Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Unatumiaje yale unayojifunza kupitia falsafa hii mpya ya maisha kufanya maisha yako kuwa bora zaidi kila siku? Hili ni swali muhimu unalopaswa kujiuliza kila siku.
Mwanafalsafa Plato amewahi kunukuliwa akisema unexamined life is note woth living, akiwa na maana kwamba maisha ambayo hayachunguzwi, hayana thamani ya kuyaishi. Katika mambo tunayofanya kila siku, kuna tunayofanya vizuri na kuna tunayokosea. Tunapata nafasi ya kujua mazuri na mabaya tunayofanya pale tunapochukua hatua na kuanza kujichunguza wenyewe, kujihoji na kujua kwa undani madhara ya kila tunachokifanya.
Hivyo kujiuliza swali la jinsi gani unatumia falsafa mpya ya maisha kuboresha maisha yako ni jukumu lako kufanya kila siku. Yape maisha yako thamani ya kuyaishi kwa kuyachunguza na kuyahoji kupitia kila unachofanya.
Hakuna kitu ambacho kinatokea kama ajali kwenye maisha, kila kitu kinachukua muda mpaka kutokea.
Hakuna mtu anayefunga biashara kwa hasara ya siku moja, bali kuna kuwa na hasara za siku nyingi mpaka biashara inakufa.
Hakuna mtu anayeugua kwa kitu cha mara moja, bali mtu anakuwa kwenye mazingira yanayochochea ugonjwa kwa muda mrefu mpaka anafikia hatua ya kuugua.
Hakuna mtu anayefukuzwa kazi kwa kosa moja, bali mtu anakuwa na makosa mengi mpaka anakuwa mzigo kwenye kazi na hivyo anafukuzwa.
Hakuna ndoa inayovunjika kwa kosa la siku moja, bali kunakuwa na makosa mengi ambayo yamefikia hatua ya watu kushindwa kuendelea kuwa pamoja.
Kila kitu kinachotokea kwenye amisha yetu, kina muda mrefu wa kusababishwa, lakini wengi huwa hatuoni muda huo kwa sababu hatuyachunguzi maisha yetu, hatuhoji matendo yetu, tunakwenda tu na mambo yanavyokwenda.
Tungekuwa na utaratibu wa kuyachunguza maisha yetu na kujihoji, tungeona mwenendo wetu siyo mzuri, tungeona dalili za biashara kwenda kwa hasara, tungeona mwenendo wetu kwenye kazi ukiwa siyo mzuri na pia tungeona mahusiano yetu na wengine yakianza kuporomoka.
Plato aliona hili zaidi ya miaka 2000 iliyopita na kuona umuhimu wa watu kuchunguza maisha yao na kuhoji matendo yao. Lakini mpaka leo hii kuna kundi kubwa la watu ambao hawachunguzi maisha yao wala kuhoji matendo yao, wao wanaendelea kufanya kile wanachofanya, mpaka pale mambo yanapokuwa hayawezekani tena, ndipo wanatafuta njia mbadala, kwa bahati mbaya sana wakati huu wanakuwa wameshachelewa sana.
Kuishi na kuwa hai.
Kuna tofauti kati ya kuishi na kuwa hai.
Unaishi pale unapokuwa na maana ya maisha yako, unapojua ni kipi unachangia kwenye maisha ya wengine. Unaishi kama unafanya kile unachopenda kufanya na unayafurahia maisha yako. unapoyachunguza maisha yako na kuhoji matendo yako ni dalili nzuri za kwamba unaishi. Hii ni kwa sababu unajua maisha yako ni zaidi tu ya kuwa hai, unajua kuna kitu unadaiwa kwa wengine na kuwa tayari kukitoa.
Kuwa hai ni pale ambapo unachofanya ni kile kinachokufanya uendelee kuwa hai. Na hivyo msukumo wako mkubwa kwenye maisha yako ni kujiangalia wewe binafsi, kuangalia ni kipi kitakuvusha. Unakuwa hai pale ambapo hufikirii mchango wako kwa wengine, hufikirii kutoa bali unafikiria kupokea, unaangalia ni kipi unachopata. Unapokuwa hai unakazana kufanya vitu ambavyo vitakufanya uendelee kuwa hai, hata kama vitu hivyo havina manufaa kwa watu wengine.
