Waswahili wanasema, ongea na watu, upate viatu. Wataka ya watu na huna viatu? Huu ni usemi ambao umebeba ukweli mkubwa sana kwenye maisha yetu ya kila siku kwenye kazi, biashara na mafanikio kwa ujumla.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, utakipata kutoka kwa wengine. Iwe unafanya biashara, wateja wako ni watu wengine, iwe umeajiriwa, bosi wako, wafanyakazi wenzako ni watu muhimu kwako kufikia malengo yako. na hata kwenye familia, ndugu zako, mwenza wako, watoto ni watu muhimu kwenye maisha yako.

Ili kufanikiwa lazima uwajue vizuri wale watu wanaokuzunguka na wanaohusika na kile unachofanya au maisha yako. Na njia ya uhakika ya kuwajua vizuri ni kuongea nao.

Ongea na watu upate viatu;

Kadiri unavyoongea na wateja wa biashara yako ndivyo unavyoyajua mahitaji yao halisi na hivyo kuweza kuboresha biashara yako.

Kadiri unavyoongea na bosi wako na wafanyakazi wenzako ndivyo unavyojua kile hasa kilichopo ndani yao, kinachowasukuma kufanya maamuzi yao na changamoto wanazokutana nazo.

Kadiri unavyoongea na watu wako wa karibu, ndivyo unavyowajua vizuri, kujua changamoto wanazopitia, hofu zao na hata mipango yao ya maisha.

Kwa kujua haya kuhusu wengine kunakuwezesha kujua namna bora ya kushirikiana nao ili kuboresha maisha yao na ya kwako pia.

SOMA; VITU 100 AMBAVYO KILA MJASIRIAMALI ANATAKIWA KUJUA NA KUFANYA ILI KUFANIKISHA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.

Unawezaje kuonea na watu?

Changamoto kubwa kwenye dunia ya sasa ni kuongea na watu. Teknolojia imekua kiasi kwamba watu wawili wanaweza kukaa mahali pamoja zaidi ya saa moja na wasipate muda wa kuongea, kila mtu anakuwa amemezwa na simu yake.

Ili kuweza kuongea na watu, kwanza weka simu yako pembeni na mawazo yako yote yawe kwenye hayo mazungumzo. Waulize maswali, taka kujua ziadi kuhusu wao, wapongeze kwa hatua wanazopiga hata kama ni ndogo. Watu wanapenda sana kuongelea mambo yao, unapowasikiliza wanajisikia wa kipekee sana, na watakupa taarifa nyingi sana unazohitaji.

Ongea na watu upate viatu, usitake ya watu kama huna viatu.

Anza leo kuongea na watu, iwe unawajua au la, anzisha maongezi popote unapokuwepo, na utashangaa jinsi unavyoweza kutengeneza mahusiano bora na wengine.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)