USHAURI; Jinsi Ya Kuepuka Dharura Zako Na Za Wengine Kuwa Kikwazo Cha Kufikia Malengo Yako.

Habari rafiki yangu?
Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia malengo yetu. Kupitia makala hizi za ushauri wa changamoto tunapeana mawazo mbadala ya kuweza kutatua zile changamoto ambazo ni kikwazo kwetu kufikia malengo na mipango yetu.

Waswahili huwa wanasema mipango siyo matumizi, wakiwa na maana kwamba japo unaweza kuweka mipango mizuri na mikubwa, bado utekelezaji utakuwa tofauti na ulivyokuwa umepanga. Haiwezekani kila kitu kikaenda kama unavyotaka wewe, na kama itatokea hivyo basi unachofanya siyo kikubwa au kama ni kikubwa basi haiwezi kutokea mara nyingi.

Kitu chochote kikubwa utakachopanga kufanya, utakapoanza kutekeleza utakutana na changamoto mbalimbali. Kama hukujipanga vizuri ni rahisi sana kwako kukata tamaa na kuishia pale baada ya kujiaminisha kwamba haiwezekani. Leo kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto tutakwenda kuangalia jinsi ya kuzuia dharura zako binafsi na za watu wa karibu yako kuwa kikwazo kwako kufikia malengo yako.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

Kabla hatujaingia kwenye ushauri juu ya hili, haya hapa ni maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusiana na changamoto hii;

Changamoto yangu unakuta umeishaweka malengo yako mfano. Ya mwezi 1 au miezi 6 inatokea tatizo la ndugu na marafiki wameuguliwa au wakiwa na shida mbalimbali wanaomba msaada wako na unakuta una familia watoto wanasoma na kitega uchumi unacho kimoja tu. Ukikataa kwamba Huna pesa wanakulaumu nifanyeje? Naomba ushauri wako. Nakutakia ujenzi mwema wa Taifa. P. W. Marwa.

Pamoja na wewe kupanga mambo yako vizuri, bado huwezi kuzuia dharura kutokea kwako na kwa wale ambao ni wa karibu kwako. Hivyo unahitaji kuwa na mpango wa ziada juu ya dharura hizi kama kweli unataka kufikia malengo yako. Kwa kukoa mpango wa ziada, unajiweka kwenye nafasi ya kushindwa kabla hata hujaanza kufanya kile ulichopanga kufanya. Nina mambo matatu muhimu sana nataka kuyaongea kuhusiana na hili la dharura na malengo yako;

Jambo la kwanza jua dharura zipo na zitaendelea kuwepo.
Hata siku moja usijitetee ya kwamba kilichokuzuia wewe kufikia malengo yako ni dharura ambazo umekutana nazo kwenye maisha yako. kwa kusema hivi utakuwa unawaonesha watu kwamba bado hujakomaa na hukuwa umejitoa kweli katika kuyafikia malengo yako.

Dharura zipo na zitaendelea kuwepo, huwezi kuzuia watu kuumwa au kupata changamoto ambazo zinahitaji msaada wa haraka. Hivyo kama wewe kweli umejipanga kufikia malengo yako, ni lazima uwe na fungu la ziada kwa ajili ya dharura hizi. Unahitaji kuwa na kiasi cha fedha ambacho umekitenga kwa ajili ya dharura ambazo zinajitokeza kwenye maisha yako na ya wale ambao ni wa karibu kwako.
Kwa kuwa na fungu hili utaweza kuituliza akili yako na kuweza kufanyia kazi malengo yako. Wewe mwenyewe unajua ni kiasi gani cha dharura unaweza kuhitaji kwa kipindi cha mwezi au kipindi kingine, kuwa na kiwango cha aina hiyo.

Kitu cha pili; kuwa na vigezo vya wewe kutoa msaada kwenye dharura za wengine.
Kwenye haya maisha, watu huwa wanatafuta njia rahisi ya kuondokana na matatizo na changamoto zao. Na watu wakishapata njia hiyo rahisi huwa hawajiumizi tena kufikiria. Hivyo kama umekuwa ni mtu wa kuwasaidia wengine wanapokuwa kwenye dharura, watu watakuwa na utegemezi mkubwa kwako. Kila wanapopata tatizo kidogo wanakuja kwako kwa sababu wanajua utawasaidia.
Sasa wewe usiwe mtu wa kusaidia kila kitu, hata vitu vidogo ambavyo mtu angeweza kutatua mwenyewe. Badala yake weka viwango au vigezo ambavyo utatumia kutoa msaada kwa wengine. Na mtu anapokuja kwako kwa kutaka msaada kwa dharura yake, mpe njia nyingine anazoweza kuzitumia kutatua changamoto zake. Ukianza kuwapa njia hizi utaona wengi wanapunguza kuleta changamoto ndogo ndogo.

Sikufundishi uwe na roho mbaya, bali nakufundisha uweze kuwasaidia watu kutatua changamoto zao wenyewe, hasa zile ambazo ni ndogo. Hata kama huna njia ya kuwashauri njia nyingine za kufuata, unaweza kuwahoji ni juhudi kiasi gani wameshachukua mpaka kufika pale walipo sasa. Ninachotaka ufanye ni isiwe rahisi kwako kutoa misaada hasa midogo midogo. Yaani mtu anapopata changamoto asiache kutafuta njia nyingine kwa sababu upo, bali awe ameshatafuta kila njia na imeshindikana ndiyo akaja kwako.

Kwa kufanya hivi utasaidia mambo mawili muhimu sana;
1. Utawajengea watu uwezo wa kuanza kufanyia kazi changamoto zao na kuacha kuwa tegemezi wa moja kwa moja.
2. Utapunguza mzigo wa moja kwa moja kwako, hasa changamoto ndogo ndogo ambazo watu wanaweza kutatua wenyewe.

Kitu cha tatu ni kuongeza vyanzo vyako vya mapato.
Kuwa na chanzo kimoja cha kipato, hasa ajira ni hatari kubwa sana kwenye maisha ya sasa. Zamani ilikuwa ni kitu salama kabisa, lakini kwa sasa ni hatari kubwa. Ajira zimekuwa siyo za uhakika tena na maisha yanakwenda kasi kuliko ajira inavyokwenda. Kipato cha ajira kinaongezeka taratibu wakati gharama za maisha zinaongezeka kwa kasi kubwa.

Hivyo unahitaji kutengeneza vyanzo vya ziada vya mapato. Na unaweza kutengeneza vyanzo hivyo ukiwa bado upo kwenye ajira yako. hii itakupa uhuru hasa unapokutana na changamoto. Wafanyakazi wengi huwa wanapata shida sana wanapokutana na changamoto katikati ya mwezi, kwa sababu fedha wanakuwa hawana na hivyo kuishia kwenye mikopo ambayo wanatozwa riba kubwa. Mwisho wa siku mtu anakuwa anafanyia kazi riba za mikopo, kwa sababu anapopokea mshahara anaishia kulipa mikopo yenye riba kubwa, halafu anaanza tena kukopa.

Unaweza kuwa na vyanzo nane tofauti vya mapato. Kujua jinsi ya kujitengenezea vyanzo hivi tofauti vya mapato, nunua kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA, Jinsi ya kuanza na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa. Bonyeza hayo maandishi kukipata.
Fanyia kazi haya ambayo umejifunza na utaweza kuondokana na changamoto hii ya dharura kuwa kikwazo cha kufikia malengo yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: