Kama ulichofanya jana kinaonekana kikubwa kuliko ulichofanya leo, basi leo hujafanya kitu kikubwa. Na tunaweza kusema bila ya shaka kwamba leo hujafanya chochote, kama lengo lako ni kuwa na mafanikio kwenye maisha.
Kama umekuwa unawaambia watu na kujiambia mwenyewe kwamba enzi zako ulikuwa unafanya makubwa, basi unadhihirisha kwamba sasa hivi hakuna unachofanya, zaidi ya kuongea.
Kufanikiwa siyo mwisho wa safari, bali ndiyo safari yenyewe. Hivyo kila siku unahitaji kufanikiwa, ndiyo maana ni muhimu kuboresha kile unachofanya KILA SIKU. Uifanye leo kama ulivyofanya jana, bali leo fanya kwa ubora zaidi ya ulivyofanya jana. Kwa njia hii hutakaa chini na kusifia vya jana, bali utakuwa na vya leo ambavyo vitakuwa bora sana kwako.
Ni marufuku ifike siku uanze kufikiri au kusema kwamba wakati wangu umepita, kama bado upo hai, wakati wako haujapita, kadiri maisha yako yanavyobadilika, nawe unahitaji kubadilika ili kuhakikisha kila siku yako ni siku ya mafanikio.
Kama ambavyo tumekuwa tunashirikishana mara nyingi, hakuna siku moja utakayoyafikia mafanikio yote unayoyataka, bali mafanikio ni mkusanyiko wa siku ulizoziishi vizuri kwenye maisha yako.
Je leo unakwenda kufanya kipi ambacho kitaifanya siku ya leo iwe bora kuliko ya jana? Hili ni swali la kujiuliza kila unapoianza siku mpya, na kulifanyia kazi kwenye siku yako. Hata kama unabadili kitu kidogo sana, siyo sawa na kufanya kwa mazoea.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)