Kujua na kufanya ni vitu viwili tofauti kabisa. Japo wengi wamekuwa wanavifananisha, lakini ni vitu ambavyo havifanani hata kidogo. Kujua ni hatua moja, kufanya ni hatua nyingine muhimu sana. Na mbaya zaidi kufanya ni hatua ngumu kuliko kujua.
Watu wengi wanajua ya kwamba kula vyakula bora ni muhimu kwa afya zao, lakini hawafanyi hivyo. Wengi wanajua ya kwamba matumizi ya vilevi kupitiliza au uvutaji wa sigara ni hatari, lakini wanafanya hivyo.
Watu wengi wanajua ili kufanikiwa unahitaji kuweka juhudi kubwa kwenye kile wanachofanya, wanahitaji kutokukata tamaa na kila siku kupiga hatua. Lakini wengi hawawezi kufanya hivyo, hawapo tayari kuweka juhudi kubwa na wanapokutana na changamoto wanakuwa wa kwanza kukata tamaa na kuacha kufanya.
Watu wengi wanajua ni njia zipi bora za kuendesha na kukuza biashara zao. Wanajua kwamba mzunguko wa fedha kwenye biashara ni muhimu, unahitaji kudhibiti matumizi na kuongeza mauzo. Lakini wengi bado hawawezi kudhibiti matumizi yao ya biashara.
Hapo ulipo wewe unajua vitu vingi sana juu ya kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio, lakini hufanyii kazi vitu hivyo unavyovijua na hivyo maisha yako yanazidi kuwa magumu na ya hovyo. Unajua ya kwamba furaha inaanzia ndani yako mwenyewe na sio kwa watu wengine au vitu vingine, lakini bado unasubiri watu au vitu ndiyo vikupe furaha.
Kujua pekee haitoshi, unahitaji kufanya kile unachojua. Na siyo kufanya mara moja, bali unahitaji kufanya kwa kurudia tena na tena na tena. Kufanya mara moja hakuleti matokeo unayotaka, bali kufanya mara nyingi bila ya kuchoka.
Kujua kitu halafu hukifanyi, kunakuumiza sana kuliko yule ambaye hajui. Wewe ambaye unajua na hukufanya nafsi yako inakuumiza zaidi kuliko yule ambaye hajui na hafanyi.
Hebu sasa tumia kile ambacho unakijua, katika maisha yako ya kila siku, jichunguze kwa kila unachofanya na jiulize je hivi ninavyofanya ndivyo ninavyojua? Je ndiyo njia ya kupata matokeo bora? Kama jibu ni hapana tumia njia ile bora ambayo umeshajifunza.
Usiwe mjuaji pekee, bali kuwa mfanyaji. Na mambo madogo madogo ndiyo yanayoleta mafanikio makubwa, usiyapuuze. Kuwa tayari kuweka juhudi na utapata matokeo bora.
TUPO PAMOJA.
Kocha Makirita Amani.