Maisha bora, yenye furaha na mafanikio yanaanza na pale mtu anapokuwa huru kwenye maisha. Ndiyo maana kuna watu wengi ambao kwa nje wanaweza kuonekana wamefanikiwa lakini ndani yao wanaona maisha yao bado hayapo kama ambavyo walitaka yawe. Uhuru wa maisha ndiyo unaoleta kila kitu kwenye maisha, lakini pia uhuru huu ni mgumu sana kupatikana kutokana na changamoto ambazo tutazijadili leo kwenye makala yetu hii ya FALSAFA MPYA YA MAISHA.
Ni matumaini yangu kwamba uko vizuri mwanafalsafa mwenzangu, ukiendelea kujijengea falsafa ya maisha yako ambayo itakusaidia kwenye kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako. maisha bila ya falsafa ni maisha ambayo hayawezi kuwa na mchango mkubwa kwa wengine, yanakuwa ni maisha ya kupita tu, kusukuma siku ziende. Lakini maisha yanayoendeshwa kwa falsafa yanakuwa na mchango kwa wengine, na kunakuwa na dhumuni la maisha hayo.
Changamoto za kuondoka kwenye vifungo vya maisha na kupata uhuru wa maisha.
Kuna changamoto kubwa tatu ambazo zimekuwa zinawazuia watu kuweza kuondoka kwenye vifungo vya maisha na kuweza kupata uhuru kamili wa maisha yao.
Changamoto ya kwanza; wewe binafsi.
Kama kuna kitu kikubwa ambacho kinakuzuia wewe kuwa huru basi ni wewe mwenyewe. Na hii imekuwa ndiyo changamoto ngumu kuliko zote kuivuka kutokana na jinsi ambavyo imeshazama ndani yako na pia ni ngumu kuijua na kuifanyia kazi.
Kuna njia mbalimbali ambazo tunazitumia sisi wenyewe kujiweka kwenye vifungo ambavyo vinatunyima uhuru.
Kuwategemea wengine kama chanzo cha furaha yako ni moja ya njia ambazo watu wamekuwa wakijiweka kwenye vifungo na kukosa uhuru. Pale ambapo unaona wengine ndiyo wanaoweza kukupa wewe furaha, unawategemea moja kwa moja. Kwa utegemezi huu unakosa kabisa furaha na hata uhuru wako.
Kutaka kumfurahisha kila mtu ni njia nyingine ambayo watu wamekuwa wanaitumia kupoteza uhuru wao. Ni vigumu sana kuweza kumfurahisha kila mtu na kujaribu kufanya hivyo inapelekea mtu kufanya vitu ambavyo hapendi kufanya na wala havina mchango wowote kwenye maisha yake. Pale mtu anapojaribu kumridhisha kila mtu anajikuta akishindwa kufanya yale mambo ambayo ni muhimu kwake hasa pale wale anaotaka kuwaridhisha hawaendani na mambo hayo.
Njia ya kuondokana na changamoto hizi;
Jua kabisa ya kwamba furaha ya maisha yako haitoki kwa wengine, bali inaanza na wewe mwenyewe. Furaha inaanza na wewe pale ambapo unayakubali maisha yako na kuona yana maana kwako na kwa wengine. Furaha haianzii nje yako bali ndani yako.
Jua ya kwamba huwezi kumfurahisha kila mtu, utakapochagua kuishi yale maisha ambayo ni muhimu kwako, kuna watu ambao utawaudhi, hata kama maisha yako hayawaathiri moja kwa moja. Kuna watu watakosoa kila unachofanya na kuonesha ni kwa namna gani unakosea. Kama unajua kile unachotaka kwenye maisha yako, na hujavunja sheria zozote, achana na watu hao na songa mbele. Wale ambao ni muhimu na wanakuelewa watakuwa pamoja na wewe.
Changamoto ya pili; Jamii.
Jamii zimekuwa kikwazo kikubwa sana kwa watu kuwa na maisha huru, kuna vifungo vingi vya kijamii ambavyo vinafanya watu kuishi maisha ambayo hawayafurahii.
Jamii zinakazana kuwatengenezea watu hadithi za maisha yao, kwamba watu kama wewe huwa hawafanyi hivi au huwa wanafanya vile. Kwa hadithi kama hizi unashindwa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako kama hayaendani na ile hadithi ambayo jamii imekuwa inakuuzia. Kuna hadithi kuhusu elimu, kazi, namna ya kuishi na mengine mengi.
Kuna watu ambao wapo kwenye kazi ambazo ni mizigo kwao, lakini hawawezi kuacha kwa sababu jamii zitawachukulia ni watu wa ajabu. Mtu yupo radhi ateseke kwenye kazi kwa miaka mingi ili tu jamii imwone anafanya kazi ambayo inakubalika kwenye jamii.
