Mafanikio makubwa kwenye maisha yako yanaanza na uhuru wako. Huwezi kusema una mafanikio kama huna uhuru. Uhuru ndiyo utakuwezesha kufanya kile ambacho unataka kufanya kwenye maisha yako, ambacho ndiyo kinakuletea furaha na mafanikio.

Watu wengi bado wameendelea kuwa watumwa wa wengine, wameshindwa kuwa huru na hivyo kujikuta maisha yao yanaamuliwa na watu wengine. Wanaweza kuwa wanapenda sana uhuru ila hata wanapopewa hawawezi kuutumia na hivyo kujikuta wakirudi tena kwenye utumwa.

Kuna kitu kimoja kinachowafanya wengi waendelee kuwa watumwa, bila ya kufanyia kazi kitu hiki mtu hawezi kuondoka kwenye utumwa, hata kama atapewa uhuru mkubwa kiasi gani.

Kitu hiko ndiyo tunakwenda kujifunza hapa ili na wewe uweze kukifanyia kazi na kununua uhuru wa maisha yako.

Kitu kinachowafanya wengi kuendelea kuwa watumwa wa wengine ni kukosa NIDHAMU BINAFSI. Bila ya nidhamu binafsi hakuna hatua kubwa unayoweza kupiga hapa duniani kwa kuwa na uhuru wako mwenyewe. Hata unapokuwa huru utajikuta unarudi kwenye utumwa wa wengine.

Nidhamu binafsi ni pale unapoweza kufanya kile ulichopanga kufanya, kwa wakati uliopanga kufanya iwe unapenda kufanya au la. Na hii ndiyo changamoto kubwa sana, kwa sababu tunapopanga na kutekeleza ni vitu tofauti.

Kwa mfano, kama umeajiriwa utalazimika kuamka asubuhi na mapema ili uweze kuwahi kazini, iwe siku hiyo unajisikia au hujisikii. Hapa unaongozwa na nidhamu ya wengine. Sasa je unapokuwa umejiajiri unaweza kuamka asubuhi kila siku na kuwahi kwenye eneo lako la kazi hata kama hujisikii? Hapa ndipo changamoto kubwa ilipo.

Na watu walioajiriwa huwa wanajidanganya jambo moja kuhusu kujiajiri, kwamba watakuwa na uhuru wa kufanya kile wanachotaka kufanya. Wakiingia kwenye kujiajiri wanaingia na mtazamo huo na hivyo kukosa nidhamu binafsi, wanashindwa na kurudi kuajiriwa.

SOMA; Jinsi Ya Kujenga Nidhamu Binafsi.

Jijengee nidhamu binafsi, weza kujiadhibu wewe mwenyewe, jilazimishe kufanya kila ambacho unajua ni muhimu kwako kufanya, wakati mwingine unahitaji kujitesa, kutokujionea huruma ndiyo uweze kupata kile unachotaka. Hii game siyo rahisi, wengi wanapotea kwa sababu hawawezi kujitoa vya kutosha, usiwe mmoja wao.

Jijengee nidhamu binafsi, anza kwa kufanya kile ambacho umepanga kufanya, hata kama kuna sababu gani inayokushawishi usifanye, halafu endelea kwa kutekeleza kila unachoahidi, hakuna kitakachokuzuia kuwa huru na kufanikiwa. Kama nidhamu binafsi itakushinda, watu watakutumia kutimiza ndoto zao wenyewe.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)