Watu ulionao karibu kwenye maisha yako, wale ambao wanakuzunguka na unatumia muda mwingi kuwa nao kwenye maisha yako, hawajaja kwenye maisha yako kwa bahati mbaya, bali umewakaribisha wewe mwenyewe.
Hukujikuta tu upo katikati ya watu fulani ambao wana tabia fulani, bali wewe mwenyewe uliwavutia watu hawa mpaka wakafika kwenye maisha yako. uliwavuta na kuwakaribisha kwako kwa kujua au kutokujua. Wewe ndiye uliyewaruhusu waje na kuwa karibu na wewe kwenye maisha yako, sio wao wenyewe waliopanga kuja.
Ni muhimu sana kulijua hili ili tuweze kubadili maisha yetu. Kwa sababu tumekuwa tunajifunza mara nyingi kwamba wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Yaani tabia zako, mienendo yako na hata mafanikio yako kwenye maisha hayatakuwa tofauti na wale watu watano wa karibu sana kwako.
Hili ni eneo muhimu sana la kuangalia kwenye safari yako ya mafanikio, kama unataka kujua utafanikiwa kwa kiwango gani, waangalie kwanza wale wanaokuzunguka, maana huwezi kwenda mbali sana kuliko wao.
Unawakaribishaje watu hao wanaokuzunguka?
Unawakaribisha kwa kukubaliana na yale wanayofanya na namna wanavyoendesha maisha yao. Kwa kifupi unakubaliana na tabia zao na kuona siyo mbaya sana. Hivyo na wewe unaathirika na tabia walizonazo. Kama usingekuwa unakubaliana nao kwenye mambo wanayofanya, ukaribu wenu usingedumu.
Kama watu wanaokuzunguka siyo waaminifu, hii ni kwa sababu wewe mwenyewe siyo mwaminifu, au hujali kuhusu uaminifu. Mtu anaweza kufanya jambo lisilo la uaminifu na usisumbuke naye. Lakini kama wewe ni mwaminifu na unathamini sana uaminifu, utasisitiza uaminifu kwenye kila jambo, wale ambao siyo waaminifu hawatafurahia hili na hivyo watakaa mbali na wewe.
Tunawavutia watu kuwa karibu na sisi kutokana na tabia tunazozipenda au tunazoweza kuzivumilia.
Ni wakati sasa wa kuwamulika wale wanaotuzunguka na kuona kama wana vigezo vya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, kama hawana vigezo hivyo jiangalie umewakaribishaje.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hivi Ndivyo Unavyowapa Watu Wengine Ruhusa Ya Kukuumiza Wewe.
Uzuri ni kwamba ili kuwafukuza wale ambao hawaendani na wewe, huhitaji kugombana nao, bali unahitaji kujali yale ambayo ni ya muhimu kwako, na taratibu wataanza kukaa mbali na wewe.
Tengeneza mahusiano bora yatakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa. Ni heri kuwa na mahusiano machache ambayo yana msaada kwako kuliko kuwa na mahusiano mengi ambao ni mzigo kwako.
TUPO PAMOJA,
KOCHA MAKIRITA AMANI.
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)