Brand ni lile jina ambalo biashara inakuwa imejijengea kwenye jamii na wateja wake. Ni ile sifa ya kipekee ambayo biashara inayo na inajulikana na wengine.

Coca Cola ni brand, unaposikia tu neno coca cola unajua ni kinywaji bora, hata kama hujawahi kunywa.

Samsung ni brand, unaposikia neno samsung unajua ni simu bora na zenye uwezo mkubwa.

Google ni brand, unaposikia google unajua kwamba unaweza kupata chochote unachotaka.

Azam ni brand, unaposikia azam unajua mambo ya chakula yanahusika.

Dar ex press ni brand, unaposikia hilo jina unajua usafiri wa uhakika unahusika.

Amka Mtanzania ni brand, Kisima Cha Maarifa ni brand, unaposikia maneno hayo unajua unapata maarifa bora ya kufikia mafanikio.

Je unawezaje kuifanya biashara yako nayo kuwa brand?

Siyo kazi ngumu, kila biashara inaweza kufanywa kuwa brand. Unachohitaji ni kujua ni kipi hasa unawapatia wateja wako, kisha kukitoa kwa utofauti na wengine wanavyotoa. Pia unahitaji kusimamia kile ambacho unakitoa, kwa maneno mengine lazima biashara yako iwe na misingi fulani.

Lazima uwe na miiko, kwamba vitu fulani huwezi kufanya. Lazima ujali ubora wa kile unachotoa hata kama mazingira yanabadilika kiasi gani, usifanye kitu ambacho kitaharibu ubora wa huduma zako.

Kwa mfano kipindi cha mwisho wa mwaka, watu wengi huwa wanasafiri na hivyo makampuni ya mabasi huwa yanaongeza nauli za mabasi yao ili kufaidika zaidi. Lakini kuna makampuni kama Dar ex press wao hawaongezi nauli kwa sababu ya msimu, nauli zao ni zile zile na huduma zao ubora ni ule ule, hii inawajenga sana wao kama brand. Kila mtu anakuwa anajua wanatoa huduma bora wakati wote.

Unahitaji pia kuwa na hadithi nzuri kuhusu biashara yako, kitu kitakachowafanya wateja wajisikie ufahari kuwa sehemu ya biashara hiyo. Wape watu nafasi ya kujivunia kupitia kile wanachokipata kupitia biashara yako, na watapeleka hadithi hii kwa wengine pia.

Unahitaji kuwa na alama za kibiashara ambazo watu wakiziona moja kwa moja wanajua ni kitu gani kinahusika. Angalia nembo za makampuni makubwa, hata kama hakuna jina, kuiona tu nembo unajua hii ni kampuni fulani. Nembo inakutofautisha na wengine, na watu wanapoona nembo ya biashara yako wanakumbuka kuhusu biashara hiyo.

Ifanye biashara yako kuwa brand, linda sifa ya biashara yako kwa kutoa huduma bora wakati wote na kusimamia kile unachoamini kupitia biashara hiyo.

Nakutakia kila la kheri katika ukuaji wa biashara yako.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

MUHIMU; Kama una swali, maoni au changamoto yoyote ya kibiashara, weka kwenye maoni hapo chini na tutajadiliana zaidi na kama itahitajika nitaandaa makala ya kuhusu jambo hilo kwenye makala zijazo.

Kwa ushauri wa moja kwa moja kuhusu biashara yako kutoka kwangu bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.