Ni tabia ya binadamu kupenda vitu vya muda mfupi, vitu vinavyoonekana haraka.

Ni sheria ya asili kwamba vitu vizuri haviji haraka, na mambo yote bora yanatokea kwa muda mrefu.

Hapa ndipo unapoanzia mkanganyiko ambao unawazuia wengi kupata kile wanachotaka. Kumbuka mara zote unapokwenda kinyume na sheria za asili, unapoteza.

Unapoangalia mambo unayopata kwa muda mfupi, unapoteza yale ambayo ungeweza kupata kwa muda mrefu. Unapofikiria kupata majibu ya haraka, unayoyaona sasa, unapoteza muda wa kutengeneza majibu bora zaidi baadaye.

Tunapenda kuona majibu ya haraka, lakini majibu haya huwa siyo bora. Tuna uvumilivu kidogo sana wa kusubiri kwa muda mrefu, lakini muda mrefu ndiyo unaoleta majibu bora.

Tunahitaji kuondokana na tabia yetu binadamu ya kutaka majibu ya haraka, ya kutaka matokeo ya muda mfupi na tuanze kufikiria matokeo ya muda mrefu.

Kwa mfano kama chanzo chako pekee cha kipato ni ajira, kwa muda mfupi mambo yatakwenda vizuri, hasa kama kipato chako ni kikubwa. Lakini unajua ajira inakutegemea wewe uwepo moja kwa moja kwenye ajira, inapotokea haupo tena, matatizo ndiyo yanaanza. Hivyo hapa unahitaji kufikiria muda mrefu kifedha, uwe na uwekezaji ambao kwa muda mrefu utakupa uhuru wa kifedha. Inawezekana uwekezaji huo usiwe na faida ndani ya muda mfupi, lakini kwa muda mrefu ukakunufaisha sana.

SOMA; BIASHARA LEO; Sababu Ya Mteja Wako Kwenda Kwa Mshindani Wako.

Kwenye biashara hili ndiyo liko wazi kuliko maeneo mengine yoyote, unaweza ukamdanganya mteja leo ukapata faida ya haraka. Lakini ataujua ukweli, hatanunua tena kwako, na mbaya zaidi atamwambia kila anayemjua asinunue kwako. Utapata faida ndogo ya muda mfupi, lakini utapoteza faida kubwa ya muda mrefu.

Hata kwenye afya, afya njema na imara inajengwa kwa muda mrefu, kwa kufanya maamuzi sahihi kiafya kila siku kuhusu vyakula, mazoezi na kupumzika. Kuna njia za haraka kama dawa, lakini hizi haziji bila ya madhara.

Usiishie kuangalia matokeo ya haraka, usiishie kufikiria kwa muda mfupi. Angalia muda mrefu, huko ndipo penye matokeo bora zaidi kwako.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)