Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Ni imani yangu kubwa kwamba unaendelea vyema huku ukiyaendesha maisha yako kwa misingi ya falsafa tunayojifunza kila siku. Maisha bora, yenye furaha na mafanikio yanaanza na wewe mwenyewe, kwa kuishi vile ambavyo unapenda kuishi, kwa kufanya kile ambacho unaweza kukifanya vizuri.
Duniani tupo watu tofauti, pamoja na wingi wetu hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu. Na pia kuna watu wanapendelea vitu tofauti tofauti. Ndani ya jamii moja, watu wote hawawezi kufanana kwa vile wanavyopendelea kufanya.
Tofauti hizi ndizo zinazoleta tamaduni mbalimbali. Kwenye kila jamii kuna tamaduni mbalimbali ambazo zinatofautiana na watu wanavutiwa kwenye utamaduni fulani ambao unaendana na vile wanavyoamini wao.
Tatizo kubwa kwenye jamii zetu linaanzia pale utamaduni mmoja unapojiona ni bora kuliko utamaduni mwingine. Hapa ndipo mahusiano ya kijamii yanapoingia mgogoro na watu kushindwa kuelewana na hatimaye kuishia kwenye vita na mapigano.
Kama tungeweza kuelewa kwamba hakuna utamaduni ambao ni bora kuliko mwingine, bali ni tamaduni zinazotofautiana kutokana na kutofautiana kwa watu, tungeepusha mambo mengi sana. Kama tungeweza kuwaheshimu watu kwa kile wanachofanya au kuamini, bila ya kuwahukumu kwamba ni hovyo kuliko tunavyofanya sisi, tungejenga ushirikiano mkubwa kwenye jamii zetu.
Kwa kipimo chochote kile, Mchaga siyo bora kuliko Mzaramo, na wala mzaramo siyo bora kuliko mchaga, bali ni tamaduni mbili tofauti.
Kwa kipimo chochote kile, Mkristo siyo bora kuliko Mwislamu, na wala mwislamu siyo bora kuliko mkristo, hizi ni tamaduni mbili tofauti.
Kwa kipimo chochote kile, mwenye dini siyo bora kuliko asiye na dini, na wala asiye na dini siyo bora kuliko mwenye dini, bali hizi ni tamaduni mbili tofauti.
Tumekuwa tunapoteza nguvu zetu nyingi kutaka kudhibitisha kitu ambacho hatuwezi kudhibitisha, na katika kufanya hivyo tunaharibu mahusiano yetu. Kutaka kudhibitisha kwamba utamaduni mmoja ni bora kuliko utamaduni mwingine ni kupoteza nguvu kwa sababu hakuna kipimo unachoweza kutumia kudhibitisha.
Hii ni kwa sababu tamaduni tofauti zina vitu tofauti, na watu wanavutiwa kwenye tamaduni hizo kutokana na kile wanachoamini. Pale ambapo utamaduni fulani unaendana na kile wanachoamini wao, wanakuwa tayari kwenda na utamaduni huo.
Hivyo badala ya kutafuta nani bora kwa kuangalia tofauti zetu, ni vyema tukatumia nguvu hiyo kuangalia ni namna gani tamaduni mbalimbali zinavyoendana. Ni vyema tukaangalia tunaweza kushirikianaje ili kuwa na jamii bora licha ya tofauti zetu. Na hapa ndipo tunakuwa tumevuka fikra za chini na kuweza kujenga jamii bora yenye ushirikiano mkubwa.
Lakini hili ni gumu kwa namna tamaduni zetu zilivyotengenezwa. Misingi ya tamaduni nyingi ilikuwa kutengeneza ushawishi mkubwa kwa wengine na hivyo kuhitaji kujionesha kwamba ni bora zaidi ya tamaduni nyingine. Lakini sisi tunahitaji kuvuka hili.
Kwa mfano kwenye utamaduni wa dini, mwislamu atamwona mkristo ni kafiri na mkristo atamwona mwislamu ni mtu wa mataifa. Haya ni matabaka ambayo yamepitwa na wakati ambayo hayana msaada wowote kwenye jamii zetu. Wewe kama ni mwislamu na ni mgonjwa, utajikuta unatibiwa na daktari ambaye ni mkristo, wewe kumwona ni kafiri hakubadili chochote kuhsu yeye. Hivyo pia kwa mkristo, ukiwa mwanafunzi utafundishwa na mwislamu, ambaye umataifa wake haumbadilishi kwa namna yoyote ile.
Kila mtu ni bora kwa kile anachofanya, bila ya kujali anatokea kwenye utamaduni gani. Na mwisho wa siku kila utamaduni upo kwa nia njema ya kuwawezesha watu kuwa na maisha bora. Kwa mfano kwa dini, zote zina dhumuni la kuwawezesha watu kuishi kwa wema ili waweze kuingia ufalme wa mbinguni. Hivyo ni faida zaidi kama tamaduni zitashirikiana kuliko zikitaka kushindana.
Mheshimu kila mtu kwa utu wake, siyo kabila lake, dini yake, au rangi yake. Kila mtu ana mchango kwenye jamii aliyopo, kama akipewa nafasi ya kutoa mchango wake. Tuanze kwa kuthamini michango ya wenzetu, kwa kuwaheshimu walivyo na kuona namna ya kushirikiana nao. Tuweke pembeni tofauti zetu.
Hakuna utamaduni ambao ni bora kuliko mwingine, au ambao ni mbaya kuliko mwingine. Tamaduni zinatofautiana na watu wanavutiwa kwenye utamaduni unaoendana na kile wanachoamini. Kutumia nguvu kuonesha nani ni bora, hakutawafanya watu wahame utamaduni mmoja kwenda mwingine. Mtu ambaye ni mkristo hataingia kwenye uislamu kwa sababu ameambiwa uislamu ni bora kuliko ukristo, ila ataingia kama ataona unaendana na kile anachoamini.
Tujenge jamii bora yenye ushirikiano kwa kuelewa tofauti zetu ndizo zinatufanya tuchague tamaduni tofauti. Tuheshimiane kwenye hilo na tushirikiane.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Pata vitabu vya kujisomea ili kuwa na maisha ya mafanikio kwa kutembelea www.mobileuniversity.ac.tz