Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha, ambapo tunashirikishana maarifa muhimu ya kujenga maisha yenye furaha na mafanikio makubwa.

Leo tutakwenda kuangalia kuhusu MAISHA YENYE MAANA, ikiwa ni swali ambalo nililizwa na mmoja wa rafiki na msomaji mwenzetu. Yeye alitaka kujua nini hasa ya maisha yenye maana kama ambavyo nimekuwa natumia neno hilo kwenye makala mbalimbali ninazoandika.

Kuna vitu viwili vikubwa ambavyo tunavipigania kwenye maisha yetu, FURAHA NA MAANA, furaha tumekuwa tunajadili mara kwa mara, lakini maana hatujapata nafasi kubwa ya kujadili. Hivyo leo tutaanza kujadili MAANA na kadiri tunavyopata nafasi tutaendelea kushirikishana kuhusu maana ya maisha ili tuweze kuwa na maisha bora.

Mwanzoni watu walikuwa wakifikiri kwamba MAISHA YENYE FURAHA NA MAISHA YENYE MAANA NI KITU KIMOJA, lakini baada ya kufanyika kwa tafiti nyingi za kisaikolojia, majibu yanaonesha kwamba furaha na maana haviendi pamoja wakati wote. Kuna baadhi ya vitu vinatupa furaha lakini havitupi maana. Kwa mfano kupokea zawadi kunaleta furaha, lakini hakuleti maana kubwa. Ila kutoa zawadi kunaleta maana kubwa kuliko furaha. Kuweka juhudi kubwa, na kujitoa kufanya kazi kupita kiwango, kunaweza kusilete furaha kwa wakati huo, lakini kunakuletea maana kubwa ya kile unachokifanya.

Nini maana ya MAISHA YENYE MAANA?

Maisha yenye maana ni yale maisha ambayo yanaendana na wewe, kwa kile ambacho unapenda kufanya na kile ambacho unakithamini. Kila mmoja wetu ni wa tofauti, na hivyo tuna uwezo tofauti, vipaji tofauti na pia tunathamini vitu tofauti. Maisha yenye maana ni yale maisha ambayo yanaendana na sisi, kwa kuweza kutumia uwezo wetu na vipaji vyetu, na kuvithamini vile ambavyo vina maana kwetu.

Maisha yenye maana ni yale yanayotutofautisha sisi na wengine, na kutuwezesha kutoa mchango mkubwa kwa wale ambao wanatuzunguka kupitia kile ambacho tunakifanya.

Inakuwa changamoto kubwa kuweza kuishi maisha yenye maana kwa sababu jamii inatuchukulia wote kama tunafanana kwa kila kitu, na hivyo kusisitizwa tuwe sawa kwenye kila kitu. Kwa mfano kumekuwa na ile dhana kwamba kila mtoto anayezaliwa anatakiwa kwenda shule, kusoma na kufaulu ili apate kazi ambayo ataifanya kwenye maisha yake, ataoa au kuolewa na kisha kuzaa na kulea watoto ili nao warudie mzunguko huo huo.

Wakati mtu anaanza safari hii hawezi kuona kasoro, yeye atakazana kusoma ili afaulu, atatafuta kazi nzuri na huenda akaipata na ataanza maisha ya familia. Lakini kadiri maisha yanavyokwenda, na changamoto za maisha anazokutana nazo ndiyo anaanza kuyafikiria maisha zaidi na kuona kuna kitu kinakosekana.

Zile ahadi ambazo alipewa kwamba kwa kuwa na elimu na kazi nzuri basi maisha yatakuwa bora anaona hazitimii kwa sababu maisha hayakosi changamoto. Hapa ndipo mtu anapoanza kutafuta maana ya maisha yake, ili angalau aone changamoto anazopitia siyo bure tu bali kuna mchango mkubwa anaotoa kwake na kwa wanaomzunguka.

Hali hii huwa inawasumbua wengi hasa wanapofikia utu uzima na kuona kuna kitu ambacho kinakosekana kwenye maisha yao.

Je unawezaje kuishi MAISHA YENYE MAANA?

Maisha yenye maana ndiyo unatakiwa kuwa msingi wa kwanza kabisa kwenye maisha yetu. Kwa sababu kwa kujua maana ya maisha yetu kutatuwezesha kuzivuka changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yetu ya kila siku bila ya kukata tamaa. Kama huoni maana ya kile unachofanya kwenye maisha yako, ni rahisi sana kukata tamaa pale unapokutana na changamoto, na kitu kimoja ambacho tuna uhakika nacho ni kwamba lazima utakutana na changamoto.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili kuwa na maisha yenye maana.

  1. Jua uwezo mkubwa ulipo ndani yako, pamoja na vipaji ulivyonavyo.

Kitu kimoja ambacho hatufundishwi kwenye jamii zetu na hata kwenye mfumo wa elimu ni ule uwezo mkubwa ambao upo ndani ya kila mmoja wetu. Tumekuwa tunalinganishwa na wengine na hivyo kujiona ni bora au hovyo ukilinganisha na wengine. Hatupati nafasi ya kujua kwamba tuna uwezo mkubwa zaidi ya tunaotumia kwa sasa.

Pia ni muhimu ujue vipaji vyako, jua ni vitu gani unavyopendelea kwenye maisha yako. Ukishavijua yajenge maisha yako kulingana na uwezo ulionao na vipaji ulivyonavyo. Kwa kuwa kufanya vitu vinavyoendana na vipaji vyako kunaleta maana ya maisha yako, basi geuza vipaji vyako kuwa sehemu ya kazi au biashara yako. kwa njia hii utahamasika kuweka juhudi hata pale unapokutana na changamoto. Wakati wengine wanaona kitu ni mzigo, wewe ndiyo unafurahia kwa sababu ni kitu unachopenda kufanya.

  1. Jua ni vitu gani unathamini kwenye maisha yako.

Kila mmoja wetu kuna vitu ambavyo anathamini kwenye maisha, kuna maadili ambayo amejijengea kwenye maisha yake. Ni kupitia maadili haya mtu anaendesha maisha yake kwa namna ambavyo atasimamia kile ambacho anakiamini na kukithamini. Wanafalsafa wanasema kama huwezi kusimama kwa chochote, basi utaangushwa na chochote. Unapokuwa na kitu unachosimamia kwenye maisha, maisha yako yatakuwa na maana. Kwa sababu kuna vitu ambavyo utavifanya mara zote na kuna vitu ambavyo vitakuwa mwiko kwako kufanya.

  1. Jua kusudi la maisha yako.

Ni kitu gani ambacho unataka watu wakukumbuke nacho siku ambayo hutakuwa hapa duniani? Ni kitu gani ambacho unapata msukumo wa kukifanya kwenye maisha yako, ambacho unajua kitawanufaisha wengine pia. Hili ni swali ambalo litakuwezesha kujenga maisha yenye maana.

Ni muhimu kujua kusudi la maisha yako, ambalo litakupa sababu ya kuamka kila siku na kwenda kuweka juhudi, hata kama kwa sasa huoni matokeo uliyokuwa unategemea. Juhudi unazoweka zinakuwa na maana kwako kwa sababu zinaendana na kusudi la maisha yako.

  1. Kuwa tayari kusimama mwenyewe.

Ili kuishi maisha yenye maana, kwanza unahitaji kujitenga na kundi kubwa la watu, ambao wanafanya vitu kwa sababu kila mtu anafanya. Hivi ndivyo jamii inavyokwenda, watu wanafanya vitu siyo kwa sababu ni muhimu kwao, au kwa sababu vina maana kwao ila kwa sababu kila mtu anafanya, au wanategemewa kufanya.

Kwa mfano wapo watu ambao wanakunywa pombe, siyo kwa sababu pombe ina maana yoyote kwenye maisha yao, bali kwa sababu marafiki zao wanatumia pombe na hivyo wanatumia ili wawe pamoja na marafiki zao. Wengine wanafanya kazi au biashara kwa sababu wanataka kuonekana na wengine wanafanya hivyo. Maisha haya kwa nje yanaweza kuonekana mazuri, ila kwa ndani ni maisha yenye utupu. Mtu anapotoka kwenye kundi hilo la watu na kuwa mwenyewe ndiyo anaona jinsi maisha yake yalivyo na utupu na kukosa maana.

Kujenga maisha yenye maana, jua ni mambo gani muhimu kwako kulingana na vipaji vyako na kusudi la maisha yako. Na vifanye vitu hivyo hata kama wengine hawafanyi au wanakupinga. Utakapopata yale matokeo unayotaka, maisha yako yatakuwa bora kuliko ungefuata kundi.

  1. Wajali watu kuliko vitu.

Tunatakiwa kuwajali watu na kutumia vitu, lakini zama hizi tunajali vitu na kutumia watu, hili limekuwa kikwazo katika kutengeneza maisha yenye maana. Ili kuona maana ya maisha yako, ni lazima uone ni kwa namna gani umegusa maisha ya wengine, angalia ni namna gani maisha ya wengine yanakuwa bora kupitia wewe. Hili linaleta ridhiko kubwa sana kwenye maisha yetu.

Huwa nasema siku utakayoondoka hapa duniani, watu hawatakumbuka ulikuwa na nyumba ngapi au magari mangapi, bali watakumbuka yale ambayo umefanya kwenye maisha yao. Kama umewahi kuhudhuria msiba na watu wakawa wanasoma wasifu wa marehemu, hutasikia hata siku moja watu wakisema alikuwa na magari haya, alikuwa na mshahara huu. Lakini watu watasema yale ambayo marehemu amefanya kwenye maisha yao. Wajali watu, na fanya yale ambayo yanafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwenye maisha ya wengine.

Hatuishi ili siku tukifa tusifiwe, ila katika kuishi maisha yenye maana, tunaacha alama kubwa tukiwa hai na hata pale tunapoondoka duniani.

Maisha yenye maana yanaanza na sisi wenyewe, kwa kujua ni vitu gani ambavyo ni muhimu kwetu ambavyo vinaendana na uwezo wetu, vipaji vyetu na maadili yetu. Kisha kutumia vitu hivyo kufanya maisha yetu na ya wale wanaotuzunguka kuwa bora zaidi.

Nina imani kuna kitu umeongeza kwenye falsafa yako mpya ya maisha, kifanyie kazi katika kujenga maisha bora.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)