Hekima ni uwezo wa kufikiri na kutenda kwa kutumia ujuzi, uzoefu, uelewa na ufahamu ili kupata matokeo bora kwako mwenyewe na kwa wengine pia.
Hekima inahusisha kuwa na ujuzi au uelewa wa jambo, kutumia uzoefu ambao mtu unao kwenye jambo hilo na kisha kufanya maamuzi ambayo ni bora.
Hekima ni kitu ambacho kinajengwa, kwa mtu kujielimisha na kupata taarifa za kutosha kuhusiana na kile anachofanya kwenye maisha, kujifunza kupitia kila anachofanya na hata kupitia wengine na kisha kutumia mazingira aliyopo kufanya maamuzi ambayo ni bora kwa wakati husika.
Wanafalsafa wote waliowahi kuishi, walikuwa wakichukulia HEKIMA kama kiwango cha juu kabisa cha maisha ambacho mtu anaweza kufikia. Na kwa kufikia kiwango hiki mtu anakuwa na maisha bora na yenye furaha, bila ya kujali ameanzia wapi au anamiliki nini.
Kama ambavyo tunajua, maisha yana changamoto nyingi, na hakuna changamoto zinazofanana, hata baada ya kutatua changamoto moja, inapokuja nyingine, bado unahitaji kufanya maamuzi yanayoendana na changamoto ile. Katika hali kama hizi ni hekima pekee inayoweza kumsaidia mtu kufanya maamuzi bora na kuondoka kwenye changamoto hiyo aliyopo.
Mara nyingi watu wamekuwa wakitumia neno busara kumaanisha hekima, ni maneno ambayo yanaweza kumaanisha kitu kimoja.
Hekima ndiyo inawatofautisha watu katika maamuzi wanayofanya, kwenye hali moja watu wawili wanaweza kufanya maamuzi kwa taarifa walizonazo, mmoja akafanya maamuzi yanayofanikiwa huku mwingine maamuzi yake yakishindwa.
Unapokuwa na hekima unakuwa na uhuru mkubwa kwenye maisha yako, unaweza kupambana na kila changamoto na kila siku kwako ni siku mpya ya kujifunza na kufanya yaliyo bora.
Je unaweza kujijengea hekima?
Swali ambalo wengi wamekuwa wanauliza ni je hekima mtu anazaliwa nayo au mtu yeyote anaweza kujijengea? Jibu ni kwamba mtu yeyote anaweza kujijengea hekima, japo kuna tofauti kutokana na malezi ambayo mtu amepata. Kuna watu ambao wamepata malezi bora na hivyo kuwa na misingi mizuri ya hekima. Na kuna wale ambao wamepata malezi mabovu na hivyo kukosa kabisa misingi ya hekima na busara. Lakini jambo zuri ni kwamba yeyote anayetaka kujijengea hekima kwenye maisha yake, anaweza kufanya hivyo.
Jinsi ya kujijengea hekima.
Hizi hapa ni njia kumi za kujijengea hekima kwenye maisha yako.
- Jijue wewe mwenyewe. Hii ni hatua muhimu sana ya kujijengea busara kwenye maisha yako. jua ni maeneo gani ambayo una nguvu na maeneo yapi ambayo una udhaifu. Jua ni mambo gani unayafanya vizuri na mchango gani unaoweza kutoa kwa wengine. Unapojijua wewe mwenyewe, inakuwa rahisi kujisimamia na kujijengea nidhamu.
- Zijue tabia halisi za watu. Hekima haitaki unafiki, mara nyingi tunawaangalia watu kwa nje na juu juu lakini hatuendi ndani na kujua tabia halisi za watu. Jua kwamba kila mtu anafanya kitu kwa sababu kuna msukumo uko ndani yake, kwa kuelewa hili utaweza kutatua matatizo na changamoto nyingi, pia utaweza kuwahamasisha watu kuchukua hatua. Kwa kawaida binadamu ni wabinafsi, wenye wivu, wanaopenda kupokea zaidi ya kutoa, wanaotaka kila kitu kianze na wao kwanza, wavivu, wanaopenda mteremko na tabia nyingine ambazo wengi hawapendi kuzizungumzia wazi. Lakini pia watu wanapenda kusifiwa, wanapenda kuonekana ni wa muhimu, na wanapenda kuwa na mchango fulani kwenye kila wanachofanya. Kwa kujua na kuchunguza tabia hizi za watu kwenye kila kitu wanachofanya watu, utaona wazi namna ya kutatua changamoto yoyote.
- Jifunze sana, soma sana. Jifunze kupitia wengine, jifunze kupitia wewe mwenyewe. Soma vitabu, soma maisha ya watu ambao kwa viwango vyako unaona wamefanikiwa sana. Soma falsafa ambazo zimedumu kwa miaka mingi, hizi zina kitu ambacho kimekuwa kinawasaidia wengi.
- Uliza sana maswali, hoji kila kitu, usikubaliane na vitu kwa urahisi tu, usichukulie vitu juu juu, uliza maswali. Usiogope kuchekwa kwamba utaonekana hujui, utajua zaidi na kuweza kufanya maamuzi bora. Jihoji wewe mwenyewe kwenye kila hatua unayochukua kwenye maisha yako, jiulize kama ungechukua hatua mbadala matokeo yangekuwaje.
- Kuwa mtu wa vitendo, kila unachojifunza kitumie, angalia ni kwa namna gani unaweza kutumia yale ambayo unajifunza kwenye maisha yako. sehemu muhimu ya HEKIMA ni uzoefu, na uzoefu unaupata siyo kwa kusoma bali kwa kufanya. Fanya na tumia uzoefu wako kujifunza zaidi. Pia angalia wengine wanavyofanya na jifunze zaidi.
- Kubali kwamba huwezi kujua kila kitu. Huu ndiyo msingi wa wanafalsafa wengi, walikuwa wapo tayari kujifunza mara zote na kutoka kwa yeyote. Pale tu unapoanza kufikiria kwamba unajua kila kitu, ndipo unapoanza kupotea na unapoteza hekima. Socrates, mmoja wa wanafalsafa wakubwa sana kuwahi kutokea aliwahi kutoa kauli hii; NAJUA KITU KIMOJA KWA HAKIKA, SIJUI CHOCHOTE. Fikiria mtu kama Socrates aliyekuwa anafundisha falsafa alikiri kwamba hajui chochote, hii ilikuwa inampa hamasa ya kujifunza kila siku. hivyo na wewe kubali hujui chochote na kuwa tayari kufundishika, hata kama umri wako umekwenda kiasi gani, kuna mengi ya kujifunza hata kwa watoto wadogo.
- Kuwa na washauri, kwa kiingereza MENTORS, hawa ni watu ambao wanakuongoza kwenye maisha na kile unachofanya. Unaweza kuwa na mentor wa moja kwa moja ambaye mnakutana na anakushauri na kukuelekeza. Ila pia unaweza kuwa na mentor ambaye siyo wa moja kwa moja, yaani unajifunza kupitia yeye ila hamkutani, au hata wakati mwingine hayupo hai. Vitabu via vinaweza kuwa mamentor wazuri sana. Mmoja wa mamentor wangu amewahi kuandika vitabu 100 ni sawa na mentor mmoja, hivyo unahitaji kusoma vingi.
- Kuwa na falsafa yako ya maisha, kuwa na kitu ambacho unasimamia kwenye maisha. Hapa unahitaji kuwa na falsafa inayoendana na kile unachoamini kwenye maisha, na chochote unachofanya kwenye maisha yako, usiende kinyume na falsafa yako hiyo. Kuwa na miiko kwenye maisha yako, jikataze vitu fulani ambavyo umekuwa unapenda kufanya lakini vinakuletea matatizo. Moja ya mahitaji ya kuwa na hekima ni kuweza kudhibiti hisia zako na kujijengea nidhamu binafsi. kama huna nidhamu binafsi, huwezi kuwa na busara.
- Kuwa tayari kuwasaidia wengine, kila unachofanya, hakikisha kina maada kwa wengine, na kama hata hakina msaada basi kisiwaumize. Unapokuwa na hekima unahitaji kuishi kwenye dunia ambayo haiwezekani, wengi husema ideal au UTOPIA, hii ina maana kwamba unajihukumu kwa kila unachofanya, na njia nzuri ya kujihukumu ni kutumia sheria ya dhahabu, GOLDEN RULE, ambayo inasema kwamba WAFANYIE WENGINE KILE AMBACHO UNGEPENDA NA WAO WAKUFANYIE WEWE. Njia nyingine ya kujihukumu ni kujiuliza je ikiwa kila mtu duniani angefanya kile ambacho mimi nafanya dunia ingekuwa sehemu salama ya kuishi? Maswali hata yatakufanya ujali maisha ya wengine.
- Kuwa mnyenyekevu. Hakuna kitu kinaharibu watu kama mafanikio madogo, wengi wanapoanza wanakuwa wanyenyekevu, ila wanapopata mafanikio madogo huanza kujioa wao ni wajanja sana na wengine ni wajinga. Hujitamba na kujionesha kwa kile ambacho wamefanikiwa kufanya. Hii siyo njia ya busara na hekima. Hekima ni kuwa mnyenyekevu, hata kama una fedha na madaraka kiasi gani, hata kama una mafanikio makubwa kiasi gani, usijitape mbele ya wengine, usiwadharau wengine ambao hawajaweza kupata kile ambacho wewe umepata. Na muhimu zaidi, wewe kupata haimaanishi una akili kuwazidi waliokosa, mara zote kuwa mtu wa shukrani na kuwa mnyenyekevu. Jua mwisho wa siku maisha yako hayatapimwa kwa ulichomiliki bali kwa namna ulivyogusa maisha ya wengine.
- Nyongeza; usikimbilie kuhukumu. Nilikuambia nitakupa mambo kumi, siyo kwamba yapo kumi, yapo mengi sana, lakini nimechagua yale kumi muhimu ya kuanza nayo. Mengine tutaendelea kujifunza kadiri tunavyokwenda, yapo mengi sana. Hili moja nilitaka kulisahau, na ni muhimu sana sana, usikimbilie kuhukumu. Tunaishi kwenye jamii ambazo kabla hujamaliza hata kueleza matatizo yako tayari watu wana majibu, kila mtu ni mshauri na kila mtu anaweza kutoa maoni yake kwenye kila jambo linalotokea. Mtu anaweza kusikia kitu kutoka kwa mtu mwingine ambaye naye alisikia na tayari akahukumu. Kuwa na hekima unatakiwa kuepuka kukimbilia kuhukumu, badala yake jifunze kusikiliza zaidi, sikiliza kila upande, hoji zaidi na unganisha matukio. Mwisho ndiyo uweze kufanya maamuzi kipi ni kipi. Kwa mfano unaweza kuona habari mtu kabakwa, haraka haraka utasema wanaume washenzi sana, ona huyu kambaka mwenzake. Lakini hapo umepata taarifa ya upande mmoja tu, hujui upande wa pili kuna nini. Huenda huyo anayesemekana kabaka ana ugonjwa, au huenda ni watu wanaojuana na mwanamke ameamua kumkomoa mwanaume baada ya kushindwa kuelewana, au huenda huyu mwanamke amekuwa akila hela za mwanaume na kumdanganya siku moja watafanya mapenzi, lakini kila siku anamkwepa, siku hiyo mwanaume kapata upenyo na akaona lazima autumie. Huu ni mfano tu lakini unakisi mengi ambayo yanaendelea kabla jambo halijatokea.
Anza na haya 11, yafanyie kazi na tuendelee kujifunza kwa pamoja. Yapo mengi ya kujijengea HEKIMA, tutaendelea kujifunza mengi kadiri tunavyokwenda.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.