Habari mpendwa rafiki na msomaji wa AMKA MTANZANIA? Natumaini unaendelea vema katika kujenga na kuboresha maisha yako na kugusa maisha ya watu wengine kulingana na kile unachofanya, licha ya kukumbana na changamoto za hapa na pale ambazo hatuwezi kuzikwepa kwani changamoto ni sehemu ya maisha yetu. Hivyo basi, ndugu msomaji karibu katika makala yetu ya leo tuweze kusafiri pamoja mpaka mwisho wa makala hii.
Siku zote upendo huzaa upendo na mambo hasi huzaa mambo hasi. Katika jamii yetu ya leo kumeibuka kansa inayoenea kwa kasi sana ambayo athari yake ni kubwa inayomwathiri mtu mmoja mpaka jamii kwa ujumla. Kuna mambo hasi ambayo yanasambaa kwa kasi katika jamii yetu na hivyo tusipoyakemea yataendelea kusambaa kama vile kansa katika mwili hatimaye kuathiri jamii kwa ujumla.

Leo katika makala yetu tutakwenda kuinuka na kwenda kuzika majeneza ambayo yamekuwa mzigo katika maisha yetu. Kwanini tuendelee kukaa na majeneza ambayo yanatuumiza na wakati tunaweza kwenda kuyazika. Tukiendelea kukaa na vitu ambavyo vinatuathiri katika miili yetu ni kama ugonjwa wa kansa ambao tusipouwahi unaweza kuenea mwili mzima. Ili tuweze kuwa na jamii bora ni muhimu kujenga familia bora. Hatuwezi kuwa na jamii bora kama hatujengi familia bora na familia bora inajengwa na mimi pamoja na wewe kulingana na nafasi yako uliyonayo katika familia hata jamii pia.
Hakuna kitu kitakachotokea katika maisha yetu bila kuinuka na kwenda kutenda. Ukiwa unahisi njaa inuka na kwenda kutafuta chakula, kama una uzito uliopitiliza inuka nenda kafanye mazoezi, kama umezungukwa na wakatisha tamaa inuka nenda kazungukwe na watu chanya. Sasa yafuatayo ni mambo unayotakiwa kuinuka na kwenda kuyazika.

1. Kutosamehe;
Kama uko kwenye jeneza la kutosamehe tafadhali inuka na nenda kazike jeneza hilo. Kukaa katika jeneza la kutosamehe ni kubeba mzigo mkubwa ambao unakutesa na kukunyima raha. Kukaa bila kusamehe ni kujizibia fursa na baraka. Kuendelea kusema nimekusamehe lakini sitokuja kusahau ni kuendelea kukaa katika jeneza la kutokusamehe. Kumbuka msamaha ni zaidi ya kutamka kwa mdomo. Msamaha ni kumaliza chuki na maumivu yote ndani ya moyo. Kutosamehe ni kuendelea kueneza ugonjwa wa kansa katika mwili wako ambao utakuathiri wewe mwenyewe na jamii kiujumla. Hivyo, kusamehe ni amri na siyo hiari na mwasisi wa msamaha ni Mwenyezi Mungu kama yeye anatusamehe kwa nini wewe usimsamehe jirani au ndugu yako? Inuka na nenda kasamehe na kuzika kabisa hilo jeneza la kutosamehe.

2. Kutowajibika;
Inuka nenda kawajibike hakuna kitu kitakachokuja katika maisha yako bila kuwajibika. Huu siyo muda wa kumlaumu mtu juu ya maisha yako na jukumu la maisha yako ni lako mwenyewe wewe ndio mwenye maamuzi ya kuweka chanel yoyote katika maisha yako na kuiangalia ukiwa umekaa kwenye kochi. Kama wewe ni baba, mama, kiongozi wa serikali au wa dini inuka na wajibika katika nafasi yako. Usipowajibika utawaambukiza kizazi chako laana ambayo itasambaa kama kansa na kuathiri mpaka jamii kwa ujumla. Wajibika usisubiri mpaka uwe na cheo ndio uchukue hatua na kuongoza yaani wewe ongoza bila kuwa na cheo chochote chukua hatua usisubiri ruhusa. Mwandishi mashuhuri duniani Robin Sharma anasema lead without a title katika kitabu chake cha the leader who had no title, usisubiri kuambiwa chukua hatua.

3. Wivu;
Wivu ni kama kansa katika karni hii ya 21 ambayo inasababisha watu kutafuta mali hata katika njia zisizostahili. Hakuna wivu mzuri wala mbaya wivu ni wivu tu. Utatamani kitu ambacho huna uwezo wako utaingiwa na tambaa itakayokupelekea kutenda kitu ambacho hakistahili. Watu wanaoneana wivu bila sababu ya msingi, watu wanauana sababu ya kisa cha wivu. Wivu ni hali ya kuwa na mtazamo hasi juu ya mtu Fulani au kitu Fulani. Wapo watu ambao hawapendi tu kuona wenzao wakifanikiwa katika jambo lolote, anataka kuona wote muwe sawa na kubaki katika jeneza hilo. Kwa hiyo, inuka nenda kazike jeneza la wivu. Hakuna mtu aliyekatazwa kufanikiwa bali unajikataza mwenyewe na hakuna kizuizi cha umri katika mafanikio.

SOMA; USHAURI; Biashara Unazoweza Kuanza Kwa Mtaji Wa Tsh Laki Mbili Na Kuweza Kufanikiwa.

4. Chuki;
Inuka nenda kaondoe chuki uliyonayo wewe na jirani, kaka, dada, shangazi, mjomba, rafiki, jamaa yako nk. Chuki huzaa mauti usipoimaliza leo itazaa mauti katika jamii yetu. Usipoinuka leo na kwenda kuzika jeneza la chuki hatimaye itakuja kusambaa kama kansa kwako binafsi, familia yako na jamii kwa ujumla. Kukaa na jeneza la chuki bila kuinuka ni kwenda kulizika ni utumwa wa kujitakia yaani wa hiari basi mimi leo nakushurutisha inuka nenda kamalize chuki na uwe na amani ya moyo kwani maisha yetu ni mafupi sana kuishi katika hali ya mtazamo hasi. Dawa ya mtu anayekuchukia ni kumpenda bila sababu.

5. Ubinafsi;
Ubinafsi ni hali ya kujiona wewe unastahili zaidi kuliko mtu mwingine. Katika jamii ya leo kuna ugonjwa huu wa ubinafsi ambao unasambaa kwa kasi sana. Unakuta watu wanaongea na kulalamika eti watu wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa maarifa je ulishawahi kuwasaidia maarifa hayo? Au ulishawahi kuwasaidia watu maarifa uliyokuwa nayo na kuwa msaada kwa watu au umeyakalia tu unahisi ukiwasaidia watu watakupita au? Kama watu wangeweza kukaa na maarifa au thamani waliyonayo je leo dunia ingekuwaje? Hata chombo unachotumia leo kusoma hapa angeamua kukaa na ubinafsi wake je leo tungewezaje kuwasiliana? Toa kile ulichonacho uweze kuisaidia dunia na wala dunia haitoweza kukukumbuka na ubinafsi wako bali itakukumbuka kwa mchango wako uliowasaidia siyo kujifaidisha tu wewe na familia yako tu. Ubinafsi hauwezi kuleta maendeleo na kujenga taifa hivyo basi, inuka nenda kazike jeneza hili la ubinafsi kwani likiendelea kuwepo litazidi kusambaa kama kansa hatimaye kuathiri jamii yetu kwani ubinafsi hautoweza kurefusha wasifu wako pale unapokuwa unasomwa wakati wewe umelala kwenye jeneza na watu watakulilia kama wewe uligusa maisha yao na kuacha kumbukumbu katika maisha yao.

6. Umbea, Majungu na Kusengenya;
watu wamefanya umbea, majungu na masengenyo kuwa kama sehemu ya maisha yao na kuishi nayo kama vile ni desturi, ni jambo tu la kawaida. Siyo sahihi kukaa na majeneza ya umbea, majungu na masengenyo kwani yanaleta majeraha ya moyo kwa watu tafadhali wewe uliobeba majeneza haya inuka hapo ulipo kama ni kazini, msikitini, kanisani, mtaani na sehemu nyingine inuka nenda kazike haya majeneza kwani hayana faida zaidi ya kukurudisha nyuma kimaendeleo na kukupotezea muda. Hii ni kansa mbaya inayosambaa kwa kasi katika shuguli zetu za kazi hata uzalishaji wa hali ya juu unapungua na maendeleo hayawezi kuletwa na majungu, umbea na masengenyo bali hii ni kansa mbaya inayorudisha nyuma maendeleo.

7. Uvivu;
Uvivu ni kikwazo cha maendeleo kwa mtu, jamii mpaka taifa kwa ujumla. Uvivu ni utumwa, ugonjwa ambao unashambulia jamii kwa kasi sana, kasi hii inakwenda kuathiri jamii yetu. Kuna watu wavivu hata wa kufanya usafi wa mwili wake binafsi, uvivu ni adui wa maendeleo. Siku hizi kuna uvivu hata wa akili yaani uvivu wa kushindwa kufikiri kitu kidogo anaona aulize gugo, watu siku hizi hawafikirii na kufikiri ni kazi ngumu sana wanaofikiri ndio wanaleta mageuzi hapa duniani. Uvivu unaleta matokeo hafifu katika kazi, unaleta kero katika mahusiano yetu uvivu ni mbaya. Hivyo basi, tafadhali inuka nenda kazike jeneza la uvivu ukiendelea kukaa nalo litasambaa na kuambukiza watu wengine.

SOMA; Umuhimu Wa Mawasiliano Katika Kujenga Mahusiano Bora Ya Kijamii.

8. Kulalamika;
Kulalamika ni kupoteza muda na nguvu. Chukua hatua badala ya kulalamika ili uokoe nguvu na muda wako kwani ni rasilimali mbili muhimu katika rasilimali muhimu sana hapa duniani. Siku hizi tabia za watu ni kukaa vibarazani, vijiweni, makazini ni kulalamika tu bila sababu. Leo inuka nenda kazike jeneza la kulalamika kwani ni kansa inayoenea kwa kasi zaidi. Unakuta mtu analalamika hana muda kusoma vitabu na kutanua wigo wa maarifa lakini anao muda wa kuangalia mpira, maigizo, filamu, kufuatilia habari na mitandao ya kijamii lakini muda wa kulisha chakula cha ubongo wake hana kabisa hivyo badilika na kazike hayo majeneza ambayo yanaharibu maisha yako.

9. Kuhukumu;
Watu siku hizi wamegeuka kuwa Mafarisayo kwa kuwahukumu watu wanajiona wao ni kama malaika wa kuhukumu watu. Haijalishi vyeo tulivyonavyo hapa duniani kwa Mungu wote tupo sawa. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuhukumu wala sio mimi wala wewe. Acha kuhukumu kwa macho ya kibinadamu huna ukweli wowote juu ya mtu unaanza kumuhukumu bila sababu. Usihukumu, usihukumu, usihukumu inuka nenda kazike jeneza la kuhukumu mara moja. Huu ugonjwa unaenea kwa kasi na kusambaa kama vile kansa inavyoshambulia mwili wa binadamu. Tuache kuhukumu bila kujua ukweli

10. Ulevi;
Nguvu kazi ya vijana inapungua kila siku kwa ajili ya unywaji wa pombe kwa kupindukia. Vijana wanaangamia kwa janga la unywaji viroba mtu yuko radhi kukosa chakula lakini apate kiroba. Watu wanaamkia kwenye vilabu vya pombe asubuhi badala ya kuamkia katika kazi. Watu ukiwaona wamechoka wamechakaa hawana hata nguvu je mtu huyu ataweza kuwa na familia bora na kujenga jamii bora? Ulevi unaleta magomvi katika familia, jamii nk. Madhara ya ulevi ni makubwa sana hasa kwa vijana wanaozeeka kabla hata ya umri wao ukiwaona nyuso zao utafikiri ni wazee wa miaka mingi kumbe ni vijana. Kama uko katika jeneza hili au unaona watu wanaangamia kuwa balozi wao hakikisha wanainuka na kwenda kuyazika majeneza hayo kwani yanasambaa kwa kasi katika jamii yetu.
Mwisho, maisha yetu ni mafupi sana kuendelea kuishi katika hali ya mitazamo hasi na maisha yetu ni marefu kama tukitumia muda vizuri na kuishi katika mtazamo chanya. Vitu vyote vya mtazamo hasi ni majeneza ambayo tunatakiwa kuinuka na kwenda kuyazika kuliko kuendelea kukaa nayo na mwishowe kusambaa kwa kasi na kuleta athari kubwa kwa jamii.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com