Pale jamii inapokuwa na watu wengi ambao wapo hai badala ya kuishi, ndipo tunapokutana na changamoto nyingi. Ndipo watu wanaposhindwa kushirikiana na kutokea kwa hali za kutokuelewana.
Hatua za kuyachunguza maisha yako.
Kuyachunguza maisha yako siyo zoezi gumu kufanya kama wengi tunavyofikiri, ni zoezi rahisi na tunaloweza kulifanya kila siku.
Unaweza kufanya zoezi hili kila mwisho wa siku yako, na unaipitia siku yako nzima. Angalia ni vitu gani vizuri umefanya kwenye siku hiyo, na vipi ambavyo siyo vizuri ulivyofanya. Jiulize ni mambo yapi mazuri umeyafanya na unahitaji kuendelea kuyafanya kwenye siku inayofuata. Pia jiulize ni mambo yapi ambayo siyo mazuri umeyafanya na unahitaji kuyaepuka kwenye siku zinazofuata.
Pia kwenye yale mazuri uliyofanya, jiulize ungeweza kuyafanyaje kwa ubora zaidi. Kama ungepata nafasi ya kufanya tena, ungeongeza nini. Na kwa sababu utapata nafasi ya kufanya tena, basi utajua ubora wa kuongeza.
Unapoyachunguza maisha yako kila siku, unajua tabia nzuri za kuendeleza na tabia ambazo siyo nzuri za kuacha. Kama uliteleza na kufanya kitu ambacho siyo sahihi, unajirekebisha kabla hujazoea kufanya na ukawa utaratibu wa maisha yako.
Pia kila wiki unahitaji kujichunguza, hasa kwa yale uliyotekeleza kwenye wiki husika na uliyoshindwa kutekeleza. Pia kwenye muda huo unapanga mambo unayohitaji kutekeleza kwenye wiki inayoanza. Unafanya hivyo kwenye mwezi na hata mwaka.
Tumia sheria ya vitu vitatu.
Ili kurahisisha kuyachunguza maisha yako na kuhoji matendo yako, kuwa na sheria ya vitu vitatu. Sheria hii inakwenda kwamba kila siku orodhesha vitu vitatu mara tatu.
Orodhesha vitu vitatua ambavyo umefanikiwa kufanya vinavyokusogeza karibu na malengo yako na kukufikisha kwenye maisha ya ndoto zako.
Orodhesha vitu vitatu ambavyo umeshindwa kufanya au umevifanya kwa makosa na hivyo kuwa kikwazo kwako kufikia malengo yako.
Orodhesha vitu vitatu ambavyo unahitaji kuboresha zaidi, unavyohitaji kufanya kwa ubora. Pia unaweza kuorodhesha vitu vitatu ulivyojifunza kwenye siku yako.
Zoezi hili linaweza kuchukua dakika tano mpaka dakika kumi na tano, lakini litayafanya maisha yako kuwa bora sana.
Fanya hivi kila siku na jikumbushe ni wapi unapotaka kufika. Na inakuwa bora sana kama utaandika kuliko kujiambia tu mwenyewe, unapoandika unamaanisha zaidi kuliko kufikiria kwenye akili yako pekee.
Kwenye falsafa yetu hii mpya ya maisha, kuyachunguza maisha yetu na kuhoji matendo yetu ni sehemu kuu ya maisha yetu, na kila siku tunahitaji kufanya TATU MARA TATU.
Tuyape thamani maisha yetu kwa kuyachunguza kila siku, tujikamate wenyewe tukikosea kabla hata wengine hawajaona makosa yetu. Hii ni njia bora ya kutufikisha kwenye malengo yetu na kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika kujenga falsafa mpya ya maisha yetu.
TUPO PAMOJA,
Rafiki Na Kocha wako,
Makirita Amani,