kamwe hautaweza kuirudisha tena. Fanya yafuatayo ili kubadilisha hali hii
1. Usiwe Shabiki wa Hadithi Unapokuwa Mahala pa Kazi.
Jitahidi sana unapokuwa mahala pa kazi usiwe shabiki wa hadithi zinazoletwa katika eneo hilo. Mara nyingi hadithi hizi huanza asubuhi tu , au mara tu mnapoingia ofisini kwakua ndio muda ambao kwa siku hiyo mnaonana na kila mmoja alikutana na mambo mbalimbali tangu siku/ muda mlipoachana. Kila mmoja atakua na taarifa zake labda juu ya siasa, urembo, mpira, majirani nk. Ukishabikia tu hadithi hizo, unajikuta ile ari ya kufanya kazi imeondoka, muda wa chai umefika, mara chakula cha mchana. Na muda wa kutoka haukawii. Na hapo ndio huwa mwisho wa siku na unaona kabisa kuwa hukuitendea haki siku hiyo nzima. Sio lazima ufahamu kila taarifa. Labda kama taarifa hiyo ni ya maana, sio kila taarifa tu lazima uwe nayo. Mfano jirani wa mfanyakazi mwenzio amehama na akaiba vitasa vya nyumba aliyohama, yaani hii inaweza kuwa habari ya hata saa moja na haikusaidii kitu wewe wala huyo unayeongea naye zaidi ya kupoteza muda wenu.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
2. Weka Ratiba ya Muda wa Kazi na Muda wa Kubadilishana Mawazo na Wengine.
Itakusaidia sana kama utakuwa na ratiba ya siku yenye mchanganuo wa muda, panga ratiba hiyo usiku na ipe muda ili kesho yake usiende nje ya ratiba kama hakutakuwa na dharura ambayo inaweza kuharibu/kubadili ratiba yako hiyo. Unapopanga muda wako wa kazi hakikisha umeweka na muda wa kubadilishana mawazo na wenzako kwakua kuna baadhi ya taarifa ambazo unazihitaji pia kutoka kwao lakini sio kupoteza muda. Unaweza kutenga muda wa chai au muda wa chakula cha mchana kuwa ndiyo muda wa kuongea na wengine, au hata baada ya chakula cha mchana wakati akili inakua imechoka na hauwezi kufanya kazi ya kutumia akili nyingi sana. Hii haimaanishi uongee hadithi yoyote ile, kwakua kwa kufanya hivi baada ya kuachana na rafiki zako akili ina tabia ya kurudia yale mliyoyaongea na unaweza kujikuta ukitafakari vitu ambavyo havikujengi. Jitahidi kujihusisha na habari ambazo zitakufanya uwe bora zaidi katika maisha yako.
3. Tumia Mbinu Hizi:
Kuna baadhi ya njia mbadala unaweza kuzitumia kama ikiwezekana. Unaweza kuweka “head phone” ili watu wajue kuna kitu unasikiliza hivyo hawawezi kukuambia kitu kwakua watajua hauwasikii. Kumbuka kuwa hii itatokana na namna mahala pako pa kazi palivyo na kama unaona kufanya hivyo hakuwezi kukuletea shida.
Kitu kingine unachoweza kufanya ni kuhamia kwenye ofisi ya watu wengine ambayo ina utulivu na uwaage wenzako kuwa upo huko kama watakuhitaji. Baada ya muda rudi ofisini ili wajue kwamba upo. Wakikuuliza kwa nini umeenda kukaa ofisi nyingine waambie kuna kazi ya haraka unahitaji uimalize na ungependa kukaa huko ili uikamilishe kwa haraka.
SOMA; Mabadiliko; Yalikuwepo, Yapo Na Yataendelea Kuwepo.
Basi hizo ni baadhi ya njia zinazoweza kukusaidia kuokoa muda wako mwingi unaopotea kutokana na hadithi nyingi za kila siku. Naomba nikuhakikishie kuwa, kama utazingatia muda utakuwa msaada sana kwa wale unaofanya nao kazi kwani baada ya muda lazima na wao watabadili tabia zao. Hata kama wanakucheka lakini ndani yao watakuwa wakiheshimu sana tabia yako ya kutunza muda , kuna wengine watakuja kuomba ushauri na wengine wataanza kubadilika kidogo kidogo. Unachotakiwa ni wewe kuanzisha tabia hii nzuri na kuidumisha bila kujali wengine wanasema nini.
Mawasiliano: 0767 900 110 / 0714 900 110
Whatsaap: 0652 025244
Face book: ESTHER ESTHER
Blog: www.boreshamaisha.blogspot.com
estherngulwa87@gmail.com

One thought on “Njia Tatu Za Kuongeza Ufanisi Wako Eneo La Kazi Na Kuepuka Kupoteza Muda Kwa Hadithi Zisizo Na Msaada Kwako.

Add yours

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: