Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu kwenye makala yetu ya leo ya FALSAFA MPYA YA MAISHA ambapo tunashirikishana mambo muhimu kuhusu maisha ili tuweze kuwa na maisha bora yenye furaha na mafanikio makubwa.
Tatizo moja ambalo limekuwa linafanya maisha ya wengi kuwa ya hovyo ni kukosa misingi. Tumekuwa kwenye jamii ambazo hatupewi misingi ya kusimamia kwenye maisha yetu. Na hata kama tunapewa misingi, hatupewi kuielewa badala yake tunapewa kwa vitisho kwamba ukifanya hivi ni adhabu au dhambi. Kwa njia hii watu wamekuwa wakivunja misingi hiyo pale ambapo wanajua hakuna anayewaona. Tatizo la misingi ni kwamba ukiivunja tu maisha yako yanakuwa magumu, iwe wengine wamekuona au la.
Hivyo leo tunarudi kwenye misingi ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuisimamia kama kweli anataka kuwa na maisha bora na yenye mafanikio. Misingi minne tutakayokwenda kushirikishana hapa siyo mipya, na huenda umeshaisikia kwenye maeneo mbalimbali kama dini au falsafa nyinginezo.
Misingi hii imekuwepo kwa zaidi ya miaka 2000, imekuwepo tangu kipindi cha mwanafalsafa Aristotle. Misingi hii iliwawezesha wanafalsafa hao kuwa na maisha bora na kuweza kutengeneza jamii bora kwa kipindi chao. Lakini mpaka sasa bado siyo watu wote wanaoweza kusimamia misingi hii na hivyo yatupasa tukumbushane kwa lugha rahisi tunayoweza kuelewana.
Kumbuka lengo letu kwenye falsafa hii mpya ya maisha ni kujenga msingi wa maisha bora, siyo tu kujua vitu bali kuvitumia vitu hivyo kuboresha maisha yetu. Hivyo basi, unapojifunza misingi hii minne, unahitaji kuanza kuiishi kama ulikuwa bado hujaanza kufanya hivyo.
Misingi minne ya maisha ya wema.
Maisha ya wema ni maisha ambayo yana manufaa kwa mtu na kwa jamii inayomzunguka. Ni maisha ambayo mtu anaangalia mbali na anaangalia jamii kwa ujumla badala ya kujiangalia yeye mwenyewe. Kupitia maisha haya mtu anaielewa na kuiishi sheria iliyo kuu ambayo ni kumfanyia mwingine kile ambacho ungependa yeye akufanyie wewe.
Hii hapa ni misingi minne ya maisha haya ya wema.
Msingi wa kwanza; BUSARA NA HEKIMA (WISDOM/PRUDENCE).
Katika misingi minne, busara na hekima ndiyo msingi muhimu sana, kwa sababu ni kupitia msingi huu ndiyo tunafanya maamuzi yote muhimu kwenye maisha yetu.
Busara inatokana na maarifa sahihi na kuweza kuyatumia maarifa hayo kwenye eneo sahihi. Busara pia inatokana na uzoefu ambao mtu anakuwa amepitia kwenye maisha yake. Hakuna mtu ambaye anazaliwa na busara, bali mtu anajijengea busara, kwa kupata maarifa na kuyatumia kwa usahihi.
Busara ni tofauti kabisa na akili, kuwa na akili haimaanishi kuwa na busara. Kwa mfano mtu anaweza kujua kitu siyo kizuri kufanya, lakini akakifanya, akili anayo ila amekosa busara.
Busara inatuwezesha kufanya maamuzi bora kwenye maisha yetu, kuepuka kufanya makosa na kuweza kupata kile ambacho tunakitaka.
Ili kujijengea busara unahitaji kufanya yafuatayo;
- Kuwa tayari kujifunza kila siku na kila wakati. Jifunze kupitia kila unachofanya na kila unayekutana naye.
- Jua ya kwamba hujui. Pale ambapo mtu anaanza kujiona anajua kila kitu ndipo anapopoteza busara. Hakuna mtu anayejua kila kitu, hivyo usijione unajua kila kitu, hata kama unajua vitu vingi kuliko wengine.
- Jifunze kupitia makosa yako, wenye busara hawakatai makosa yao, bali wanayakubali na kujifunza. Na watu wapo tayari pale ambapo mtu anakiri makosa na kuahidi kutorudia tena. Wenye busara wanajua hakuna aliyekamilika, ila waliokosa busara hukazana wasionekane wana makosa.
Jijengee busara, hili ni zoezi la kila siku kwenye maisha yako.
Msingi wa pili ni HAKI (JUSTICE).
Msingi wa haki ni kumpa mtu kile anachostahili na kutekeleza wajibu na majukumu yetu kwa wakati. Katika jamii zetu tunachanganyikana na watu mbalimbali, kuna ambao wana uwezo na mamlaka kuliko sisi, wengine wana uwezo na mamlaka ya chini kuliko sisi. Ni jinsi gani unaweza kwenda na watu hawa inategemea na jinsi ulivyojijengea msingi wa haki.
Unapokuwa mtu wa haki unawapa watu kile ambacho wanastahili kupata. Unafanya hivyo bila ya kujali kama mtu huyo ana uwezo zaidi yako au ana uwezo wa chini yako. Pia unapokea majukumu yako na kuyatekeleza kwa wakati.
Tatizo la jamii zetu ni kwamba wale wenye uwezo na mamlaka kubwa wanaweza kuamua kuwafanyia chochote wale ambao wako chini yao, kwa sababu wanajua hawana cha kuwafanya. Lakini kama ilivyo sheria ya dunia, kila kitu kinapita na kuna siku aliyekuwa juu anaweza kuwa chini.
Jenga maisha yako kwenye msingi wa haki, wape watu kile ambacho wanastahili kupewa, tekeleza majukumu yako kwa wakati.
Kama kila mtu angefagia njia yake, tungekuwa na dunia ambayo ni safi sana. Kama kila mtu angetekeleza wajibu wake kwa wakati, dunia ingekuwa sehemu bora sana ya kuishi. Tuanze kutengeneza hili, kwa kutekeleza wajibu wetu na kuwapa watu kile ambacho wanastahili kupewa.
Msingi wa tatu ni UJASIRI (FORTITUDE/COURAGE)
Maisha siyo rahisi, siyo kila kitu kitakwenda kama tulivyopanga, na njia yetu ya kuelekea mafanikio ina vikwazo na changamoto nyingi. Tunahitaji ujasiri ili kuweza kupambana na changamoto hizi na kuweza kufikia yale maisha ambayo tunayataka. Ujasiri ni msingi muhimu kwenye maisha ya wema. Ujasiri unatuwezesha kusimamia haki hasa pale ambapo jamii nzima haifanyi hivyo.
Hofu ni changamoto nyingine kubwa kwa wengi kufikia mafanikio. Watu wanakuwa na malengo na mipango mikubwa, ila wanapoanza utekelezaji hofu inapiga hodi. Hofu inaanzia ndani yao na pia inatoka kwa wale wanaowazunguka. Wale wanaofanikiwa ni wanaoweza kuizidi hofu na kufanya.
Ujasiri siyo kutokuwa na hofu, bali mtu kufanya licha ya kuwa na hofu. Ujasiri unatuwezesha kuyaweka maisha yetu hatarini katika kusimamia kile ambacho tunakiamini na tunajua ni haki.
Jijengee ujasiri na huu utakuwezesha kusimamia kile unachoamini.
Msingi wa nne ni KIASI (TEMPERANCE)
Tunahitaji kuwa na kiasi kwenye kila jambo tunalofanya, hasa kwenye hamu na starehe zetu. Kwa asili tunapenda kutimiza hamu zetu, hamu ya chakula, hamu ya kunywa na pia tunapenda kustarehe na kupumzika. Japokuwa vitu hivi ni vizuri na muhimu kwetu, hatuwezi kupata kadiri tunavyotaka. Tunahitaji kuwa na kiasi kwenye kila tunachofanya. Tunapofanya kupita kiasi tunajiharibia mambo mengine mazuri kwenye maisha yetu na kuingilia maisha ya wengine pia.
Misingi hii minne inategemeana sana, kukosa msingi mmoja kunaharibu misingi mingine mitatu. Na hivyo kukosa msingi mmoja pekee kunakufanya usiwe mtu mwema. Kwa mfano kukosa kiasi kunatuondolea ujasiri na kama hatuna ujasiri hatuwezi kusimamia haki, bila ya haki hatuwezi kusema tuna busara au hekima.
Misingi hii minne inapaswa kwenda pamoja kwenye maisha yetu ya kila siku.
Ongeza misingi hii minne kwenye falsafa yako mpya ya maisha, na ishi misingi hii kila siku.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,