Biashara zina changamoto mbalimbali katika uendeshaji. Zile biashara ambazo unaona zimekua na kufanikiwa, siyo kwamba hazina changamoto ila waendeshaji wa biashara hizo wanajua jinsi ya kukabiliana na changamoto za kibiashara wanazokutana nazo. Moja ya changamoto ambazo zinasumbua biashara nyingi ni hali ya kutokuelewana baina ya mteja na mfanyabiashara.
Kuna nyakati ambazo mteja anakutana na changamoto kupitia biashara yako. inawezekana ameuziwa kitu ambacho yeye hakuagiza. Au ameuziwa kitu lakini hakijamsaidia kama alivyokuwa anatarajia. Wakati mwingine mteja anafanya makosa ambayo yanafanya kile alichouziwa kishindwe kumsaidia. Hizi ni hali ambazo zinaweza kutengeneza hali ya kutokuelewana na wateja wako, hasa pale unapokosa mbinu nzuri za kukabiliana na hali hizi.
Katika dunia ya sasa ambapo utandawazi umekua sana, ni rahisi kwa taarifa ambazo siyo sahihi kuhusu biashara yako kusambaa kwa kasi. Hivyo mteja ambaye hajaridhika na biashara yako anaweza kutoa taarifa hasi kuhusu biashara yako na kukupunguzia wateja. Ni muhimu sana kuhakikisha unatatua changamoto zote ambazo wateja wanakutana nazo kwenye biashara yako ili kuepusha taarifa zisizo sahihi kusambaa kuhusu biashara yako.
Kitu kingine muhimu kujua ni kwamba wateja ambao wana changamoto au matatizo na biashara yako ndiyo wateja unaweza kuwatumia kujifunza na kujenga biashara yako vizuri. Wateja hawa ndio wanaokufanya uone maeneo ya biashara yako ambayo umekuwa huyafuatilii kwa karibu. Na pia watakusaidia kuondokana na changamoto kama hizo kwa wateja wa baadaye kwenye biashara yako.
Katika kutatua changamoto ambazo mteja anakutana nazo kwenye biashara yako zingatia mambo yafuatayo;
Mwelewe mteja vizuri kabla hujajaribu kutatua changamoto yake. Hakuna kitu muhimu kama kumwelewa vizuri mtu, kuelewa hali anayopitia na changamoto yake hasa. Unapomwelewa mtu vizuri ndipo unapoweza kuchukua hatua ambazo zitamsaidia kuondokana na changamoto ambayo anapitia. Na wakati unajaribu kumwelewa mtu vizuri usihukumu kabla hujasikia na kuelewa vizuri. Ni rahisi kuhukumu kwamba mteja alifanya makosa mwenyewe kwa kuagiza kitu ambacho hakiendani na mahitaji yake, lakini kumbe hakupewa maelezo sahihi kulingana na kile alichoagiza. Kwa kujua hili itakusaidia kurekebisha utoaji wa taarifa ili baadaye changamoto kama hiyo isitokee kwa wateja wengine. Kabla hujakimbilia kutoa uamuzi wako, mwelewe mteja, na ili kumwelewa vizuri vaa viatu vyake. Jiulize kama wewe ungekuwa ndiyo mteja, je ungekuwa unajisikiaje kwenye hali ambayo unapitia? Unapovaa viatu vya mteja wako unamwelewa vizuri kwa kile anachopitia.
Angalia maslahi na siyo ushindi. Kitu kikubwa ambacho kinafikia mfanyabiashara na mteja kushindwa kuelewana kabisa ni pale ambapo mfanyabiashara anapotaka kuonesha kwamba matatizo ni ya mteja na hivyo yeye hahusiki. Katika kutafuta hilo mfanyabiashara anataka ashinde na mteja ashindwe, na hivyo itapelekea kuwa na mashindano ya muda mrefu. Ni muhimu kujua ya kwamba unachohitaji kwenye hali kama hii siyo kushinda, bali kuangalia maslahi ya mteja na ya kwako na kisha kuona ni kwa jinsi gani unaweza kutatua tatizo hilo na wote mkanufaika. Kwa kubadili mtazamo wako kutoka kwenye mashindano kuja kwenye kuangalia maslahi utaona sehemu ambayo kwa pamoja mnaweza kunufaika. Kumbuka jinsi ambavyo wewe hutaki kupoteza, ndivyo ambavyo mteja naye hataki kupoteza. Unapofikiria njia ambayo inawanufaisha wote kwa pamoja, utapata mwanga zaidi.
Kuwa tayari kuingia hasara kutatua changamoto ya mteja na kuendeleza mahusiano yenu ya kibiashara. Kuna wakati ambapo utahitaji kuchukua hatua ambayo wewe itakupa hasara lakini itamridhisha mteja na hivyo kumfanya aendelee kuja kwenye biashara yako. wakati mwingine unafanya hivi hata kama mteja ndiye mwenye makosa. Hii unajua kwa kuangalia thamani ambayo mteja analeta kwenye biashara yako, na kama ni biashara ambayo ni endelevu unapima thamani ya baadaye pia. Unaweza kuingia hasara kidogo sasa lakini ukajenga uaminifu mkubwa sana kwa wateja wako. Na hapa wateja wanaporidhishwa wanasambaza habari zako kwa watu wengine wengi.
Hakuna mtu ambaye anakuja kwenye biashara yako akitegemea kupata changamoto, hivyo inapotokea mteja wako amepata changamoto kwenye biashara yako, ni jukumu lako kama mmiliki wa biashara kuhakikisha changamoto ya mteja imetatuliwa na ameridhika na huduma aliyoipata. Hili ni eneo muhimu la biashara yako hivyo ni muhimu ukawa na utaratibu mzuri wa kutatua changamoto za wateja wako.
Changamoto kama hizi zinanitokea kwenye biashara yangu kila wakati, katika ujumbe huu nmejifunza kitu.
LikeLike
Vizuri kwa kujifunza,
Muhimu sasa ni uchukue hatua.
LikeLike