Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kuzingatia Unapoomba Na Kupokea Ushauri Wa Biashara.

Moja ya vitu ambavyo vinapatikana kwa urahisi sana kwenye jamii zetu ni ushauri. Karibu kila mtu anaweza kumshauri kila mtu kuhusu kila kitu. Hakuna kitu ambacho watu wapo tayari kutoa kama ushauri. Sema tu tatizo lako na kwa haraka sana watu wanakupa ushauri ambao kwa wao wanaona ni bora kwako kufuata. Lakini ushauri huu unaotolewa na kila mtu siyo ushauri bora kufuata kwenye kila unachofanya. Wapo watu wengi ambao wamepokea ushauri na kuutumia ukawapa matokeo mabaya kuliko yale ambayo walikuwa nayo.

Ushauri wa biashara umekuwa unatolewa kirahisi sana. Nenda popote na waulize watu ni biashara gani nzuri nifanye, kila mtu atakupa maoni yake, na watakupa mifano jinsi wengine walivyonufaika na biashara hiyo wanayokushauri. Usipofanya tathmini ya kutosha, unaweza kuingia kichwa kichwa na mwisho ukajikuta unaumia badala ya kunufaika.

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA

 
Leo tunakwenda kushirikishana mambo ya kuzingatia katika ushauri ili uweze kupata ushauri bora utakaoiwezesha biashara yako kukua zaidi.

1. Pata ushauri wa kitaalamu.
Kuwa makini na ushauri unaopokea, jiulize unatoka wapi ushauri huo. Pokea ushauri kutoka kwa watu ambao wana uzoefu na uelewa juu ya kile wanachokushauri. Hapa utapata ushauri unaoendana na uhalisia. Unapopata ushauri kutoka kwa wanaofanya, unapata kile hasa unachokwenda kukutana nacho, hapa unapewa ukweli unaoendana na kile unachotaka kujua.

Wale wasiokuwa na uzoefu au utaalamu watakuambia vitu ambavyo wao pia wamesikia. Huenda walisikia watu wanasema biashara fulani inalipa, wakaona watu watatu wanaofanya biashara hiyo na inawalipa, halafu wanakushauri na wewe. Kwa njia hii hutapata picha halisi ya kile unachokwenda kufanya. Kuwepo kwa watu wachache waliofanikiwa kwenye biashara fulani hakuifanyi biashara hiyo kuwa bora.
SOMA; USHAURI; Biashara Nzuri, Inayolipa Na Unayoweza Kuifanya.

2. Siyo kila kitu kwenye ushauri kitakufaa wewe.
Jambo jingine muhimu sana kuzingatia kwenye ushauri ni kujua kwamba siyo kila kitu kwenye ushauri kitakufaa wewe katika biashara yako. Badala yake unahitaji kuangalia ni vipi kwenye ushauri unaopata vinakufaa kwenye biashara yako. Pia angalia namna ambavyo unaweza kuboresha ushauri unaoupata uendane na biashara yako wewe. Anayekupa ushauri atakupa kulingana na uzoefu wake yeye, lakini wewe ndiye unayeijua biashara yako vizuri zaidi, hivyo jua kipi unaweza kukitumia wapi.
Ushauri siyo msaafu kwamba utumike kama ulivyo, bali unahitaji kuuchambua na kuona ni vitu gani vinaweza kwenda na hali uliyonayo wewe. Pokea ushauri na uchambue ukiangalia biashara yako na malengo yako ya kibiashara.

3. Mambo yanabadilika, kilichowezekana jana siyo lazima kiwezekane leo.
Hili ni muhimu kulizingatia kwenye ushauri unaopokea, wengine watakupa ushauri ambao ulileta matokeo mazuri siku za nyuma. Lakini kutokana na mabadiliko ambayo yametokea, ushauri huo unaweza usitoe matokeo bora kwa sasa. Unapopokea ushauri, angalia nyakati ambapo ushauri huo ulikuwa bora, kisha angalia nyakati hizi baada ya mabadiliko. Kisha angalia ni jinsi gani unaweza kuboresha ushauri huo uendane na hali ya sasa. Hata kwenye biashara yako mwenyewe, mbinu zilizokufikisha hapo ulipo sasa, siyo zitakazokupeleka mbali zaidi, ni lazima ujue mabadiliko yanayotokea yanakuhitaji wewe ubadili nini.

4. Unaweza kujishauri mwenyewe pia.
Kila kitu unachofanya kwenye biashara yako, kitumie kama sehemu ya kujifunza. Hivyo unapokutana na changamoto yoyote kwenye biashara yako, jikumbushe changamoto kama hizo ulizopitia siku za nyuma, ulichukua hatua gani na ukapata majibu gani. Hapa unaweza kurudia hatua hizo ulizochukua au kuchukua hatua tofauti na ulizochukua awali. Pia unaweza kuwaangalia wengine jinsi ambavyo wamekuwa wanafanya mambo yao, na ukajiuliza kwenye hali kama hii, mtu fulani angefanya nini? Hapa unaweza kujishauri wewe mwenyewe na kupata matokeo mazuri. Mtu huyu unayemtumia kama mfano anakuwa ni mtu anayekuhamasisha kutokana na mafanikio aliyopata kwenye kile anachofanya.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoweza kutajirika kwa kuanza na shilingi elfu moja

5. Ushauri wa bure una gharama kubwa.
Kila ushauri unaopokea unaulipia, unaweza kuchagua kulipa mwanzo na kupata ushauri bora ambao utakuepusha na hasara, au unaweza kuamua kuchukua ushauri wa bure na ukalipa wakati utakapotumia ushauri huo na kupata hasara. Ushauri wa bure una gharama kubwa kwa sababu utapata ushauri ambao siyo bora na hivyo utakapoutekeleza lazima utakutana na changamoto na kupata hasara. Hivyo usikimbilie ushauri wa bure, ni vyema ukachukua muda kuchuja kila ushauri unaoupata kabla hujaufanyia kazi.
Hakuna mtu anayeweza kufanya kila kitu mwenyewe, hakuna mtu anayeweza kujua kila kitu mwenyewe, hii ndiyo maana tunahitaji ushauri mara kwa mara ili tuweze kufanya maamuzi bora kwenye biashara zetu. Hakikisha ushauri unaoupata unaufanya uendane na biashara yako kabla hujaanza kuutumia.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako,
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kwa ushauri bonyeza maandishi haya kupata utaratibu wa ushauri. karibu sana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: