Kabla Hujachukua Mkopo, Jiulize Kuna Ulazima Sana Kwako Wa Kufanya Hivyo?

Ni muhimu sana sisi kujiuliza maswali kadhaa kabla ya kuamua kununua au kukopa, iwe ni fedha au kitu chochote kile. Tunapaswa kujiuliza kwamba, je, fedha tunazotaka kukopa kweli tunazihitaji? Au je, kitu hiki tunachokinunua kweli tunakihitaji kwa wakati huo?
Baada ya kujiuliza maswali hayo muhimu, ni vizuri sana kuendelea kujiuliza swali lingine ya kwamba, iwapo kweli tunazihitaji hizo fedha au kitu kingine chochote, je, tunazihitaji hizo fedha au kitu kingine chochote, je, tunazihitaji kwa ajili ya matumizi muhimu na ya lazima kwa wakati huu?
Bila kujiuliza maswali haya kwanza, kabla hatujajiingiza kwenye manunuzi au mikopo, kwa kweli itakuwa ni sawa na kuendesha mashua baharini wakati wa usiku wenye giza nene na upepo mkali, huku tukiwa hatujui tuendako wala tutokako.
Ni hivi karibuni ambapo jamaa yangu mmoja aliweza kumchinja ng’ombe wake kwa ajili ya kumuuza na kujipatia fedha. Wateja wake wakubwa walikuwa ni majirani zake pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa maofisini. Lakini kama ilivyo kawaida kwenye biashara, wakopaji huwa hawakosekani. Kwani walijitokeza baadhi ya wateja waliomsihi jirani huyo awakopeshe japo tu kilo chache za nyama hiyo.
Uzuri ni kwamba, wateja wote waliomba kukopeshwa walikuwa ni wafanyakazi wa ofisini hivyo kwake kilikuwa ni kitu ambacho hakimpi wasiwasi kabisa. Wengi wao walitoa ahadi za kulipa madeni yao mara ifikapo mwisho wa mwezi, mara baada ya kupokea mishahara yao. Kwa vile jirani yangu huyo alikuwa akiwafahamu vyema watu hao, hakusita hata kidogo kuwakopesha nyama hiyo.

Basi ilipotimia muda huo jirani yangu kwa furaha alianza kufutilia madeni yake hayo akiamini kwa vyovyote vile ni lazima atalipwa. Lakini jambo la ajabu na la kusikitisha ni kwamba, jirani yangu huyo hakupata pesa zake kama alivyotarajia.
Kisa? Taarifa alizozipata ni kwamba wafanyakazi wale hawapokei mishahara kamili, kwa sababu mishahara yao, karibu yote hukatwa hukohuko makao makuu kwa ajili ya kulipia madeni ya mikopo waliyokopa kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha. Ilielezwa kwamba walikuwa wamekopa vitu vingi kama majokofu, redio,televisheni na wengine hata samani za ndani na vingine.
Hali hiyo ilimkasirisha sana jirani yangu huyo kwani alihisi tayari alikuwa ameshatapeliwa kwa kuwa walijua fika kwamba kulipa kwao itakuwa ni kwa tabu sasa kwanini walikopa? Alipoendelea kufuatilia alipewa ahadi tena mwezi ujao, mwisho aliamua kuachana nayo kama wakimpa hiyo pesa sawa, wasipompa pia ni sawa kwani alikuwa ameamua kusamehe.
Bila shaka hali kama hii imekuwa ni jambo la kawaida katika jamii yetu, kwani watu wengi hivi sasa ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa maofisini na wengine, wamekuwa wakiingiliwa na tamaa kubwa ya kutaka kukopakopa kila kitu wanachokiona kwa macho kuwa ni kizuri kwao. Ilimradi tu wamehakikishiwa mahali fulani kunatolewa mkopo na ulipaji wake ni rahisi.
Watu hawa bila kufahamu kwamba, wamekuwa wakijitwisha na kujibebesha mizigo isiyo ya lazima, wamekuwa wakikumbana na adha, mihangaiko, kufuatwa fuatwa, kudaiwa daiwa, kukimbia kimbia, kujificha kwa hofu ya kudaiwa na kuadhiriwa na mengine. Bila shaka umewahi kusikia hata redioni juu ya watu walioamua kujiua wakiacha ujumbe kwamba, wameamua kufanya hivyo kutokana na mizigo ya madeni.
Watu hao wamekosa utashi na nguvu za kuweza kuzuia nguvu za ushawishi zinalopelekwa kwao kupitia tamaa zao binafsi au kwa kupitia kwa maofisa na watumishi mbalimbali wa vyombo hivyo vyenye mamlaka na uwezo wa kuwakopesha.
Jambo moja ambalo watu hawataki kulitambua na kulikubali ni kwamba mikopo inapaswa kutafutwa pale tu tunapohitaji kuitumia kwa matumizi maalumu na muhimu na si katika kila kitu tunachohisi tunakitamani na ndiyo maana kabla hujachukua mkopo, jiulize ni lazima sana kwako kufanya hivyo?
Mikopo ni nyenzo muhimu sana katika  kuanzisha, kukuza, kuendeleza na kustawisha miradi mbalimbali ya kiuchumi na ya kimaendeleo. Lakini, pamoja na umuhimu huo, ni vizuri kwa watu kuitambua nguvu yenye mvuto na ushawishi mkubwa iliyomo ndani ya mikopo. Nguvu hii hufanya kazi kupitia mambo makuu yafuatayo;-
Kwa kujenga taswira au picha ndani ya akili ya mkopaji, ihusuyo vitu au mambo mbalimbali atakayoweza kuyapata kwa kutumia mkopo huo. Kwa kuibua nguvu ya ushindani itokanayo na ubinafsi na choyo iliyomo ndani ya binadamu.
Kwa kumhakikishia mkopaji kwamba hana haja ya kuwa na wasiwasi na hofu yoyote ile, kwani atamudu kuurejesha mkopo huo na kwa wakati huohuo kufanikisha mambo yake yote.
Jambo la maana ni kuona kwamba, ili mtu aweze kujiingiza ndani ya mkopo anapaswa kuvaa silaha kamili ambazo kushirikiana pamoja na mambo mengine ya ufahamu kamili, utambuzi makini na uwezo timilifu wa kuweza kurejesha mikopo hiyo.
Ikumbukwe kwamba, suala la mikopo linabaki kuwa ni hiari ya mtu. Hivyo, ni bora kuwa na hiari kutafuta na kukopa mikopo kwa mambo muhimu  na yanayojenga kuliko kuwa na hiari ya kukopa kwa ajili ya mambo ya hovyohovyo, kwani wakati umefika sasa wa watu kubadilika.
Ni fedheha na aibu kwa mtu kuweza kudaiwa daiwa tena madeni madogo na kukufanya ukimbie kimbie bila uhuru. Ni muhimu kwetu kubadilika ili tuweze kuepukana na hata kuondokana na ulevi au utumwa huu wa mikopo. Narudia kusema, kopa kama una la maana la kufanyia mikopo hiyo, usikope kwa sababu wengine wanakopa.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, endelea kutembelea AMKA MTANZANIAkwa kujifunza kila siku.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: