Tumekuwa tunafikiri ya kwamba ili kufanikiwa kwenye maisha, mara zote tunahitaji kupiga hatua mbele. Tunahitaji kwenda mbele kwa mbele na nyuma ni mwiko kabisa. Lakini hakuna sehemu muhimu kwenye mafanikio yako kama kupiga hatua nyuma. Tena naweza kusema kama unaona kila kitu kinakwenda mbele peke yake kuwa na wasiwasi, huenda kuna vitu haviko vizuri au unaelekea kwenye shimo baya sana ambalo litakupoteza kabisa.

Kama una shilingi elfu kumi, unaweza kuitumia kufanya kitu ambacho ni kizuri na kikakuletea faida, au unaweza kukaa nayo bila ya kuifanyia chochote au unaweza kuitumia kufanya kitu na ukaipoteza. Wengi watakazana kuhakikisha hawaitumii hiyo elfu kumi kwa kufanya kitu ambapo wataipoteza, wakiamini kwamba kuipoteza fedha hiyo ni hasara kubwa. Lakini inawezekana kwenye kuipoteza fedha hiyo ukapata faida kubwa sana hasa kwa baadaye.

Tunapopiga hatua nyuma tunajifunza vitu vingi kuhusu sisi wenyewe na kile ambacho tunafanya. Tunajifunza njia zipi bora kupata matokeo tunayotaka na njia zipi za kuepuka ili kukwepa hasara. Kuhusu sisi wenyewe tunajifunza mambo ambayo tumekuwa tunahofia kuyafanya na pia tunajifunza kuhusu mambo ambayo tumekuwa tunafanya kwa mazoea.

Unapopiga hatua moja nyuma, unapata nafasi ya kupiga hatua tano mbele. Unapata funzo kubwa ambalo litakuwezesha kuepuka kurudia makosa ambayo umeshayafanya. Na pale unapofanya makosa na kujifunza kwenye hatua ndogo, unaweza kuziendea hatua kubwa bila ya wasiwasi.

Ili kufanikiwa hatuhitaji kuepuka kushindwa kwa nguvu zetu zote, wala hatuhitaji kuhakikisha hatupigi hatua nyuma kamwe, badala yake tunahitaji kujifunza kwa kila hatua ambayo tunapitia kwenye maisha yetu na kwa kila tunachofanya.

Tunapopiga hatua mbele tujifunze, ni vitu gani vimetuwezesha kupiga hatua mbele. Na pia tunapopiga hatua nyuma tujifunze, ni vitu gani vimesababisha turudi nyuma.

Changamoto ipo hapa, tunapopiga hatua mbele tunaona ni kawaida, na hivyo hatujifunzi sana. Na kama tumeshapiga hatua mbele mara nyingi, tunaona ni kitu ambacho tumeshazoea kufanya. Lakini tunapopiga hatua nyuma hapa ndipo tunapostuka, hapa ndiyo tunagundua kuna kitu hakipo sawa na hivyo kuchukua hatua haraka sana. Hii ndiyo sababu watu wengi wanajifunza vizuri kupitia kushindwa kuliko kushinda.

Unapopiga hatua moja nyuma, ni fursa kubwa kwako kupiga hatua tano mbele baadaye kama utatumia vizuri hatua hiyo moja uliyopiga nyuma.

Tahadhari; usiumizwe na ile hatua unayopiga nyuma na wala usifanye mambo kwa uzembe ukiamini kushindwa kutakusukuma zaidi. Weka juhudi zako zote, halafu yale matokeo utakayopata jifunze kupitia hayo.

TUPO PAMOJA,

KOCHA.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).