Moja ya mahitaji muhimu ya kuweza kuishi maisha bora na yenye mafanikio, ni kuwajua watu. Binadamu tunaweza kujifunza mambo magumu sana na tukayajua, tunaweza kujifunza mashine ngumu na tukaweza kuzitumia, lakini kitu kimoja kinatushinda, kuweza kuwaelewa watu wengine.

Ni vigumu kuwaelewa watu wengine kwa sababu watu wapo tofauti, kile wanachoonesha nje siyo kilichopo ndani yao. Hivyo tunaweza kuwaelewa kwa kile tunachoona nje lakini siku wakafanya tofauti na tulivyowaelewa.

Ni muhimu kuwaelewa watu, na kama utashindwa kumwelewa mtu mmoja mmoja basi jua tabia za watu ambao unaweza kuzigundua haraka unapokutana na watu wa aina ile.

Kuna watu ambao wanafurahi pale wanapokuona una matatizo. Hawa ni watu ambao wanaona kuteseka kwako ni nafuu kwao. Labda wanaona maisha yao ni bora kuliko yao, au vyovyote vile. Watu hawa hawajiamini na hawaoni kama wanaweza kufanya makubwa kwenye maisha yao. Waelewe watu hawa na wasikusumbue, kazana kuondokana na changamoto zako.

Kuna watu ambao kila kitu wanakiangalia kwa upande hasi. Hawa ni watu ambao kitu kikitokea wanakuwa wa kwanza kutabiri kwamba mambo yatakuwa mabaya sana. Watu hawa wanaweza kukutisha na kukukatisha tamaa na hata ukashindwa kuendelea kufanya kile unachofanya. Mara nyingi watu hawa wanakuwa wamejawa hofu na wanatafuta watu wengine wa kuwajaza hofu zao. Waelewe watu hawa na usiwasikilize, wewe endelea kufanya.

Kuna watu ambao wanapambana usiku na mchana kukutoa hapo ulipo, wakati wewe unakazana kuwa bora, wao wanakazana kuharibu ubora wako. Na hivyo wanakuwa wanatafuta vitu vya kuharibu kile unachofanya. Wajue watu hawa na waepuke haraka sana, kwa sababu kadiri wanavyokuwa karibu na wewe ndivyo wanavyopata nafasi nzuri ya kukuharibia.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hivi Ndivyo Unavyowapa Watu Wengine Ruhusa Ya Kukuumiza Wewe.

Hawa ni baadhi ya watu ambao utakutana nao kwenye maisha yako, ambao hawatakuwa na nia njema na wewe. Ona dalili hizi mapema kabla hujaharibu mipango yako kwa sababu ya watu hawa. Kumbuka wewe ndiye mwamuzi wa mwisho wa maisha yako, usimpe mtu mwingine nafasi hii muhimu sana.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)