Mtazamo unaohitaji ili kufanikiwa kwenye biashara yako.

Kama kuna kitu ambacho kinapatikana kila mahali kwa sasa ni mafunzo na ushauri kuhusu ujasiriamali. Mambo haya ya ujasiriamali yamekuwa maarufu kwenye zama hizi kutokana na ugumu wa kupatikana kwa ajira na ugumu wa ajira zenyewe kwa wale wachache wanaozipata. Sasa hivi watu wengi wanapanga au tayari wameshaingia kwenye ujasiriamali.
 

KUPATA KITABU HIKI BONYEZA MAANDISHI HAYA.


Kitu kimoja muhimu sana ambacho watu wengi hawakijui ni kwamba ujasiriamali siyo rahisi kama ambavyo watu wanafikiri kabla ya kuingia, au wanavyofundishwa. Ujasiriamali una changamoto zake na wengi wanaoingia kwenye ujasiriamali wanashindwa. Tafiti zilizofanywa kwenye nchi zinazoendelea zinaonesha kwamba kati ya biashara kumi zinazoanzishwa kila mwaka, biashara nane zinakuwa zimeshakufa inapofikia mwaka mmoja na nusu tangu kuanza kwa biashara hizo.
Kama wewe umeshaingia kwenye ujasiriamali au biashara, au ndiyo unapanga kuingia kuna mtazamo ambao unahitaji kuwa nao ili kuweza kuendesha biashara yenye mafanikio. Kwa kuwa na mtazamo huu sahihi utaepuka kujidanganya na kudanganywa na wengine na kuweza kufanya maamuzi sahihi kwenye biashara yako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Business @ The Speed Of Thought. (Mbinu Za Kufanya Biashara Kwenye Zama Hizi Za Taarifa).

Mtazamo muhimu unaopaswa kuwa nao ni kuviona vitu katika uhalisia wake. Mara nyingi hatuoni uhalisia wa vitu, bali tunaona kile ambacho tunataka kuona au tunatarajia kuona. Namna hii ya kuangalia vitu inatukosesha fursa kubwa iliyopo kwenye vitu hivyo. Badala yake unafanya vitu kwa mazoea na hivyo kujiweka katika hatari ya biashara yako kufa pale mabadiliko yanapotokea. Mabadiliko yanatokea kila siku, hivyo ni muhimu kuwa umejiandaa kila siku.

Yafuatayo ni mambo muhimu kuzingatia ili kujijengea mtazamo wa kuiona biashara katika uhalisia wake.

Hakuna biashara ambayo ni rahisi kufanya.
Watu wengi wamekuwa wakikazana kutafuta biashara ambayo ni rahisi kufanya na itakayowaletea mafanikio ya haraka. Ukweli ni kwamba hakuna biashara ambayo ni rahisi kufanya au itakayokufikisha kwenye mafanikio ya haraka. Kila biashara ina ugumu wake, na huwezi kuujua ugumu huo mpaka pale utakapoingia kwenye biashara hiyo na kuifanya. Hivyo kigezo cha kuchagua biashara ya kufanya hakipaswi kuwa urahisi wa biashara, bali mapenzi na ile aina ya biashara unayofanya. Unapokuwa unapenda kile unachofanya, ugumu hauwezi kukuzuia kufanikiwa.

Kila biashara ina changamoto zake.
Sehemu kubwa ua ugumu wa biashara inatokana changamoto ambazo kila biashara inapitia. Katika nyakati hizi za changamoto ndipo biashara zinazofanikiwa na zinazoshindwa zinapotofautiana. Kila biashara inapitia changamoto mbalimbali. Changamoto hizi zinaweza kuwa kubwa au ndogo lakini zinakuwa na madhara kwenye biashara. Wafanyabiashara ambao wanafanikiwa, wanatarajia kukutana na changamoto hizi na wanajua wakizitatua wanapata mbinu bora zaidi za kibiashara. Wafanyabiashara wanaoshindwa hawategemei kukutana na changamoto, wanaona mambo yote yataenda kama walivyopangwa. Wanapokutana na changamoto wanakuwa hawajajiandaa na hivyo kukata tamaa haraka.

SOMA; Tabia Nne(4) zinazowatofautisha wafanyabiashara wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Mabadiliko yanatokea kila siku, unahitaji kwenda na mabadiliko.
Moja ya vitu vinavyopelekea biashara nyingi kufa ni kuendeshwa kwa mazoea. Inafika wakati mfanyabiashara anafanya mambo kama kawaida, kama ambavyo amezoea kufanya wakati wote. Pale mfanyabiashara anapofanya kitu fulani kikampa matokeo mazuri, basi kila wakati anaendelea kutumia njia ile iliyompa matokeo mazuri. Njia hii inaweza kufanya vizuri kwa kipindi fulani, ila inahitaji kuboreshwa kadiri siku zinavyokwenda. Kuna mambo mengi ambayo yanabadilika kwenye biashara kila siku, unahitaji kuwa karibu na biashara yako, na kuifuatilia kwa umakini ili kuyaona mabadiliko haya mapema na kuchukua hatua.

Biashara inahitaji muda ili kukua na kufanikiwa.
Kitu kingine ambacho kinazuia biashara nyingi kukua ni ile haraka ambayo watu wanakuwa nayo kwenye matokeo ya biashara hiyo. Watu wanataka kuanzisha biashara leo halafu baada ya miezi michache wawe matajiri wakubwa kupitia biashara zao. Mawazo kama haya yanawapa hamasa mwanzoni, ila pale wanapokutana na changamoto na mafanikio kuchelewa wanakata tamaa na kuona biashara waliyochagua haiwafai. Tatizo halipo kwenye biashara, kwa sababu biashara yoyote ile kuna watu ambao wanaifanya na wanafanikiwa. Tatizo lipo kwenye ule mtazamo ambao mfanyabiashara anakuwa nao kwenye biashara yake. Anapofikiria ni sehemu ya kufanikiwa haraka, anajiweka kwenye nafasi ya kukata tamaa haraka.

SOMA; Wazo Bora Na Mtaji Pekee Havitoshi Kuifanya Biashara Ifanikiwe, Unahitaji Kitu Hiki Kimoja Muhimu Sana Kwa Mafanikio Ya Biashara Yako.

Kila kitu kwenye maisha yetu kinaanzia kwenye mtazamo wetu, hivyo ndivyo ilivyo pia kwenye biashara na ujasiriamali. Wale wenye mtizamo sahihi wanaweza kuanzisha na kukuza biashara zao bila ya kujali wanapitia kipindi gani. Ila wale wenye mtizamo ambao siyo sahihi, wamekuwa wanashindwa kwenye biashara hata kama kila kitu kinakwenda vizuri. Anza kujijengea mtazamo sahihi kwenye biashara yako na utavuna matunda sahihi.

TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: