Unapokuwa barabarani iwe unatembea kwa miguu au unaendesha gari, utafika sehemu ya barabara ambayo imepinda. Hakuna barabara ambayo imenyooka moja kwa moja, hivyo unapofika kwenye sehemu iliyopinda unachofanya ni kukata kona, ili kuendelea kuifuata barabara itakayokufikisha kwenye safari yako.
Kama utafika kwenye kona halafu ukakataa kukata kona kwa sababu unataka njia iwe imenyooka tu, utaondoka kabisa kwenye njia hiyo au utakuwa ndiyo mwisho wa safari yako. Huenda unajiuliza hili lina maana gani kwenye maisha yako, nataka nikuambie lina maana kubwa sana.
Malengo na mipango uliyojiwekea kwenye maisha yako, siyo yote itakwenda kama ulivyopanga, kwa kiasi kikubwa sana mambo hayataenda kama ulivyopanga. Hivi ndiyo kona za maisha yetu. Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni ile hatua wanayochukua wanapofika kwenye kona hizi.
Wapo ambao wanaona ndiyo mwisho wa safari, mambo hayawezekani tena, kwa sababu wamefanya kila wanachoweza lakini hawapati matokeo mazuri. Wanakataa kukata kona na safari inaishia hapo au wanatoka kabisa kwenye njia na kupotea.
MUHIMU KUSOMA; Hii Ndio Changamoto Kubwa Ya Zama Hizi.
Wapo ambao wakifika kwenye kona wanajua wanatakiwa kukata kona ili kuendelea na safari, hawa ni wale ambao mambo yanapokwenda tofauti na walivyopanga wanakaa chini na kujiuliza ni kipi kimesababisha mambo yaende tofauti, wanabadili mipango yao na kuboresha zaidi kisha wanaendelea na safari. Wanajua kona zipo na hivyo wanakata kona hizi ili kufika mwisho wa safari zao.
Je wewe umekuwa unafanya nini unapofika kwenye kona za maisha yako? umekuwa unakata kona hizo au umekuwa unaishia hapo na kuona ndiyo mwisho wa safari? Jiulize swali hili leo na fanya marekebisho ili usiwe kikwazo chako mwenyewe kwenye kufikia mafanikio.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)