Kuna watu ambao wanateseka kwenye ndoa kwa miaka mingi lakini hawawezi kuchukua hatua kwa sababu anaogopa jamii itamchukuliaje. Hivyo anakubali kuishi maisha yasiyo huru ili tu kwa nje jamii imwone yupo kwenye ndoa.
Kutaka kuiridhisha jamii ni utumwa ambao ni mzito sana kubeba. Na ni utumwa wenye manyanyaso makubwa kuliko hata ule wa kujitakia mwenyewe. Kwa sababu unapojaribu kwenda tofauti na jamii inavyotaka, kila mtu anakuona unakosea sana na hivyo kuona ni heri uendelee kufanya kile kinachokubalika hata kama siyo bora kwako.
Hatua ya kuchukua kwenye changamoto hii.
Elewa kwamba jamii ipo kwa ajili ya ushirikiano na siyo kwa ajili ya kufanya maisha yako yawe hovyo. Na pia elewa taratibu nyingi za kijamii kwa sasa hazina ule umuhimu ambao ulikuwepo zamani. Kwa sasa tunapaswa kuishi kwenye jamii kwa kushirikiana na sio kupeana hofu. Fanya yale maamuzi ambayo ni muhimu kwako, na wale ambao wanakujali kweli kwenye jamii watakuwa pamoja na wewe. Usiogope kama vile jamii itakutenga na kukuacha, hii ni hofu ambayo imejengwa kwa wanajamii ili wakubaliane kwa kila kitu, lakini kwa dunia ya sasa, hakuna anayeweza kukutenga na kila mtu.
Changamoto ya tatu; Dini.
Hapa ndipo pagumu kwa sababu panahusisha hisia zaidi ya kufikiri. Kwa kifupi ni kwamba upo kwenye dini uliyopo, kwa nafasi kubwa ni kutokana na ulizaliwa kwenye jamii yenye dini hiyo, iwe ni wazazi, walezi au jamii kwa ujumla. Ni watu wachache sana ambao wamekuja kuijua dini ukubwani, au kuhama dini kabisa wakiwa wakubwa. Hivyo kama wewe ni muisilamu uko hivyo kwa sababu ulizaliwa kwenye jamii ya Kiislamu. Na kama ni Mkristo ni kwa sababu ulizaliwa kwenye jamii ya Kikristo.
Sasa dini hizi ambazo umekua nazo tangu utoto zimepandikiza mambo mengi katika akili yako. Mambo haya yanapelekea baadhi ya watu kuishi maisha yasiyokuwa na uhuru. Kama ambavyo tumewahi kujadili kwenye moja ya makala za FALSAFA, lengo kuu la dini yoyote ni kumwezesha mtu kukua kiroho. Unapokua kiroho unajua ni nini dhumuni la maisha yako na unaweza kupambana na changamoto unazokutana nazo kwenye maisha. Lakini dini nyingi zimekuwa zinawajenga watu kwenye misingi ya hofu, na tena hofu ya vitu ambavyo havipo kwa sasa.
Kuna mambo mengi ambayo ni muhimu kwa watu kufanya, lakini wanashindwa kuyafanya kwa sababu ya dini zao. Wanaona watachukuliwaje na wale waumini wenzao. Hili limekuwa linapelekea wengi kuwa na unafiki na kuwa na maisha yenye pande mbili. Upande wa kwanza ni ule ambao unaonekana na watu wengine, na upande wa pili ni ule ambao hauonekani na wengine. Dini zimekuwa zinawazuia watu kuishi yale maisha yenye uhuru na hivyo kujikuta wakifanya mambo ambayo ni mabaya zaidi.
Jinsi ya kuondokana na changamoto hii.
Kwenye dini yoyote ambayo upo, tafuta kukua kiroho. Acha ushabiki wa mambo ambayo hayana msingi, acha kujazwa hofu ambazo zinakufanya uone maisha kama hayana maana, badala yake tafuta ukuaji wa kiroho, ambao utakuwezesha kujua dhumuni la maisha yako na pia kukuwezesha kupambana na changamoto za maisha ambazo unakutana nazo kila siku.
Uhuru wa maisha ndiyo kitu pekee tunachohitaji ili kuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio. Uhuru huu unaweza kuutengeneza wewe mwenyewe kwa kuchagua kufanya kile ambacho ni muhimu kwako ila tu kisiwe kinaingilia uhuru wa wengine au kuvunja sheria na taratibu.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea uhuru wa maisha yako,
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz